• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Mapinduzi ndani ya Jubilee ni haramu – Kioni

Mapinduzi ndani ya Jubilee ni haramu – Kioni

NA RICHARD MUNGUTI

KATIBU Mkuu wa chama cha Jubilee (SG) kinachokumbwa na utata wa uongozi Bw Jeremiah Kioni ameomba jopo la kuamua mizozo ya vyama vya kisiasa (PPDT) liharamishe mabadiliko ya uongozi chamani humo yaliyotokana na mkutano ulioitishwa na kuandaliwa na naibu wake Joshua Kutuny.

Bw Kioni alieleza jopo hilo linaloongozwa na wakili Desma Nungo kwamba Katiba ya Jubilee inatambua tu mikutano iliyoandaliwa na Katibu Mkuu (SG).

Hivyo basi, Bw Kioni kupitia kwa wakili Mbuthi Gathenji, alieleza jopo hilo kwamba teuzi za mbunge maalum Sabina Chege na Bw Kanini Kega kutwaa uongozi wa Jubilee hazina mashiko kisheria.

“Sheria haiwatambui Kega na Chege kuwa viongozi halisi wa Jubilee. Walipaa uongozini kwa njia ya mkato na inafaa wapokonywe mamlaka hayo bandia,” Bw Gathenji alieleza PPDT.

Bw Gathenji pamoja na wakili Jackson Awele wanaomwakilisha Bw Kioni walieleza jopo hilo mapinduzi hayo ya uongozi wa Jubilee yanastahili kufutiliwa mbali na uongozi halisi kurejeshwa chamani.

Mawakili hao walieleza jopo hilo kuwa uteuzi wa Bi Chege kuwa kiongozi mpya wa Jubilee na Bw Kega kuwa SG umepotoka na hautambuliki kisheria.

PPDT ilielezwa wakati wa mapinduzi hayo yaliyofanywa mjini Naivasha mnamo Februari 2023, Bi Chege alitwaa uongozi wa Jubilee badala ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta naye Bw Kega ambaye ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) akatwaa wadhifa wa SG.

“Naibu wa SG wa Jubilee Bw Kutuny hana mamlaka kisheria kuandaa mkutano wowote wa Jubilee,” Gathenji alieleza jopo hilo la PPDT.

Pia mawakili hao walilalamika Kioni hakupewa muda wa kujitetea dhidi ya madai kwamba anasimamia chama cha Jubilee kama mali yake binafsi.

Jopo hilo liliombwa lirejeshe utulivu ndani ya chama.

PPDT ilielezwa msajili wa vyama (RPP) Anne Nderitu amechangia katika mtafaruku ulioko ndani ya Jubilee kwa kutambua mrengo wa Chege na Kega huku akijua wamevunja sheria.

Kwa upande wao, Chege na Kega walitetea hatua ya kumtimua uongozini Bw Kioni na wenzake kwa utovu wa nidhamu.

Wiki iliyopita, jopo hilo lilifutilia mbali uteuzi wa Bi Chege na Bw Kega hadi kesi iliyoshtakiwa na Bw Kioni isikilizwe na kuamuliwa.

Jopo hilo lilimrejesha Bw Kioni uongozini.

Kusikilizwa kwa mzozo huo kulikamilishwa Alhamisi alasiri na arifa ya uamuzi itapelekwa kwa mawakili.

Kwa sasa ni Bw Kioni anayefaa kuendeleza masuala ya Jubilee.

  • Tags

You can share this post!

Wafuasi wa Jicho Pevu wakabiliana na wenzao wa Hassan Omar

Kocha Rafael Benitez apokezwa mikoba ya kunoa Celta Vigo ya...

T L