• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mwanzo mpya

Mwanzo mpya

NA BENSON MATHEKA

BAADA ya wiki kadha za malumbano kati ya wawakilishi wa muungano wa wa Azimio la Umoja-One Kenya na wenzao katika upande wa serikali, hatimaye viongozi hao wameonekana kuweka tofauti zao kando na kuweka maslahi ya nchi mbele.

Hii ni baada ya wanachama wa kamati ya mazungumzo yanayoendela katika Bomas of Kenya, Nairobi kuafikiana kuhusu ajenda watakazoangazia kwenye mazungumzo hayo.

Awali, viongozi wa pande zote walionekana kuwa na misimamo mikali na kutamausha wengi kuhusu uwezekano wa kupata mwafaka, hasa baada ya upinzani kutishia kurejea kwenye maandamano upya.

Kamati za kitaalamu za Azimio na Kenya Kwanza zilikubali masuala ambayo Bw Odinga amekuwa akisisitiza yajadiliwe na ambayo upande wa serikali unaoongozwa na Rais William Ruto umekuwa ukipinga.

Kamati hizo zinazoongozwa na Jeremiah Kioni (Azimio) na Muthomi Thiankolu zilikubali takriban matakwa yote ya Bw Odinga, ikiwemo kuweka muda ambao mazungumzo hayo yanafaa kukamilika.

Kamati hizo zilikubaliana kuwa mazungumzo hayo ya kutatua mzozo wa kisiasa kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 yakamilike ndani ya siku sitini.

Bw Odinga amekuwa akitishia kurudia maandamano mazungumzo hayo yakifeli.

Suala la gharama ya maisha ambalo Bw Odinga amekuwa akisema ni lazima lijadiliwe kwa lengo la kupunguzia Wakenya mzigo, limeonekana kupewa kipaumbele pamoja na masuala ya kikatiba ambayo yamepangwa kuangaziwa.

Katika orodha ambayo pande zote zilikubaliana kujadiliwa, masuala hayo yamo katika kundi la kwanza miongoni mwa makundi matano ya ajenda za mazungumzo.

“Ibara 43 ya katiba, gharama ya maisha na masuala yanayohusiana nayo,” ndio ajenda ya kwanza katika kundi la kwanza katika orodha iliyokabidhiwa wenyeviti wenza wa Kamati ya Mdahalo ya Kitaifa, Kalonzo Musyoka( Azimio) na Kimani Ichungw’ah (Kenya Kwanza).

Ibara 43 ya katiba inahusu haki za kimsingi za jamii kama vile utoshelevu wa chakula, huduma za afya, makao na usalama kwa kila Mkenya.

Hii ni licha ya Rais Ruto kuongoza washirika wake kupuuza suala hilo wakisema ni jukumu la serikali na haliwezi kujadiliwa nje yake.

Rais Ruto amekuwa akisisitiza kuwa serikali yake ina mpango wa kupunguza gharama ya maisha.
Kamati za kiufundi za pande zote pia zilikubali takwa la Bw Odinga kuhusu kukaguliwa kwa sava za kura ya urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

IEBC

Kulingana na orodha ya kamati hizo, suala hilo litajadiliwa chini ya ajenda ya Haki katika Uchaguzi na Masuala husika kama kuundwa upya kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kuchunguzwa upya kwa mipaka, masuala ambayo Bw Odinga alihimiza yajadiliwe.

Ingawa Kenya Kwanza haikuwa ikipinga suala ya kuundwa upya kwa IEBC, Rais Ruto na washirika wake wamekuwa wakipuuza kukaguliwa kwa sava wakisema, mchakato wa uchaguzi uliisha mwaka 2022 na kuwahimiza vinara wa Azimio kusubiri hadi 2027.

Bw Odinga ameonekana kupata ushindi mwingine katika mazungumzo hayo baada ya kamati za kuorodhesha suala la jamii zote kujumuishwa serikalini licha ya viongozi wa Kenya Kwanza kujigamba kuwa, wameunda utawala wao kwa kutegemea jamii zilizopigia kura muungano wao.

Aidha, kamati itajadili kuheshimiwa kwa vyama vya kisiasa na demokrasia ya vyama vingi katika juhuzi za kuzuia serikali kununua wabunge wa upinzani.

“Kuhakikisha kuna mbinu za kutosha za kukosoa serikali na heshima kwa vyama na miungano ya kisiasa,” ni moja ya masuala yaliyoorodheshwa kujadiliwa.

Masuala ambayo Kenya Kwanza iliwasilisha kwa mazungumzo ambayo Azimio haikupinga pia yameratibiwa kujadiliwa yakiwemo kutekelezwa kwa kanuni ya thuluthi mbili ya usawa wa jinsia, kuweka Hazina ya Maeneo Bunge katika katiba, kuidhinishwa kwa wadhifa wa mkuu wa mawaziri katika katiba na kuanzishwa kwa afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani bungeni ambayo inatarajiwa kumfaidi Bw Odinga.

Mazungumzo hayo yametambuliwa kisheria baada ya kuidhinishwa na Bunge na Seneti. Huu pia ni ushindi kwa Bw Odinga ambaye alishinikiza yafanyike kupitia maandamano.

“Leo tumeanza hatua muhimu kuelekea enzi mpya ya mazungumzo ya kisiasa kwa njia ya amani. Kwa kujitolea kuandika upya historia yetu, tumerasmisha makubaliano kuhusu mfumokazi na ajenda ambazo zitakuwa msingi wa Mazungumzo ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa,” alisema Bw Ichungwa’h jana Jumatano.

Bw Kalonzo alisema nia njema, uwazi na uadilifu ndio msingi wa mdahalo wa kweli.

  • Tags

You can share this post!

Dogo wa umri wa miaka 10 kuhutubia kongamano la tabianchi...

Lamu yatajwa miongoni mwa miji 13 mizuri duniani

T L