• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
MAKALA MAALUM: Jinsi Ruto anavyopanga kuuzima umaarufu wa marehemu Moi

MAKALA MAALUM: Jinsi Ruto anavyopanga kuuzima umaarufu wa marehemu Moi

NA ERIC MATARA

ALIYEKUWA Rais wa Kenya hayati Mzee Daniel Arap Moi alitawala kwa miaka 24 huku akionyesha ubabe, kwenye serikali yake na kuamua hata mrithi wake.

Miaka miwili baada ya kifo cha chake, hadhi yake kisiasa bado inadhihirika.Wakati wa kifo chake, tayari alikuwa amehakikisha kuwa wanawe wawili Gideon Moi na Raymond Moi walikuwa serikalini huku Gideon Moi akiwa seneta wa Kaunti ya Baringo na Raymond kuwa Mbunge wa Nakuru-Rongai.

Hata hivyo, chini ya miezi minne kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022, Naibu Rais William Ruto, ambaye ni mpinzani mkuu wa Moi, anaonekana kuwa amebuni mkakati wa kukomesha uongozi na umaarufu wa Mzee Moi na ushawishi wa chama cha KANU katika Kaunti za Nakuru na Baringo.

Tayari, chama cha United Democratic Movement (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto, kimewadhamini wagombeaji katika viti mbalimbali vya ubunge na seneti huko Kaunti za Nakuru na Baringo kukabiliana na Kanu.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema ushawishi wa kitambo wa Moi katika Kaunti za Nakuru na Baringo unakabiliwa na mzozo mkubwa kutoka kwa chama cha UDA.

“Mbunge wa Naibu wa Rais amevamia Nakuru na Baringo ambayo zamani ilijulikana kuwa ngome ya Moi na kusimamisha wagombea wa UDA. Dkt Ruto ana nia ya kudhibiti maeneo hayo mawili kama sehemu ya ngome ya kisiasa ya Bonde la Ufa,” Mwanasheria na mchambuzi wa kisiasa Steve Kabita akasema.

Imebainika kuwa Dkt Ruto amebuni mpango mkuu wa kuwafungia vijana wa Moi wote au na miradi yao katika kaunti za Nakuru na Baringo.

“Chama cha UDA kinalenga kusimamisha wagombeaji wenye nguvu huko Rongai na Baringo ili kupunguza ushawishi wa Moi baada ya 2022. Tunataka kuhakikisha kuwa viongozi wote waliochaguliwa Nakuru na Baringo ni wa chama cha UDA katika uchaguzi wa Agosti,” akasema mmoja wa wafuasi wa Naibu Rais, ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Katika eneobunge la Rongai kwa mfano, kifungua mimba wa marehemu Rais Moi, Bw Raymond Moi anatarajiwa kukabiliana na mgombea wa UDA.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema, kinatazamiwa kuwa kinyang’anyiro hicho kati ya wawili hao huenda kikazua utata.

“Raymond Moi lazima aimarishe umaarufu wake ili kushikilia kiti chake, kwa sababu uhusiano wa baridi kati ya familia ya Mzee Moi na Dkt Ruto unaweza kutatiza mambo kwake. Bw Raymond atalazimika kukesha ili kupanga mkakati wa kupata ushindi huku wimbi la UDA likiendelea katika Bonde la Ufa,” wakili na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Steve Kabita aliliambia Taifa Leo.

UDA inatazamiwa kuwasilisha mmoja wa wagombea watano wanaomezea mate tikiti ya UDA katika eneobunge la Cosmopolitan.

Marudio

Marudio ya kura za mchujo za UDA yamepangwa Jumanne, baada ya zoezi hilo kukumbwa na matatizo wiki iliyopita.

Katika uteuzi wa UDA katika eneobunge la Rongai, Bw Paul Chebor, aliyekuwa Diwani wa Solai aliibuka mshindi katika mchujo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Katika matokeo hayo yaliyozozaniwa, Chebor alipata kura 8,428 huku mpinzani wake wa karibu Raymond Komen akipata kura 7,973, tofauti ya kura 1,055.

Wagombea wengine watatu walipata kura chini ya 500.

Hata hivyo, Raymond Komen aliyakataa matokeo hayo akidai yalikuwa ya udanganyifu na matatizo mbalimbali ikiwemo ujazaji wa masanduku ya kura na kubadilisha takwimu kwenye fomu zilizosainiwa na mawakala wake.

