• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:58 PM
Mivutano kuhusu tiketi za ODM ‘itamharibia Raila’

Mivutano kuhusu tiketi za ODM ‘itamharibia Raila’

VICTOR RABALLA NA KASSIM ADINASI

WAWANIAJI viti katika ngome ya kiongozi wa ODM Raila Odinga ya Luo Nyanza, wameonywa dhidi ya mivutano miongoni mwao kwani hali hiyo inaweza kuvuruga nafasi ya waziri huyo mkuu wa zamani kushinda urais.

Vigogo wa kisiasa eneo hilo wakiongozwa na Seneta wa Siaya James Orengo, walisema Jumamosi mg’ang’anio mkali wa tiketi ya ODM katika eneo hilo unaweza kumgharimu kisiasa mwanasiasa huyo mkongwe anayepania kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

“Inasikitisha kuwa msukumo wa kupata idhini ya kupeperusha bendera ya ODM katika kinyang’anyiro cha viti mbalimbali unatisha kutugawanya ilhali sisi kama jamii tunalenga kiti kikubwa nchini.

“Watu kutoka jamii nyinginezo wameelezea nia ya kumuunga mkono Bw Odinga na hivyo tusiharibu wema huu kupitia siasa za mashinani. Tuweke kando masilahi yetu ya kibinafsi kwa ajili ya wadhifa mkubwa nchini,” akasema.

Bw Orengo, ambaye ametangaza nia ya kuwania ugavana wa Siaya, alisema yu tayari kupoteza kiti hicho ikiwa hiyo itamwezesha Bw Odinga kufaulu kuingia Ikulu.

“Sharti tufaulu wakati huu. ODM inalenga kupata idadi kubwa ya viti katika bunge la kitaifa na seneti pamoja na mabunge ya kaunti. Viti hivi vitakuwa na maana kwetu kama chama kiongozi wetu akishinda urais,” akasema katika hafla ya mazishi ya Mama Wilfrida Odanga Opot katika kata ndogo ya Sirembe, eneobunge la Gem, kaunti ya Siaya.

Hata hivyo, Bw Orengo aliwaonya wakazi dhidi ya kuwachagua viongozi vigeugeu ambao watasaliti serikali ya Bw Odinga.

“Tunawataka watu ambao ni waaminifu na wamejitolea kuendeleza sera ya itikadi za ODM. Tuwe waangalifu tusiingie katika mtego wa watu ambao wanataka kutumia umaarufu wa chama chetu kama ngazi ya kuingia mamlakani,” akaeleza.

Siasa zilisheheni katika hafla hiyo ya mazishi ambayo pia ilihudhuriwa na wabunge; Samuel Atandi (Alego Usonga), Christine Ombaka (Mwakilishi wa Kike, Siaya) na wawaniaji kadha akiwemo aliyekuwa msemaji wa polisi Charles Owino.

Pia alikuwepo kakake aliyekuwa Mbunge wa Gem Jalang’o Midiwo ambaye anasaka tiketi ya ODM kuwania kiti hicho kinachoshikiliwa sasa na Bw Elisha Odhiambo.

Wito wa viongozi hao umejiri siku chache baada ya maafisa wa ODM kuwataka viongozi wa chama na wawaniaji kusitisha kampeni zao, ili kuelekeza juhudi katika kuhamasisha wakazi wajiandikishe kwa wingi kuwa wapiga kura.

Awamu ya pili ya shughuli hiyo inakamilika leo kote nchini huku idadi ndogo ya watu wakijitokeza.

kinyume na matarajio ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Maafisa wa chama hicho walisema wakazi wakijiandikisha kwa wingi wataimarisha nafasi ya Bw Odinga kushinda kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 mwaka huu.

You can share this post!

BAHARI YA MAPENZI: Kukabili mtazamo hasi dhidi ya wanawake

Kalonzo akana madai ya kutoa masharti kwa Raila

T L