• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Migawanyiko Ukambani siasa zikinoga

Migawanyiko Ukambani siasa zikinoga

PIUS MAUNDU na CHARLES WASONGA

MIGAWANYIKO jana Jumatano iliendelea kujitokeza miongoni mwa viongozi wa kisiasa Ukambani huku kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akilaumiwa kwa kutotoa mwelekeo wa kisiasa kwa wakazi wa eneo hilo kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Gavana wa Kitui Charity Ngilu, alifeli kuhudhuria mkutano ulioitishwa kuunganisha viongozi wa eneo hilo mjini Machakos, hali iliyowaacha wengi vinywa wazi.

Hii ni licha ya kwamba, mkutano huo uliitishwa na yeye Bi Ngilu kwa ushirikiano na magavana Alfred Mutua (Machakos) na Kivutha Kibwana (Makueni).

Magavana Alfred Mutua (Machakos), Kivutha Kibwana (Makueni) na Charity Ngilu (Kitui). PICHA | MAKTABA

Japo msaidizi wa Bi Ngilu alisema mwanasiasa huyo alifeli kuhudhuria mkutano huo baada ya kuugua, duru ziliambia Taifa Leo kwamba ni baada ya gavana huyo wa Kitui kuzungumza na Bw Musyoka kwa njia ya simu, ndipo akaamua kutofika Machakos.

Wawili hao walizungumza wakati ambapo wanasiasa wengine wandani wa Bw Musyoka walieleza kuwa mkutano wa viongozi wa Ukambani, utafanyika Yatta, Jumamosi.

Wakiongozwa na Seneta wa Makueni, Bw Mutula Kilonzo Junior, wanasiasa hao walipuuzilia mbali madai kwamba mkutano wa Machakos ulilenga kupanga mikakati ya kumvua Bw Musyoka taji la kigogo wa siasa za Ukambani.

“Mheshimiwa Stephen Kalonzo Musyoka anasalia kiongozi mkuu wa kisiasa na msemaji wa eneo la Ukambani. Kwa hivyo, tungependa kuwaambia watu wanaotoa madai hayo kwamba wanadanganya,” seneta huyo akasema kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya Wiper, Karen, Nairobi.

Akaongeza: “Sisi ndio viongozi kutoka eneo hilo na tunawaeleza kuwa Kalonzo hatishwi na yeyote.”

Bw Kilonzo Junior ni kiranja wa wachache katika seneti.

Wanasiasa wa Ukambani wakiongozwa na Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior, wahutubia kikao cha wanahabari katika makao makuu ya Wiper mtaani Karen, Nairobi. PICHA | CHARLES WASONGA

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba Bw Musyoka alipinga mkutano wa Machakos akihofia kuwa ungesambaratisha ajenda ya mkutano wake wa Jumamosi, katika makazi yake ya Yatta.

“Kalonzo alitaka mkutano wa Machakos ufeli kwani ungevuruga mipango yake ya Jumamosi. Hii ndio maana alimpigia simu gavana Ngilu na kumshawishi asihudhurie,” akasema mwanasiasa mmoja wa Machakos ambaye aliomba tulibane jina lake.

Waliozungumza katika mkutano, wakiwemo madiwani na wawaniaji viti mbalimbali katika kaunti zote tatu, walimlaumu Bw Musyoka kwa kufeli kutoa mwongozo kwa wakazi.

Walisema wapigakura katika eneo hilo wamechanganyikiwa, wasijue ikiwa Bw Musyoka atawania urais au la, wakiongeza kuwa Bw Musyoka anaendeleza masilahi yake ya kibinafsi.

Wanasiasa hao walitisha kuunga mkono azma ya urais ya kiongozi wa ODM Raila Odinga au wadhamini mgombeaji wa urais kutoka eneo hilo.

“Mkutano wetu wa Jumamosi utatumiwa kujadili na kutoa mwelekeo kwa jamii yetu kuhusiana na mwelekeo wa siasa ambao tunatarajia kuchukua katika siasa za kitaifa” Seneta wa Kitui, Bw Enoch Wambua, alisema.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Chokoraa wangali tishio la usalama

Jubilee ingali imara wala haijafa, adai Mbunge Kanini Kega

T L