• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Mngurumo wa Joho wakosekana siasani

Mngurumo wa Joho wakosekana siasani

NA MWANDISHI WETU

USHAWISHI wa Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, kwa siasa za Pwani na kitaifa kwa jumla umekosekana kwa takriban wiki mbili sasa baada ya kuugua kwake.

Ilibainika Bw Joho alianza kuugua punde alipowasili nchini kutoka ziara ya Uingereza ambapo alikuwa ameandamana pamoja na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, na wanasiasa wengine wa Muungano wa Azimio la Umoja.

Ingawa afisi yake haijasema wazi aliko naibu kiongozi huyo wa ODM, baadhi ya viongozi wa chama hicho walithibitisha anaendelea kupata nafuu.

Siku chache baada ya Bw Odinga na kikosi chake kukamilisha ziara yao Uingereza, Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed alifichua Bw Joho alikuwa akipokea matibabu.

Bw Mohamed ndiye alikuwa wa kwanza kumtakia heri gavana huyo wazi, kupitia kwa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Hapo jana Jumatano, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kilifi, Bi Gertrude Mbeyu, alithibitisha Bw Joho anaendelea vyema.

“Tumtakie naibu kiongozi wetu wa chama 001 Sultan Joho afueni ya haraka anapoendelea kupona. Tunakosa sana nguvu zake katika mikutano yetu ya hadhara,” akasema Bi Mbeyu.

Haijabainika wazi maradhi anayougua gavana huyo, wala mahali halisi ambapo anapokea matibabu.

Kukosekana kwake kumetokea wakati ambapo Kaunti ya Mombasa ni miongoni mwa zile ambazo ODM inakumbwa na changamoto kubwa kuamua mtindo utakaotumiwa kuchagua wanasiasa watakaowakilisha chama katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Mzozo ulitokea baada ya kubainika kuwa, Baraza la Kitaifa la Uchaguzi katika chama hicho lilikuwa linazingatia matokeo ya kura za maoni kuamua watakaopewa tikiti za kuwania viti mbalimbali ikiwemo ugavana.

Mbali na Mombasa, kaunti nyingine ambapo mzozo aina hiyo umetokea ni Kilifi.

ODM ilifanikiwa kukamilisha uteuzi wa wagombeaji katika Kaunti za Kwale na Tana River, ambapo kura za mchujo ziliandaliwa katika sehemu chache za kaunti hizo huku nafasi nyingine zikijazwa kupitia tikiti za moja kwa moja.

Katika Kaunti ya Mombasa, mvutano mkubwa zaidi ni kati ya Mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir, na mfanyabiashara Suleiman Shahbal, ambao wanang’ang’ania tikiti ya kuwania ugavana kupitia kwa ODM.Naibu Gavana, Dkt William Kingi, aliamua kuhamia Chama cha Pamoja African Alliance (PAA) akidai hangelitendewa haki katika azimio lake la kutaka kuwania ugavana kupitia ODM.

Kura za maoni zilizodhaminiwa na chama hicho zilionyesha Bw Nassir akiwa na umaarufu zaidi, ila Bw Shahbal anasisitiza wanachama wapewe nafasi kujiamulia wagombeaji wanaotaka kupitia kwa kura ya mchujo.

“Watu wa Mombasa ndio wanafaa kupewa nafasi ya kuamua ni nani anastahili kuwa diwani, mbunge, seneta na gavana. Hii itawezekana tu kupitia kura ya mchujo,” alisema Bw Shahbal.

Bw Nassir alisema yuko tayari kwa mbinu yoyote ile ambayo chama kitaamua kutumia kuteua mgombeaji atakayeshindania urithi wa kiti cha Bw Joho.

Baraza Kuu la ODM jana Jumatano lilitarajiwa kuandaa mkutano maalumu na wanasiasa wa Mombasa ili kujaribu kutafuta maelewano kati yao kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuepusha mpasuko chamani.

You can share this post!

Kinyang’anyiro cha ugavana Kakamega kuzua kivumbi kikali

Maafisa wa IEBC katika maeneobunge na kaunti wahamishwa...

T L