• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
MSIMU WA KUNUNUA BARAKA

MSIMU WA KUNUNUA BARAKA

Na CHARLES WASONGA

UCHAGUZI mkuu ujao unapoendelea kukaribia, wanasiasa wanaomezea mate viti mbalimbali, hasa kile cha urais, wamekuwa wakifululiza makanisani kutafuta baraka ili wafanikiwe katika uchaguzi huo.

Katika miezi ya hivi karibuni, wagombeaji urais ambao hapo awali ilikuwa nadra kwao kwenda kanisa Jumapili, wameonekana katika majumba hayo ya kuabudu bila kuchelewa.

Na wengi wanatoa sadaka kubwa kubwa hivi kwamba, baadhi ya wadadisi wanasema ni kama kwamba wananunua Baraka.

Kando na Naibu Rais William Ruto ambaye kwa muda wa miaka minne iliyopita amekuwa akihudhuria ibada na harambee makanisani, kiongozi wa ODM Raila Odinga, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper) na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi hawakosi kuhudhuria ibada kila wiki.

Kwa mfano wiki iliyopita, Dkt Ruto alihudhuria ibada katika Kanisa la Global Cathedral, eneo bunge la Lang’ata, kaunti ya Nairobi ambako alitoa sadaka ya Sh1 milioni.

Nao Mbw Odinga na Mudavadi walihudhuria hafla ya kutawazwa kwa Askofu mpya wa Kanisa la Kianglikana Dayosisi ya Butere, Rose Okeno ambako walizimwa kuhutubu.

Baadaye, Bw Mudavadi alielekea Murang’a kuongoza harambee katika Kanisa Katoliki la Kinyona. Kwa upande wake, Bw Musyoka aliungana na Wakristo katika kanisa la Royal Christian Church, Ongata Rongai, Kajiado kwa ibada ya Jumapili.

Wadadisi wanasema wanasiasa vigogo hawa huwa hawaendi kuabudu pekee, bali kutoa sadaka nono ili “kununua” baraka kwa ajili ya kufikia ndoto zao katika kinyang’anyiro kijacho.

“Kweli huu ni msimu wa wanasiasa kununua baraka makanisani. Ndio maana siku hizi kila Jumapili utawaona makanisani wakiombewa na makasisi huku wakiwa wamepiga magoti. Bila shaka hiyo ni hatua ya kutafuta baraka na huja baada ya wao kutoa michango ya harambee au sadaka kubwa,” asema Bw Mark Bichachi.

Mnamo Agosti 29, 2021, Bw Odinga alisambaza picha akiombewa na makasisi wa Kanisa la Bible Fellowshipi Church, Kigumo, Murang’a, alikohudhuria ibada ya Jumapili.

“Tuliungana na waumini katika Kanisa la Bibile Fellowship, eneo bunge la Kigumo kaunti ya Murang’a kwa ibada ya Jumapili. Askofu msimamizi Peter Kamau alitoa mahubiri ya kufana kuhusu umuhimu wa kutimiza yale ambayo tumeazimia kutekeleza kama viongozi,” Bw Odinga akasema kupitia Twitter.

Wiki hiyo hiyo, Bw Mudavadi alipiga magoti katika Kanisa la AIPCK, eneo bunge la Githunguri, Kiambu ambako alihudhuria ibada kabla ya kuongoza harambee.

Kwa upande wake, Dkt Ruto ametetea mtindo wake wa kuhudhuria ibada kila wiki na kutoa mamilioni ya fedha kuchangia ufadhili wa miradi mbalimbali ya kanisa, akisema anawekeza mbinguni.

“Mimi huwekeza kwa miradi ya kuendeleza kazi ya Mungu kwa kuongoza michango makanisani. Wale wengine hutumia utajiri wao kuwekeza katika mambo mengine ya kiulimwengu kama uganga. Hiyo ndio tofauti yangu na wao,” akasema mwezi jana baada ya kuhudhuria ibada katika Kanisa la Holy Tabernacle, mtaa wa Umoja II, Nairobi.

Viongozi wa upinzani, wakiongozwa na Bw Odinga wamekuwa wakikosoa Dkt Ruto kutokana na mtindo wake wa kutumia makanisa kama jukwaa la kujipigia debe kisiasa, wakidai pesa anazotoa makanisani ni za “ufisadi.”

Juzi, Dkt Ruto aliwakejeli wenzake kwa kupata “wokovu” na kufuata nyayo zake kwa kuhudhuria ibada kila Jumapili na kutoa michango makanisani.

“Hata kama wamekuja makanisani kushindana nami, nimewakaribisha. Wamekuwa wakitulaani kwa kufanya harambee kujenga makanisa lakini sasa wanakuja kujipendekeza. Sharti wanipongeze kwa kujenga makanisa. Sasa wanafaa kutubu na kuomba msamaha kwa kutokosoa,” Dkt Ruto akasema Jumapili katika Kanisa la Global Cathedral.

Jumapili, Kiongozi wa Kanisa la ACK Jackoson Ole Sapit nchini aliwazima wanasiasa kuhutubu katika madhabuhu ya makanisa yote ya kanisa hilo.

Alisema hayo kwenye hafla ya kutawazwa kwa Askofu Okeno, Butere. Vile vile, jana Ole Sapit alitisha kuwachukulia hatua za kinidhamu makasisi wa ACK watakaowaruhusu siasa katika makanisa yao.

You can share this post!

Raila na Mudavadi wamenyania kura za Magharibi

Joho na Mucheru waonya wakazi dhidi ya Ruto