• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
MAKALA MAALUM: Amekataa jinsia na ulemavu kuua ndoto yake ya udiwani

MAKALA MAALUM: Amekataa jinsia na ulemavu kuua ndoto yake ya udiwani

NA KENYA NEWS AGENCY

AJALI inapotokea, maisha ya mtu huweza kubadilika kwa namna ambayo hakutarajia.

Hayo ndiyo yaliyompata Mercy Jelagat, 24, kutoka kijiji cha Kapkeben, Kaunti ya Nandi.

Bi Jelagat alihusika katika ajali barabarani alipokuwa akielekea Kaunti ya Kisii mnamo Septemba 2018 kufanya kozi ya miezi mitatu.

Kutokana na ajali hiyo, Bi Jelagat alipata majeraha ya uti wa mgongo na kumfanya kukosa uwezo wa kutembea. Hadi sasa anatumia kiti cha magurudumu.

Miaka mitano baadaye, sasa Bi Jelagat ana nia ya kuwania kiti cha udiwani katika wadi ya Kaptumo Kaboi katika uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Akisimulia yaliyompata siku ya ajali, Bi Jelagat ambaye alihitimu kutoka Taasisi ya kiufundi ya Lessos mwaka 2021, anasema kuwa ajali hiyo haikumfanya akate tamaa maishani kwani bado anaamini kuwa ndoto yake ya kuwa kiongozi itatimia.

“Ikiwa mtu ana nia ya kuleta mabadiliko ulimwenguni, sharti abadilishe jamii yake kwanza. Hii ndiyo maana nimeamua kuwania kiti cha udiwani ili nilete mabadiliko kwa watu wetu,” akasema Bi Jelagat.

Akiwa amejawa na maono na ndoto tele, Bi Jelagat anasema hataruhusu ulemavu wake kumzuia kuwania kiti hicho cha udiwani kwani ana imani kuwa atashinda.

Anatumia kiti chake cha magurudumu kutembea kila upande wa kijiji chao kutafuta wafuasi watakaompigia kura katika uchaguzi wa Agosti 9.

Bi Jelagat ambaye ni kifunguamimba katika familia yake, anasema kuwa watu wanaoishi na ulemavu nchini mara nyingi hawapewi nafasi sawa serikalini na wanaonekana kama watu wasiojiweza na ananuia kubadili kasumba hiyo.

“Niliamua kuwania kiti cha udiwani ili kuondoa kasumba miongoni mwa watu wetu kuwa wanaoishi na ulemavu hawawezi kuongoza,” akasema Bi Jelagat.

“Sijapungukiwa bali nina kipawa. Wengine wataniona kama mtu aliyepungukiwa ila mimi najiona kama mtu mkamilifu na anayejiweza. Nitautumia ulemavu wangu ili kuwapa changamoto watu wengine kama mimi ambao wanaogopa kuwa katika nafasi za uongozi.”

Alisema nia yake kuu ya kuwania kiti hicho ni kuleta mabadiliko kwa wadi yake kwa kuwa imeachwa nyuma kimaendeleo.

“Viongozi wetu mara nyingi hawatushughulikii. Tuko nyuma sana kimaendeleo. Hii ndio maana nimeamua kuwania kiti cha udiwani ili hata sisi tufurahie maendeleo kama watu wengine,” akasema Bi Jelagat.

Baada ya mahojiano aliabiri bodaboda ili kuendeleza kampeni zake za kila siku.

Bi Jelagat alizindua kampeni zake miezi mitatu iliyopita na umaarufu wake katika eneo hilo unaendelea kuimarika.

Atapambana na wanasiasa wengine watano ambao pia wana nia ya kuwania kiti hicho.

Miongoni mwao ni mwanasiasa David Koech ambaye ni kiongozi wa wengi katika bunge la Kaunti ya Nandi.

“Sina uoga wowote kwa kuwa najua Mungu atanitetea. Nitaendeleza kampeni zangu bila kutishwa na mwanasiasa yeyote,” akasema Bi Jelagat.

Japo Bi Jelagat yuko miongoni mwa kikundi kinachochukuliwa kuwa kinahitaji usaidizi nchini, alisema kuwa hali yake haitakuwa kikwazo kwake kutimiza ndoto yake.

Kwa upande mwingine, aliwaomba wananchi waangazie sifa na uwezo wa mwanasiasa badala ya kuegemea hali na maumbile yake.

“Nikifanya kampeni zangu, wengine wananikaribisha vizuri huku wengine wakinihurumia. Hata hivyo, huwa nakaza macho ili nisiruhusu huruma zao zinivunje moyo. Watu wanafaa kujua kuwa hata watu wanaoishi na ulemavu wanapopewa nafasi za uongozi wanafanya kazi nzuri,” akasema Bi Jelagat.

Hata hivyo, anaeleza kuwa safari yake haijakuwa rahisi kutokana na uhaba wa pesa za kufanyia kampeni na kukosa uwezo wa kuzunguka kila eneo la wadi kutangaza azma yake.

Bi Jelagat ni miongoni mwa watu watatu wanaoishi na ulemavu ambao wametangaza nia yao ya kuwania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi ujao katika Kaunti hiyo ya Nandi.

Msimamizi wa wanaoishi na ulemavu katika kaunti hiyo, Daniel Kogo, alitoa wito kwa wananchi na hata serikali kuwakubali watu kama hao na kuwapa nafasi za uongozi.

Alisema kuna haja wananchi wawachague watu kama hao badala ya kungoja wateuliwe katika nafasi hizo.

“Kama jamii, tunafaa kuwatazama watu wanaoishi na ulemavu kama watu wakamilifu na wenye uwezo wa kuongoza nchi. Kadhalika, tunafaa kuelewa kuwa kuishi na ulemavu hakifai kuwa kikwazo kwa mtu kutimiza ndoto zake,” akasema Bw Kogo.

Alitoa wito kwa watu wote wanaoishi na ulemavu nchini wasikate tamaa bali waendelee kuandama ndoto zao.

“Endelea kufanya kile ukipendacho. Hali yako isikuwekee kikwazo kutimiza ndoto zako,” akashauri Bw Kogo.

You can share this post!

Polisi Rabai wasema sababu za kihistoria zinachangia mauaji...

Wanawake wapata pigo kuwania viti vikuu vya kisiasa Pwani

T L