• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
Mimi mlemavu na Raila hata hajawahi kunipigania, Kigame ajibizana na Alai

Mimi mlemavu na Raila hata hajawahi kunipigania, Kigame ajibizana na Alai

Na WANGU KANURI

Mwimbaji wa nyimbo za Injili Reuben Kigame ameibua gumzo mtandaoni baada ya kumkashifu kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga kwa kuendeleza maandamano.

Bw Kigame kwa ujumbe wake kwa kinara huyo alimweleza kuwa iwapo angependa kuwasaidia Wakenya basi aangazie gharama ya juu ya maisha wala si siasa za aliyeshinda uchaguzi wa mwaka jana.

Akimjibu, diwani wa Kileleshwa Robert Alai alimweleza Bw Kigame amuunge mkono Bw Odinga kwani alikuwa akimpigania.

“Mpiganie huyo kaka. Kila mtu aangazie nguvu zake. Ulinyang’anywa nafasi ya kuwa kwenye kinyang’anyiro. Bw Odinga anakupigania,” akasema Bw Alai.

Bw Kigame aliduwazwa na jibu lake Bw Alai huku akimweleza kuwa udhalimu wa uchaguzi huwa iwapo “unawagusa nyinyi.”

“Nionyeshe video moja, sentensi au neno moja ambalo Bw Odinga alisema wakati nilinyimwa nafasi ya kuwa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka jana.”

Jumatano, Bw Odinga alitangaza kuwa ataongoza maombi katika ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

‘Maombi’ hayo yanahofiwa kusababisha vuta nikuvute baina ya waandamanaji na polisi.

Hata hivyo, Bw Odinga ametetea msimamo wake kwa kusema kuwa maombi hayo yatasaidia kuwapa Wakenya tume itakayopigania haki za watu.

“Baada ya kutembelea kaunti za Kisii Ijumaa na Kisumu Jumamosi, tutakuwa na hafla ya maombi katika afisi za IEBC,” akasema Bw Odinga.

“Lazima tupiganie haki za uchaguzi katika nchi yetu. Hili ni jambo ambalo tumewaeleza wabunge wetu na tutaendelea kuwahimiza Wakenya watetee haki zao,” akaongeza.

Bw Kigame alinyimwa fursa ya kuwa kwenye kinyang’anyiro cha urais cha Agosti 9 mwaka jana huku IEBC ikisema kuwa hakutosheleza mahitaji ya tume ili kuwania kiti hicho.

Hata hivyo, amekuwa mstari wa mbele kuzungumzia kuhusu masuala ya nchi huku akikashifu viongozi kwa matendo yao.

  • Tags

You can share this post!

Salernitana wamtimua kocha kwa mara ya pili baada ya siku...

Wanajeshi wa KDF waua Al-Shabaab watatu, wafanikiwa kupata...

T L