• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mbunge amrukia Joho akidai hajawafaa raia ila kujipenda tu

Mbunge amrukia Joho akidai hajawafaa raia ila kujipenda tu

NA WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Changamwe, Bw Omar Mwinyi amemkashifu Gavana Hassan Joho kwa kutowajibika kuhakikisha wakazi wa Mombasa wananufaika na Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) bila malipo na elimu.

Akiongea kwenye mdahalo wa wawaniaji wa ubunge eneobunge la Changamwe, Bw Mwinyi alisema wakazi wa Mombasa wanateseka sababu ya gharama ya afya na ukosefu wa basari.

Bw Mwinyi anayedaiwa kukosana na Gavana Joho alisema serikali ya Kaunti inapokea fedha kutoka kwa serikali kuu ilhali wanafunzi wanakosa basari na kukosa elimu wakilazimika kuacha shule.

Wakati huo huo, Bw Mwinyi alitakiwa aeleze mtoto wake wa kiume alipataje kazi kama mwenyekiti wa kamati ya hazina ya Uwezo Fund.

Bw Omar alisema mwanawe ni mkazi wa Changamwe na alichaguliwa na wakazi kuwa mwenyekiti.

“Sioni shida hapo, bora anafanya kazi vizuri na hakuna ufisadi. Ni lazima serikali ya Kaunti ya Mombasa ikunje mashati iwajibike ili wananchi wasiteseke kwa sababu ina pesa na haitumii kwa wananchi katika bima ya afya wala basari. Kaunti hii ina Sh12 bilioni na eneobunge lina Sh137 milioni. Basari zetu zinaonekana lakini za kaunti hazionekani,” akasema Bw Omar.

Alisema wakazi wa Mombasa watachanganua bajeti ya Kaunti ya Mombasa. Aliisihi serikali kuu ipandishe daraja hospitali ya wilaya ya Port Reitz na ichukue uendeshaji wake.ma bora wakazi wa Changamwe wanufaike na kuboreshwa kwa afya.

“Tatizo kubwa la Mombasa ni elimu na afya swala ambalo serikali ya kaunti haijawajibika. Mombasa itaendelea kuzora endapo serikali ya kaunti haitowajibika,” alisema.

Bw Mwinyi alisema ukosefu wa ajira Mombasa ni kufuatia kufungwa kwa viwanda.

Kwenye mdahalo wa ubunge wapiga kura waliwataka wagombea hao kueleza watakachokifanya watakapoingia uongozini wakizingatia sekta ya elimu, taka, afya, ukosefu wa ajira.

“Changamwe inahitaji shule nyingi zaidi hasa za watoto walemavu ambao wametengwa sana. Nitahakikisha tunawapeleka wale waliohitimu shule za ufundi na wapate ajira,” alisema Mwidini Shee, mwaniaji.

Alisema amepata ufadhili wa elimu ya bure kwa wafadhili wa kimataifa ambao wameapa kuwasaidia wanafunzi wa Changamwe.

Mwaniaji mwingine Bw Munyoki Kyallo (Wiper) alisema atashirikiana na washika dau kuhakikisha kila mtoto anaenda shule eneo la Changamwe.

Bw Kyallo alijipata pabaya baada ya wapiga kura kumtaka kueleza wakazi wa Mombasa maendeleo aliyoyaleta alipokuwa waziri katika baraza la Gavana Joho.

“Nikiwa waziri niliweza kuhakikisha timu za voliboli na basketiboli zinapata mipira na jezi,” alisema.

Bw Abdi Daib (Jubilee) aliwasihi wakazi kumuunga mkono ili alete mageuzi kama alivyofanya mbunge wa zamani marehemu Ramadhan Kajembe.

“Alikuwa akibisha kila kiwanda na kupeleka watoto wetu wa Changamwe kazi. Nitafuata mkondo huo huo,” alisema Bw Daib.

  • Tags

You can share this post!

WANTO WARUI: Shule za kibinafsi za sekondari za chini...

Wagombeaji elfu 14 kuanguka Agosti 9

T L