• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Aliyekuwa msaidizi wa Raila akataa kuwania kwa ODM

Aliyekuwa msaidizi wa Raila akataa kuwania kwa ODM

NA GEORGE ODIWUOR

ALIYEKUWA mkuu wa wafanyakazi katika Afisi ya Waziri Mkuu, Bw Caroli Omondi, amekataa wito wa ODM kurudi katika chama hicho akitumie kugombea kiti cha ubunge Suba Kusini.

Bw Omondi alisema hatakubali shinikizo kutoka kwa maafisa wa chama hicho wanaotaka ajiunge tena na ODM alichohama akidai alinyimwa tiketi mara mbili kwenye mchujo.

Mwenyekiti wa ODM, John Mbadi alikuwa amemtaka Bw Omondi kurudi ODM na kugombea kiti cha kisiasa katika Kaunti ya Homa Bay.

Kulingana na Bw Mbadi, msaidizi huyo wa zamani wa Bw Odinga atakuwa na nguvu akiwa katika ODM.

“Ninajua nguvu ulizo nazo ukiwa ODM. Tumia chama hicho ikiwa unataka kugombea kiti cha ubunge,” Bw Mbadi alisema.

Mnamo 2017 Bw Mbadi alimshinda Bw Omondi kwenye mchujo ambao ulifanyika mara mbili katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Baada ya kukosa tiketi ya chama hicho, Bw Omondi ambaye baadaye aliteuliwa mwanachama wa bodi ya Kampuni ya Mafuta ya Kenya, alimuunga mkono kaka yake mdogo Peter Ocholla kumenyana na Bw Mbadi lakini akashindwa. Hii ilisababisha uhasama wa kisiasa kati ya Bw Omondi na ODM.

ODM sasa kinamtaka Bw Omondi kujiunga nacho tena kikisema ana nafasi kubwa ya kushinda kiti cha ubunge cha Suba Kusini.

“Chama hakingemnyima mwenyekiti wake tiketi. Lakini sitaki kuzungumzia nani alishinda mwingine kwenye mchujo uliopita.

Ukweli ni kwamba Calori atashinda kiti hicho akiwa ODM,” alisema Bw Mbadi.

Hata hivyo, Bw Omondi alisema kwamba hayuko tayari kurudi ODM lakini atagombea kiti hicho kwa tiketi ya chama kinachounga azma ya urais ya Bw Odinga kupitia muungano wa Azimio la Umoja.

Alisema yeye ni mmoja wa waanzilishi wa ODM na anakielewa vyema chama hicho.

“Chama kilinihujumu mara mbili kwa kuninyima tiketi katika azma yangu ya kuwa mbunge wa Suba Kusini. Siko tayari kugombea kiti hicho kwa tiketi ya ODM tena,” alisema Bw Omondi.

  • Tags

You can share this post!

Najuta kujiunga na Ford-Kenya, Wangamati sasa aungama

Mvurya atengewa cheo katika upeo wa Kenya Kwanza

T L