• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Mvurya atengewa cheo katika upeo wa Kenya Kwanza

Mvurya atengewa cheo katika upeo wa Kenya Kwanza

NA SIAGO CECE

GAVANA wa Kwale, Salim Mvuryaamepata fursa ya kuzamia uongozi wa kitaifa baada ya Naibu Rais William Ruto, kumshirikisha kwenye meza kuu ya Muungano wa Kenya Kwanza.

Ikizingatiwa chaguzi zilizopita, viongozi wanaokaa kwenye meza ya upeo wa muungano wa kisiasa huwa na nafasi bora ya kufanya maamuzi makuu au hata kuzingatiwa kwa nafasi kubwa za uongozi ikiwemo wadhifa wa mgombea mwenza wa urais.

Baadhi ya wanasiasa na viongozi wa kijamii wanaoegemea upande wa Dkt Ruto katika ukanda wa Pwani wamekuwa wakishinikiza gavana huyo ateuliwe kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi ujao.

Bw Mvurya, ambaye ni mwanachama wa Jubilee, huegemea upande wa Dkt Ruto chini ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Akihutubu alipozuru Kwale mnamo Jumamosi, naibu rais alisema gavana huyo anayekamilisha kipindi chake cha pili cha uongozi atakaa meza moja naye pamoja na vinara wa vyama tanzu vya Kenya Kwanza.

Kufikia sasa, vinara wenza wa mu – ungano huo ni Kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, na Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula anayeongoza Ford Kenya.

“Kutokana na utendakazi mzuri

na rekodi aliyoweka katika Kaunti ya Kwale ukilinganisha na magavana wenzake, Bw Mvurya amejizolea kiti katika siasa za kitaifa kwa sababu tungependa kazi yake iendelee.

Bw Mvurya, leo umeungana na vinara wengine wa Kenya Kwanza na sasa utakuwa mmoja wetu,” akasema Dkt Ruto.

Uamuzi huo uliungwa mkono na wabunge Khatib Mwashetani (Lungalunga), Benjamin Tayari (Kinango), Feisal Abdallah (Msambweni) na Mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa.

“Ninampa pongezi Bw Mvurya kwa kazi aliyofanya kwa sababu kati ya gatuzi sita za pwani, umeinua sura yetu. Na wewe unaweza kutembea sehemu yote Pwani na wakuskize wakijua kuna kiongozi ambaye anaweza kuwatoa kwenye lindi la umaskini,” Bi Jumwa alisema.

Kwa upande wake, Bw Mvurya alisema Pwani, hasa Kaunti ya Kwale imekuwa ikipigia kura viongozi wa kitaifa ambao hawajainua uchumi wa eneo hilo ipasavyo.

“Hapo awali wakazi wa Kwale wamekuwa wakipigia kura viongozi ambao hawajatusaidia. Shida moja kuu katika kaunti hii ni uchumi na suluhisho litakuwa serikali ya Bw Ruto,” akasema.

Muungano wa Kenya Kwanza umlikuwa katika ziara ya Pwani kwa siku mbili kuanzia Ijumaa, viongozi hao wakitembelea kaunti za Taita Taveta, Kilifi, Kwale na Mombasa.

  • Tags

You can share this post!

Aliyekuwa msaidizi wa Raila akataa kuwania kwa ODM

Mbogo adai Nassir hana rekodi nzuri ya kutekeleza miradi

T L