• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Wanawake wapata pigo kuwania viti vikuu vya kisiasa Pwani

Wanawake wapata pigo kuwania viti vikuu vya kisiasa Pwani

LUCY MKANYIKA NA KALUME KAZUNGU

MATUMAINI ya wanawake wengi kuwania ugavana Pwani katika uchaguzi ujao yameanza kudidimia, baadhi yao wakilalamika kuhangaishwa katika vyama vyao.

Wanawake ambao wameonyesha nia ya kuwania ugavana katika ukanda huo ni Naibu Gavana Fatuma Achani (Kwale), Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa (Kilifi), mwanahabari Patience Nyange (Taita Taveta), na mwanaharakati wa masuala ya kiafya Umra Omar (Lamu).

Awali, Mbunge wa Likoni Mishi Mboko aliashiria kujaribu bahati yake kwenye kinyang’anyiro cha ugavana Mombasa, lakini akabadili nia.

Bi Achani na Bi Jumwa, ambao pia wanamezea mate kiti cha ugavana kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA), wameonekana kupata uungwaji mkono chamani.

Bi Nyange amekuwa wa hivi karibuni kulalamikia kuhangaishwa katika chama cha Wiper, ambapo inasemekana kuna mpango wa kumpa aliyekuwa seneta Bw Dan Mwazo tikiti ya ugavana katika uchaguzi ujao.

Mtaalamu huyo wa mawasiliano alidai kwamba amekuwa akipigiwa simu na maafisa wa chama ili awe mgombea mwenza wa Bw Mwazo, au awanie wadhifa wa Mbunge Mwakilishi wa Kike.

Aliongeza kuwa, mkutano ulifanywa wiki jana ambapo iliafikiwa kwamba kutakuwa na mashauriano au kura ya maoni ili kupata mgombea mashuhuri zaidi chamani.

“Nitakubali tu (uamuzi wa kumteua Mwazo) kama watanionyesha matokeo ya utafiti huo. Nasubiri mawasiliano rasmi kutoka kwa chama, na wakikosa kufanya hivyo nitaondoka Wiper,” akahoji.

Katibu Mkuu wa Wiper katika kaunti hiyo, Bw Peter Shambi, alithibitisha chama kilifadhili kura ya maoni iliyobainisha Bw Mwazo kuwa maarufu kuliko wenzake, lakini uamuzi wa mwisho haujafanywa.

Wiki iliyopita, Bi Umra alieleza kuwa alihama UDA baada ya kuona hangetendewa haki.

Uamuzi wake ulikujia baada ya kubainika kuwa muungano wa Kenya Kwanza, unaojumuisha UDA, unampendelea aliyekuwa gavana Bw Issa Timamy wa ANC – iliyo pia katika Kenya Kwanza – kupeperusha bendera ya muungano huo uchaguzini.

Bw Timamy ni mwanachama wa ANC.Amani National Congress (ANC), ambacho pia ni chama tanzu cha Kenya Kwanza.

Hata hivyo, Bi Umra aliapa kusonga mbele na azimio lake la kushindania ugavana Lamu kupitia chama kingine.

“Mimi hainishtui wala kunivunja moyo katika azma yangu ya kutafuta kiti cha ugavana wa Lamu. Tuko mashinani sasa. Kampeni tumezifanya na tunaendelea nazo. Tutapatana debeni,” akasema.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Amekataa jinsia na ulemavu kuua ndoto yake...

Siri za ukora ndani ya mtaa wa Makutano ulioko kaunti ndogo...

T L