• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Wagombeaji elfu 14 kuanguka Agosti 9

Wagombeaji elfu 14 kuanguka Agosti 9

NA LEONARD ONYANGO

WAGOMBEAJI viti 14,216 wanangojewa na majuto Agosti 9 kwani sharti wapoteze kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Kulingana na orodha ya wawaniaji walioidhinishwa na Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC), jumla ya wawaniaji 16,098 watang’ang’ana kushinda viti 1,882 vya urais, ubunge, useneta, ugavana, mwanamke mwakilishi na udiwani.

Hii inamaanisha kuwa wawaniaji 14,216 lazima watashindwa licha ya kutumia mamilioni katika kampeni.

Idadi kubwa zaidi ya watakaoenda nyumbani mikono mitupu itakuwa miongoni mwa wawaniaji wa udiwani, kwani 12,985 wameidhinishwa kuwania viti 1,450 vilivyopo, hivyo 11,535 wanafanya kampeni za bure.

Katika kinyang’anyiro cha urais, wagombeaji watatu kati ya William Ruto, Bw Raila Odinga, George Wajackoyah na Mwaure Waihiga wanapoteza muda wao na pesa wakijipigia debe.

Katika viti vya ubunge, wawaniaji 2,098 wamejitosa ulingoni kusaka viti 290 huku wengine 385 wakisaka nafasi 47 za useneta.

Wawaniaji 359 nao wanasaka viti 47 vya mwanamke mwakilishi na wengine 267 viti vya ugavana katika kaunti 47.

Ripoti iliyotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Maendeleo (IDS) mnamo Juni 2022, inaonyesha kuwa mwaniaji anahitaji angalau Sh39 milioni kuendesha kampeni ili kuwa na uhakika ya kushinda useneta.Ili kuwa na nafasi nzuri ya kushinda uwakilishi wa wanawake, mwaniaji anahitaji kutumia angalau Sh24 milioni, kwa mujibu wa utafiti wa IDS.

PIGO KUBWA

Mwaniaji wa ubunge anahitaji Sh22.2 kuwa na nafasi ya kushinda kiti hicho, naye mgombea wa udiwani anahitaji Sh3.1 milioni ili kuendesha kampeni kabambe ya kushtua wapinzani wake katika wadi.

IDS inasema kuwa ili kuwa na nafasi bora ya kushinda, mwaniaji wa ugavana anahitaji angalau Sh100 milioni.

Mwaka 2021 IEBC ilikuwa imependekeza kuwa kila mwaniaji wa urais atumie Sh4.4 bilioni kwenye kampeni. Lakini kampeni za urais za mwaka huu huenda zikawa ghali zaidi ikilinganishwa na chaguzi zilizopita.

Hii inatokana na ukweli kwamba wawaniaji wa urais wanaandamana na hadi zaidi ya helikopta 10 katika mkutano mmoja wa kisiasa.

Baadhi ya watakaoanguka uchaguzi wa Agosti 9 pia watapatwa na pigo kubwa haswa ikizingatiwa kuwa walijiuzulu nyadhifa zao kutoka serikalini kujaribu bahati katika siasa.

Uwezekano wa watakaopoteza uchaguzi ujao kuteuliwa kuwa wabunge, maseneta au madiwani maalumu haupo kwani vyama vya kisiasa tayari vimetunuku nafasi hizo kwa waliopoteza katika mchujo na kupeleka orodha kwa IEBC.

Jumla ya wawaniaji 4,724 wanawania nyadhifa mbalimbali kwa tiketi ya kujitegemea. Idadi hiyo imeongezeka ikilinganishwa na 4,002 mnamo 2017.

Wakati huo huo, IEBC Jumapili ilichapisha katika Gazeti Rasmi la Serikali majina ya maafisa watakaosimamia uchaguzi katika kaunti zote 47 na vituo vya kujumlisha matokeo katika ngazi ya kaunti na maeneobunge yote 290.

Matokeo ya Kaunti ya Nairobi na Mombasa yatajumulishiwa katika jumba la KICC na Bandari Maritime Academy mtawalia.

Ajenti Mkuu wa Azimio, Saitabao Kanchory ameandikia barua IEBC akilalamika kuwa idadi kubwa ya maafisa wa kusimamia uchaguzi ngazi ya maeneobunge pamoja na manaibu wao wanatoka katika eneo la Bonde la Ufa.

Bw Kanchory alikuwa ametoa makataa ya hadi Julai 7 kwa IEBC kushughulikia malalamishi yao bila kuelezea hatua ambayo muungano huo unaoongozwa na Bw Odinga utachukua iwapo matakwa yao yatapuuzwa.

Malalamishi hayo ya muungano wa Azimio huenda yakawa miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati atakapokutana na wawaniaji wa urais kwa mara ya pili wiki ijayo.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge amrukia Joho akidai hajawafaa raia ila kujipenda tu

Kindiki, Muturi walalama Uhuru hana shukurani

T L