• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mchujo: Majeruhi wa UDA, ODM watoroka

Mchujo: Majeruhi wa UDA, ODM watoroka

NA WAANDISHI WETU

WAWANIAJI wengi walioshindwa kwenye chaguzi za mchujo zilizokamilika majuzi katika vyama vya UDA na ODM wameamua kuwania nyadhifa walizolenga kama wawaniaji huru.

Wengi wametaja hatua zao kuchangiwa na kutoridhishwa na matokeo ya chaguzi hizo, au maamuzi yaliyotolewa na vyama kuhusu wawaniaji wanaopaswa kuwania nyadhifa hizo.

Katika Kaunti ya Mombasa, mfanyabiashara Suleiman Shahbal jana Jumanne alishinikizwa na wafuasi wake awanie ugavana katika kaunti hiyo kama mwaniaji huru, baada ya ODM kutoa tiketi ya moja kwa moja kwa mbunge Abdulswamad Nassir (Mvita) kuwania nafasi hiyo.

Wafuasi hao waliokutana naye jijini Mombasa walisema wamempa siku moja kufanya uamuzi kuhusu pendekezo lao la kumtaka awanie huru.

Katika Kaunti ya Homa Bay, wawaniaji walioshindwa kwenye mchujo wa ODM wameungana dhidi ya walioshinda na kuwataka wakutane debeni kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Evans Kidero, ambaye tayari amehama ODM kuwania kama mgombea huru baada ya chama kumpa tiketi Mwakilishi Mwanamke, Gladys Wanga, amekuwa akiunganisha walioshindwa kwenye mchujo.

Anataka washirikiane na kuanza naye anapojaribu kumrithi Gavana Cyprian Awiti, anayeondoka ofisini baada ya kuhudumu kwa mihula miwili.

Wawaniaji Tom Okoth, Isaiah Oyoo, Evance Otieno, Vincent Matoka, Zachary Aseda na Isaiah Ondiek walisema uamuzi wao wa kuungana dhidi ya ODM unatokana na kutoelezwa mbinu iliyotumiwa kutoa tiketi kwa Bi Wanga.

Walisema hawatalalamika kwa jopo la kutatua mizozo la ODM, wakisema kufanya hivyo ni kuharibu wakati.

Katika Kaunti ya Kisumu, huenda aliyekuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki Ken Obura akalazimika kuwania ugavana kama mwaniaji huru, baada ya ODM kumkabidhi Gavana Anyang’ Nyong’o tiketi ya moja kwa moja.

Katika Kaunti ya Kiambu, Mbunge Patrick Wainaina (Jungle) wa Thika Mjini, alisema atawania ugavana katika kaunti hiyo kama mwaniaji huru, baada ya kutoridhishwa na matokeo ya mchujo wa chama cha UDA, ambapo Seneta Kimani Wamatangi alitangazwa kuwa mshindi.

Mbunge Patrick Wainaina (Jungle) wa Thika Mjini, alisema atawania ugavana katika Kaunti ya Kiambu kama mwaniaji huru, baada ya kutoridhishwa na matokeo ya mchujo wa chama cha UDA. PICHA | MAKTABA

Kwenye matokeo yaliyotolewa na chama hicho, Bw Wamatangi alizoa kura 86,020 ikilinganishwa na Bw Wainaina aliyepata kura 50,446.

“Kulikuwa na uhongaji wa wapiga kura katika karibu vituo vyote. Wasimamizi wa uchaguzi waliagizwa kuupendelea upande mmoja. Licha ya hayo, ninawahakikishia wafuasi wangu kwamba nitakuwa kwenye debe,” akasema Bw Wainaina.

Katika kaunti hiyo hiyo, mwanamuziki Loise Kim ameamua kuwania nafasi ya Mwakilishi Mwanamke kama mwaniaji huru, baada ya kueleza kutoridhishwa na hatua ya maafisa wa uchaguzi wa UDA kumtangaza Bi Anne Muratha kuwa mshindi wa tiketi hiyo.

Kwenye matokeo yaliyotolewa, Bi Muratha alizoa kura 83,257 dhidi ya Bi Kim aliyepata kura 67,644.

Katika Kaunti ya Embu, Seneta Njeru Ndwiga alitangaza kuwa atawania ugavana kama mwaniaji huru baada ya kushindwa na Mbunge Maalum Cecily Mbarire kwenye uteuzi wa UDA.

Bw Ndwiga ni miongoni mwa vigogo wa kisiasa kutoka eneo la Mlima Kenya Mashariki waliohamia katika chama hicho majuzi.

Katika Kaunti ya Meru, mchekeshaji Jasper Muthomi (MC Jessy) amesema kuwa atawania ubunge katika eneo la Imenti Kusini, baada ya kuraiwa na Naibu Rais William Ruto kumuunga mkono Bw Mwiti Kathaara.

Mcheshi huyo alikuwa ameahidiwa kazi katika Sekretariati ya Kampeni ya Dkt Ruto.

Hata hivyo, alisema aliraiwa na wazee kurejea kwenye kinyang’anyiro hicho.

“Nimelazimika kurejea kinyang’anyironi baada ya kuitwa na wazee walionipa baraka kuwania nafasi hiyo,” akaeleza.

Wakati huo huo, Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) na Bunge la Kitaifa, jana Jumanne ziliagizwa na Mahakama Kuu kujibu mashtaka kwenye kesi ambayo imewasilishwa na wagombea huru wakitaka kuruhusiwa kubuni chama chao wenyewe.

Jaji Anthony Mrima aliliagiza bunge, ORPP na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kujibu maswala yaliyoibuliwa na zaidi ya wawaniaji 2,000 wanaolenga kugombea nyadhifa tofauti za kisiasa nchini.

Wawaniaji hao wanataka kuruhusiwa kusajili chama chao cha Free Kenya Initiative (FKI) ili kushughulikia malalamishi yao.

Wakili Danstan Omari alimwambia jaji huyo kwamba lengo kuu la chama hicho ni kuwa kama jukwaa ambapo wawaniaji huru watakuwa wakiwasilisha malalamishi yao.

Bw Omari akishirikiana na mawakili Litty Kathurima na Michelle Omwoyo waliwasilisha stakabadhi za kesi hiyo kwa taasisi hizo tatu Aprili 13, ijapokuwa hazijatoa majibu yoyote.

Wawaniaji hao wanadai kuwa na udhibiti wa asilimia 56 ya wapigakura nchini.

Ikiwa chama hicho kitasajiliwa, kitakuwa muungano wa tatu mkubwa wa kisiasa, baada ya Azimio-One Kenya, unaoongozwa na Raila Odinga na Kenya Kwanza, unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Ripoti ya Wanderi Kamau, George Odiwuor na Richard Munguti

You can share this post!

Mahakama yakataa kuharamisha sheria ya vyama vya kisiasa

Vurugu zasitisha mchujo wa PAA kukiwa na madai ya mapendeleo

T L