• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
BAHARI YA MAPENZI: Kukabili mtazamo hasi dhidi ya wanawake

BAHARI YA MAPENZI: Kukabili mtazamo hasi dhidi ya wanawake

NA SIZARINA HAMISI

HIVI karibuni nilitembelea soko moja lililopo jijini Dar es Salaam, na wakati nikiendelea na shughuli ya kununua mahitaji yangu, mwanaume mmoja pale sokoni akanisogelea na kunishika makalio.

Nikageuka na kumuangalia usoni na nikamwambia kitendo alichokifanya sio sahihi na ninaweza kumshtaki mahakamani na akaadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Majibu yake yalinikasirisha, yakanishangaza na hata kunihuzunisha. Bila aibu akaniuliza kwa nini namjibu, sababu wanawake hawatakiwi kujibu wanaume.

Akaniambia hivi huku amenikazia macho.

“Hunipeleki kokote, ninyi wanawake ni wa kutumika tu, nitakufanya lolote nitakalo…”

Nikamuelimisha kwa utulivu kwamba, mwanamke anayo haki ya kuzungumza sawa na anavyozungumza yeye, anayo haki ya kukataa jambo asilotaka na pia anayo haki ya kuchukua hatua za kisheria iwapo atapenda kufanya hivyo.

Nina uhakika vitendo hivi vinawatokea wanawake wengi kwa namna tofauti. Na wengi huwa wananyamaza tu. Katika matukio mengi kumekuwa na mtazamo hasi kwa wanawake, hasa wakionekana ni watu dhaifu, wasiotakiwa kueleza hisia zao, wasiotakiwa kuhoji jambo lolote na wanaotakiwa wakubali lolote lile wanalotakiwa kutenda na mwanamume.

Uhalisia ni kwamba mtazamo hasi kwa wanawake umekuwepo katika jamii za Afrika; watoto wanazaliwa, wanakua hadi wanazeeka wakiishi katika utaratibu ambao kwa jinsi moja ama nyingine hauthamini sana wanawake.

Ni maisha ambayo tumeyaona ya kawaida ingawa sio ya kawaida.

Kawaida binadamu hukumbuka zaidi matukio yasiyofaa kuliko yale yaliyo mazuri.

Kwamba ni rahisi kukumbuka mtu akikutusi kuliko kukumbuka mtu aliyekuambia maneno ya faraja ama upendo.

Na kawaida hii ndio pia wanasaikolojia wanaeleza husababisha watu kuishi katika vitendo visivyofaa kuliko vile vizuri.

Wanaume ndio wahusika wakubwa kwenye hili. Kwani wapo baadhi ambao huwa na dharau na chuki kwa wanawake na kila kitu kinachohusiana nao.

Mwanamume mwenye mtizamo hasi kwa wanawake atazingatia hali yoyote ya kibinafsi au ya kazi kama fursa ya kunyanyasa, kudhalilisha, kudunisha na hata kudharau.

Bahati mbaya hali hii hujidhihirisha katika maeneo ya kazi, biashara na hata katika familia. Kwamba wapo akina dada walioelimika vya kutosha na wenye uwezo wa kupatiwa majukumu makubwa maeneo ya kazi, lakini wanatengwa sababu ya mitizamo hasi ya walio kwenye madaraka ya maamuzi.

Halikadhalika katika maeneo ya biashara, akina dada wamejikuta katika wakati mgumu pale wanapodhuhuliwa pesa ama bidhaa zao na wasiwe na nafasi ya kulalamika ama kuchukua sheria stahiki.

Muhimu kwa wanawake na wasichana wanaojipata kwenye hali ya chuki na dharau kutoka kwa waume zao, wafanyakazi wenzao, wafanyabiashara wenzao na jamii kwa ujumla; waelewe kwamba kuna sheria zinazowalinda.

Vitendo hivi sio vya kunyamazia, inafaa vizungumziwe kwa utulivu kwa madhumuni ya kuleta maelewano na kuweka mipaka pale inapobidi.

Ni vyema pia kutambua heshima ni kitu cha bure, huna sababu ya kumsujudu mtu mwingine ili kuweza kupata iliyo haki yako. Mwisho wa siku, maisha ni ya watu wawili na maelewano ni ya wawili ama zaidi. Chukua hatua stahiki!

[email protected]

You can share this post!

MALEZI KIDIJITALI: Mwongoze kwa vitendo kutumia mitandao

Mivutano kuhusu tiketi za ODM ‘itamharibia Raila’

T L