• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Raila na Ruto kuamua gavana ajaye wa Meru

Raila na Ruto kuamua gavana ajaye wa Meru

NA GITONGA MARETE

HUENDA Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga wakaamua yule atakayeibuka mshindi kwenye kinyang’anyiro cha ugavana katika Kaunti ya Meru kwenye uchaguzi wa Agosti.

Wawaniaji watatu wakuu kwenye kivumbi hicho ni Gavana Kiraitu Murungi, Seneta Mithika Linturi na Mwakilishi wa Kike, Bi Kawira Mwangaza.

Bw Murungi anatetea nafasi hiyo kwa tiketi ya chama chake cha Devolution Empowerment Party (DEP), Bw Linturi kwa tiketi ya chama cha UDA, huku Bi Mwangaza akiwania kwa tiketi ya chama cha The Independent Party (TIP).

Jumapili, Bw Linturi alimtangaza wakili Linda Kiome kutoka eneo la Imenti Kaskazini kuwa mgombea-mwenza wake, kwenye hatua inayotajwa kuwa mwanzo rasmi wa makabiliano makali ya kisiasa kati ya vigogo hao watatu.

Hata hivyo, huenda matokeo ya kinyang’anyiro hicho yakaamuliwa na Bw Odinga (anayewania urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja) na Dkt Ruto, anayewania kwa tiketi ya chama cha UDA.

Kaunti hiyo ina jumla ya wapigakura 780,858 waliosajiliwa.

Kulingana na Prof Gitile Naituli, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, huenda umaarufu wa Bw Murungi ukaathiriwa vibaya na ushirika wake wa karibu na Bw Odinga.

Anasema kuwa Dkt Ruto ana ufuasi mkubwa katika kaunti hiyo ikilinganishwa na Bw Odinga.

“Kimekuwa ni kibarua kigumu kwa wanasiasa wengi kumfanyia kampeni Bw Odinga katika eneo la Mlima Kenya, hasa eneo la Meru. Bw Murungi yuko hatarini kupoteza umaarufu wake,” akasema Prof Naituli hapo jana Jumanne, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Hata hivyo, alisema kuwa kuna uwezekano Bw Murungi bado akadumisha umaarufu wake kutokana na tajriba yake kubwa ya kisiasa.

Mdadisi huyo alieleza wapigakura wengi wanahisi kuwa kwa kuraiwa kumuunga mkono Bw Odinga, wanashurutishwa kupiga kura kwa kuzingatia mrengo fulani wa kisiasa.

Alisema hilo ni miongoni mwa masuala makuu ambayo Bw Murungi anapaswa kuzingatia wakati kampeni zitakapoanza rasmi hapo Mei.

Tangu Bw Murungi kutangaza kumuunga mkono Bw Odinga, amekuwa akikumbana na upinzani kutoka kwa wapigakura.

Ni hali ambayo wakati mwingine imemlazimu kujitenga na Bw Odinga.

Majuzi, Bw Murungi alisema kuwa hatua yake kumuunga mkono Bw Odinga haimaanishi anawalazimisha wenyeji kumpigia kura.

“Nilisema kuwa mimi na mke wangu tutampigia kura Bw Odinga. Hata hivyo, sijamlazimisha yeyote kumuunga mkono. Hata ikiwa ni Raila ama Ruto atakayechaguliwa kuwa rais, bado nitapata mgao wangu wa fedha kama gavana kuiendesha kaunti,” akasema, alipokuwa akifanya kampeni katika eneo la Mikinduri, Tigania Mashariki.

Kwa Bw Linturi, wadadisi wanasema kuwa uhusiano wake wa karibu na Dkt Ruto huenda ukampa umaarufu mkubwa ikilinganishwa na wagombeaji wengine.

  • Tags

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Jinsi Ruto anavyopanga kuuzima umaarufu wa...

Kampuni za ushonaji nguo zapiga hatua kiteknolojia kilimo...

T L