“Ninakataa matokeo kwa sababu ni ya udanganyifu na hayakubaliki, nataka kura zirudiwe,” Bw Komen aliteta katika Sekondari ya Kirobon, kituo cha kuhesabia kura cha eneobunge Ijumaa iliyopita kabla ya kuondoka kwa kishindo.

Baada ya kutathmini madai hayo, Bodi ya Taifa ya Uchaguzi ya UDA sasa imeagiza kurudiwa kwa zoezi hilo.

Kanu imeshinda kiti hicho mara nne tangu ilipoondolewa katika eneobunge kubwa la Nakuru Kaskazini – sasa Subukia – mwaka 1988.

Mchambuzi mwingine wa masuala ya kisiasa, Jesse Karanja alisema kuwa wana wa hayati Moi bado wana ushawishi mkubwa katika siasa za kaunti za Nakuru na Baringo kwa sasa na haitakuwa rahisi kwa chama cha UDA kupata ushindi.

“Ni lazima wafanye bidii kuzima ushawishi wa Kanu katika maeneo hayo.”

Raymond Moi alishinda kiti hicho mwaka wa 2013 kwa tiketi ya Kanu.

Siasa za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta za 2022 pia zinatarajiwa kuwa sababu kuu katika kinyang’anyiro cha Rongai.

Katika mpango mkuu wa kufifisha ushawishi wa familia ya Daniel arap Moi huko Nakuru na Baringo, Naibu Rais sasa anatafuta mgombeaji shupavu ili kumng’oa kiongozi huyo kijana wa Moi.

Eneobunge hilo ni la watu wengi na lina jamii kadhaa za wachache zikiwemo Waluo, Wakisii, Waluhya, Waturkana na Wakamba, wanaofanya kazi katika mashamba ya Mzee Moi, huku wengine wakinunua ardhi na kuishi katika eneobunge hilo.

“Wagombea watalazimika kuunganisha kura kutoka kwa jamii za wachache. Wagombea wanapaswa kuwapigia debe kwani wanaunda asilimia 25 ya wapiga kura katika eneo hilo,” akaongeza Bw Karanja.

Kwa upande wake, Raymond Moi, ambaye anawania kiti hicho kwa mara ya pili alinukuliwa akisema hakuna mgombeaji anayeweza kumng’oa mamlakani Rongai.

Kujiamini

Bw Raymond hapo awali alijiamini kuwa atashinda kiti hicho.

“Kwa hivyo baadhi ya watu wanafikiri wanaweza kuja kugombea dhidi yangu 2022, Wasipoteze muda na rasilimali zao. Nitawashinda jinsi nilivyowashinda 2013 na 2017,” akasema Bw Raymond.

Kwa muda wa miaka 10 iliyopita, Dkt Ruto amekuwa akiendesha maonyesho katika eneo hili, akijaribu kumsukuma Seneta Gideon Moi, mwenyekiti wa Kanu, hadi pembezoni, lakini mabadiliko ya hivi majuzi ya kisiasa yaliyoongozwa na Rais Kenyatta kitaifa yamempandisha cheo seneta huyo na kumpa ushawishi zaidi kisiasa.

Katika eneo la Bonde la Ufa, kitindamimba wa Moi, ambaye anamuunga mkono Raila Odinga, amekuwa na mapambano ya muda mrefu na Dkt Ruto, kutaka kudhibiti eneo hilo kabla ya Agosti 9.

Kijana huyo wa Moi pia amekuwa akilengwa na wawaniaji wengine kadhaa wa kisiasa, wakati mabadiliko ya kisiasa ya 2022.

Uhusiano mkubwa kati ya familia ya Moi na Kenyatta, ambao ulianza miaka ya 1960, pia umekuwa na manufaa kwa Seneta Moi, huku Uhuru akionekana kumleta katika mipango yake ya urithi.

Urafiki wake wa muda mrefu na Uhuru, ambao ulianzia enzi zao wakiwa wanafunzi katika Shule ya St Mary’s, Nairobi mwishoni mwa miaka ya 1970, umekuja kwa manufaa ukiwa umeimarishwa na uhusiano mkubwa unaozifunga familia za Kenyatta na Moi.

Wakati wa mazishi ya Mzee Moi, Februari 2020, seneta wa Baringo alikabidhiwa mfano wa fimbo ambayo ilikuwa sawa na utawala wa miaka 24 wa babake, kuashiria jukumu lisiloweza kuepukika kwake sio tu kufufua Kanu bali pia kuirejesha.

  • Tags

You can share this post!

Capwell yaendelea kujizolea umaarufu Ligi ya Kanda ya Kati

Raila na Ruto kuamua gavana ajaye wa Meru

T L