• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:21 PM
Mung’aro awafyeka mawaziri wa Kingi

Mung’aro awafyeka mawaziri wa Kingi

GAVANA wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, amewatimua mawaziri watano wa utawala wa mtangulizi wake, Bw Amason Kingi.

Katika mabadiliko ya uongozi serikalini aliyotaja kuwa ya mpito, Bw Mung’aro amebakisha mawaziri wanne wa serikali iliyopita.

Wanne hao, mbali na kusimamia wizara zao, watashikilia majukumu ya wizara nyingine huku serikali ya kaunti ikisubiri madiwani waapishwe ndipo uteuzi kamili wa mawaziri ufanyike.

Wakati huo huo, Bw Mung’aro pia amewafuta kazi maafisa wakuu wote wa idara za kaunti akisema muda wao wa kuhudumu umekamilika chini ya kandarasi walizopewa, huku akiwateua wakurugenzi ambao watashikilia nyadhifa hizo.

Hata hivyo, ameongoza muda wa kuhudumu wa katibu wa kaunti, Bw Arnold Mkare, kwa miezi sita.

Mawaziri wanne waliobaki mamlakani ni Dkt Anisa Omar katika wizara ya masuala ya jinsia, Bw Charles Dadu (Afya), Bi Rachael Musyoki (Elimu) na Bi Maureen Mwangovya (Ardhi).

Waliotimuliwa ni pamoja na Prof Gabriel Katana (Ugatuzi), Prof Josephat Mwatela (Barabara), Bw Kiringi Mwachitu (Maji), Bi Luciana Sanzua (Kilimo) na Bi Nahida Athman (Biashara na Utalii).

Akiwahutubia wanahabari ofisini mwake Jumanne, Bw Mung’aro alisema mageuzi hayo yatasaidia serikali yake kutoa huduma muhimu kwa wananchi kwa wakati unaofaa anapoendelea kupanga uongozi wa kaunti.

“Mawaziri na maafisa wakuu wanaondoka wana muda hadi Ijumaa kutoka ofisini. Ni matumaini yangu na ya watu wa Kilifi kuwa maafisa wote watawajibika vilivyo katika utendakazi wao,” akasema Bw Mung’aro.

Gavana huyo pia ameteua wakili Henry Farrajj Chipinde kama wakili wa kaunti wa muda baada ya kukamilika kwa muda wa kuhudumu wa Bibi Fondo.

Kwingineko, Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, ana kibarua kuamua iwapo ataendelea kuhudumu na mawaziri walioteuliwa na mtangulizi wake, Bw Salim Mvurya.

Bi Achani alikuwa naibu gavana wa Bw Mvurya kwa miaka 10.

Duru kutoka kwa kaunti hiyo zilisema tayari majadiliano yameanza kuhusu mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa katika baraza la mawaziri katika kaunti.

Hii ni baada ya Bi Achani kufanya mkutano wake wa kwanza na Baraza la Mawaziri linaloondoka, Jumatatu.

“Gavana alifanya kikao na baraza la mawaziri kwa zaidi ya saa 10. Walimaliza wakiwa wamechelewa hadi hatujajua matokeo,” akasema afisa aliyeomba asitajwe jina, kwa kuhofia kuadhibiwa.

Wakati wa mkutano wake wa kuwaaga wafanyakazi wa kaunti, Bw Mvurya aliwahakikishia kwamba hawatapoteza kazi zao ikiwa Bi Achani ndiye atashinda ugavana.

Taifa Leo imebainisha kuwa, miongoni mwa masuala muhimu yatakayozingatiwa katika kuamua kama mawaziri watabaki au kutimuliwa ni uaminifu ulioonyeshwa nao katika miaka iliyopita na hasa kipindi cha uchaguzi.

Hii ni kutokana na kuwa, baadhi ya wafanyakazi wa kaunti walionekana kuegemea upande wa wagombea wengine wa kiti cha ugavana wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwezi Agosti.

Gavana Achani amedokeza kuwa angependa kutimiza mipango waliyokuwa wameanza na Bw Mvurya, na vilevile kurekebisha makosa waliyoyafanya ili kuhakikisha amehudumia wananchi ipasavyo.

Baadhi ya mawaziri waliopo wanashikilia wizara zaidi ya moja baada ya wenzao kujitosa katika ugombeaji viti vya kisiasa uchaguzini.

Aliyekuwa Katibu wa Kaunti, Bw Martin Mwaro, aliyekuwa Waziri wa Michezo na Vipaji, Bw Ramadhan Bungale na aliyekuwa Waziri wa Elimu, Bw Mangale Chiforomodo walijiuzulu mapema mwaka 2022 ukianza ili kugombea viti vya kisiasa.

Bw Chiforomodo alifanikiwa kushinda ubunge Lungalunga, lakini Bw Mwaro na Bw Bungale wakashindwa walipowania ubunge Magarini na Matuga mtawalia.

Bw Mwaro kwa sasa ameteuliwa kuwa katibu wa Kaunti ya Kilifi na Gavana Mung’aro.

  • Tags

You can share this post!

Waingereza kupata waziri mkuu mpya Jumatatu, Boris akiondoka

Mwanamke atupwa jela miaka 25 kwa ulanguzi wa mihadarati

T L