• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 7:50 AM
Muturi aahidi kutumia wahitimu wasio na ajira katika vita dhidi ya ufisadi

Muturi aahidi kutumia wahitimu wasio na ajira katika vita dhidi ya ufisadi

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ameahidi kwamba akichaguliwa kuwa Rais wa tano wa taifa atatumia wahitimu kutoka vyuo vikuu wasio na ajira katika vita dhidi ya ufisadi.

Akiongea Ijumaa baada ya kuzindua mpango wa kitaifa wa upanzi wa miti katika Shule ya Msingi ya Upper Matasia, eneobunge la Kajiado, Kaskazini, Kaunti ya Kajiado, Bw Muturi alisema serikali yake itawatumia wahitimu hao kutambua maafisa serikalini.

“Nitawatumia wahitimu kama maskauti wa kuwatambua maafisa wafisadi katika utumishi wa umma. Hii ndio njia mwafaka ya kuzuia uovu huu badala ya kuwakamata washukiwa na kuwapeleka kortini ambako wao hutumia pesa walizoiba kuhujumu kesi dhidi yao,” akasema.

Bw Muturi alisema serikali yake haitavumilia uovu huo katika utumishi wa umma na kwamba maafisa wote watakaogunduliwa kujihusisha na ufisadi watapigwa kalamu.

“Nikichaguliwa kuwa rais, shoka itaangukia wafisadi. Wahitimu vibarua watakuwa na bidii kupambana na ufisadi kwa sababu wao ndio watachukua nafasi za maafisa watakaopigwa kalamu,” Spika Muturi akaambia wanahabari baada ya kuzindua mpango huo wa upanzi wa miti.

Spika huyo ameshikilia kuwa atawania urais katika uchaguzi mkuu ujao kwa tiketi ya chama cha Democratic Party of Kenya (DP).

Spika Justin Muturi apanda miche ya miti katika eneo la Ngong. PICHA | JUSTIN MUTURI

Chama hicho kiliasisiwa na Rais mstaafu Mwai Kibaki mnamo mwaka wa 1992.

You can share this post!

FATAKI: Ni upumbavu kuamini thamani ya mwanamke hushuka...

JAMVI: Mlima utatoa nani mgombea mwenza wa Raila 2022?

T L