• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
JAMVI: Mlima utatoa nani mgombea mwenza wa Raila 2022?

JAMVI: Mlima utatoa nani mgombea mwenza wa Raila 2022?

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga, anakabiliwa na kibarua kumchagua mgombea-mwenza wake kutoka ukanda wa Mlima Kenya kadri Uchaguzi Mkuu wa 2022 unapokaribia.

Kufikia sasa, watu watatu wamependekezwa kuwa wagombea-wenza wa Bw Odinga, hali inayotajwa kuzua ushindani wa kisiasa baina yao.

Watatu hao ni mwanasiasa Peter Kenneth, Gavana Lee Kinyanjui wa Nakuru na kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua.

Kulingana na wadadisi wa siasa, hali hiyo inatarajiwa kuzua mtihani wa kisiasa kwa Bw Odinga, ikizingatiwa watatu hao wana ushawishi tofauti wa kisiasa katika maeneo wanakotoka.

Bw Kenneth anatoka katika Kaunti ya Murang’a, Bw Kinyajui katika Kaunti ya Nakuru huku Bi Karua akitoka katika Kaunti ya Kirinyaga.

“Itamlazimu Bw Odinga kuwa tayari kukabili athari za kisiasa zitakazotokana na chaguo atakalofanya. Itamlazimu kutumia ujuzi wake kuhakikisha hakutakuwepo na migawanyiko yoyote ya kisiasa,” asema Bw Wahome Mwangi, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Bw Kenneth amekuwa kwenye siasa kwa muda. Alihudumu kama mbunge wa Gatanga na waziri msaidizi katika serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Aliwania urais 2013 kwa tiketi ya chama cha Kenya National Congress (KNC).

Mnamo 2017, aliwania ugavana katika Kaunti ya Nairobi kama mwaniaji huru lakini akashindwa na Bw Mike Sonko, aliyewania kwa tiketi ya Chama cha Jubilee (JP).

Bw Kenneth ameibukia kuwa miongoni mwa washirika wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta, baada ya handisheki kati yake na Bw Odinga.

Kutokana na ukaribu huo, wadadisi wanamtaja kuwa miongoni mwa wanasiasa wenye nafasi nzuri sana kuteuliwa kama mgombea-mwenza wa Bw Odinga.

“Kando na kuwa mwanasiasa, Bw Kenneth ana ukaribu mkubwa na mabwanyenye wa Mlima Kenya, hasa wale walioasisi Wakfu wa Mlima Kenya (MKF). Ni mwanasiasa mwenye tajriba pana. Hilo pia linamweka kifua mbele dhidi ya wengine,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Gavana Kinyanjui anatajwa kumwezesha Bw Odinga kupata uungwaji mkono kutoka jamii ya Wakikuyu wanaoishi katika eneo la Bonde la Ufa, wala si wale wanaoishi katika ukanda wa Mlima Kenya.

Wadadisi wanasema kuwa ingawa ameibukia kuwa mshirika wa karibu sana wa Bw Odinga na Rais Kenyatta, haonekani kuwa “mmoja wa wenyeji wa Mlima Kenya.”

“Kitaswira, Bw Kinyanjui anaonekana kutokuwa mmoja wa wenyeji wa Mlima Kenya. Ingawa amefanya juhudi kujenga taswira hiyo, bado ana kibarua kigumu. Ijapokuwa kuna uwezekano uteuzi wake kumzolea kura Bw Odinga katika eneo la Bonde la Ufa, atakuwa na kibarua kuteka nafsi za wenyeji wa Mlima, hasa katika kaunti za Nyandarua, Nyeri, Meru, Tharaka-Nithi, Kirinyaga, Embu, Murang’a na Kiambu,” akasema Prof Njoroge.

Kwa upande wake, Bi Karua anatajwa kuwa chaguo bora, ijapokuwa itamhitaji Bw Odinga na washirika wake kutumia ujuzi wao wa kisiasa “kumuuza” kwa wenyeji.

“Ni mwanasiasa mzuri na mwenye tajriba pana. Hata hivyo, itamlazimu Bw Odinga kuwarai wafuasi wake kumuunga mkono kama chaguo lake, hasa miongoni mwa wenyeji wa Mlima Kenya wanaishi katika eneo la Bonde la Ufa,” asema Bw Charles Munyua, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Hata hivyo, washirika wa Bw Odinga wanasema bado ni mapema kuwataja watu anaoweza kuwateua kama mgombea-mwenza wake.

“Ingawa wanasiasa hao wameonyesha uwezo mkubwa wa kisiasa, itamlazimu Bw Odinga kufanya ushauri wa kina kuhakikisha chaguo lake litamjenga kisiasa badala ya kumpunguzia uungwaji mkono,” asema Bw Munyua.

You can share this post!

Muturi aahidi kutumia wahitimu wasio na ajira katika vita...

Mourinho pabaya Italia baada ya Roma kuzamishwa tena ligini

T L