• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 1:05 PM
NI NCHI YA UNAFIKI

NI NCHI YA UNAFIKI

Na BENSON MATHEKA

HALI ya utangamano na utaifa wa Kenya imo hatarini kufuatia tabia za unafiki wa wazi za baadhi ya viongozi ambazo zinaweza kufanya nchi kusalia nyuma kimaendeleo, kuzidisha ukosefu wa usalama na kudidimiza demokrasia na utawala wa sheria.

Japo wataalamu wamekuwa wakitoa mchango wao kuhusu sera, utekelezaji wake unaofaa kufanikishwa na viongozi na maafisa wa serikali, wakiwemo maafisa wa usalama, umekuwa ukivurugwa huku raia wakipatiwa ahadi na matumaini hewa.

Maafisa wa usalama wanaotegemewa na raia kuwalinda, wamekuwa wakilaumiwa kwa kuwaua watu na kukiuka sheria wanazopaswa kutetea.

Hali hiyo inadhihirika wazi wakati huu wa janga la corona ambapo viongozi na maafisa wa usalama wanaendelea kukiuka na kupuuza kanuni zinazotolewa na serikali ambazo wanasukuma raia kutekeleza.

Mnamo Ijumaa, maafisa wa polisi sita walikamatwa kaunti ya Kisumu kwa kukiuka amri ya kutoka nje usiku. Ni maafisa wa polisi wanaotegemewa na serikali kutekeleza marufuku ya kuzuia msambao wa corona.

Kaunti ya Kisumu ni moja ya kaunti 13 za Nyanza na Magharibi zilizotajwa kuwa kitovu cha msambao wa virusi vya corona na shughuli zote zilisitishwa kuanzia saa moja usiku hadi saa kumi alfajiri.

Maafisa wa polisi wamelaumiwa pia kwa kupokea hongo kuruhusu watu kuingia na kutoka maeneo ambayo serikali imekuwa ikifunga katika juhudi za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.

Unafiki huo pia umedhihirishwa na viongozi ambao wamekuwa wakiandaa mikutano ya kisiasa inayohudhuriwa na watu wengi licha ya serikali kuipiga marufuku. Mnamo Ijumaa, Naibu Rais William Ruto alihutubia umati katika kaunti ya Pokot Magharibi.

Hii ilikuwa siku mbili baada ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuhutubia wakazi wa Mombasa baada ya kuhudhuria hafla moja mjini humo.

Wanaharakati wanasema ni unafiki kwa serikali kutangaza kanuni ambazo viongozi na maafisa wake wako msitari wa mbele kukiuka

“Tabia ya viongozi inaonyesha wao ndio wakiukaji wakuu wa sheria. Ikiwa wanakiuka kanuni za serikali na sheria za nchi, wanatarajia kweli Wakenya wengine, wakiwemo maafisa wa usalama kuziheshimu?” ahoji Beatrice Waithera, mwanaharakati na mfanyabiashara wa Nairobi.

Ingawa maafisa wa usalama ndio wanapaswa kuhakikisha mikutano hiyo haifanyiki miongoni mwa kanuni zingine, wamekuwa wakiwalinda viongozi wanaoandaa mikutano mikubwa ya umma ambapo watu wanasongamana.

Unafiki wa wazi pia umekuwa ukijitokeza katika mijadala muhimu ya kitaifa ambayo mirengo tofauti ya kisiasa huwa wanatumia raia wakilenga kutimiza maslahi yao ya kibinafsi na washirika wao.

Mfano wa hivi punde ni baadhi ya viongozi kupinga pendekezo kwamba, wawaniaji wa viti vya ubunge na udiwani wawe na digrii kutoka vyuo vikuu.

Baadhi ya wanaopinga pendekezo hilo wenyewe wamesomea uzamifu na licha ya kufahamu umuhimu wa masomo, wanalipinga ili kulinda maslahi ya washirika wao wakuu wa kisiasa.

Miradi na ahadi nyingi za serikali ambazo zimekuwa zikiwapa raia matumaini zimekosa kuzaa matunda baada ya viongozi na maafisa wakuu kuiwekea vikwazo kama vile kupigana na ufisadi na kutia nguvu ugatuzi.

Japo serikali kuu na wabunge wamekuwa wakilaumu mahakama kwa kuchelewesha kesi za ufisadi, imekuwa ikipunguza bajeti ya idara hiyo muhimu na hata kukataa kuapisha majaji.

Kufikia sasa, mvutano unaendelea kati ya Rais Uhuru Kenyatta na mahakama alipokataa kuapisha baadhi ya majaji walioteuliwa na Tume ya Huduma ya Mahakama miaka miwili iliyopita.

Hali ni sawa kuhusu ugatuzi ambapo magavana wamekuwa wakilia kwamba huduma katika serikali za kaunti zimekwama kwa kucheleweshewa pesa na serikali ya kitaifa.

Kulingana na Dkt Patrick Mbugua, mhadhiri na mtaalamu wa masuala ya utawala na mitafaruku, unafiki wa wanasiasa, viongozi na maafisa wa serikali ni tishio kwa uthabiti wa nchi.

Anatoa mfano wa Mpango wa Maridhiano (BBI) akisema kwamba, ingawa ulisemekana kuwa wa kuunganisha Wakenya, umewagawanya zaidi.

“Ripoti ya BBI sio ya kujenga amani ya kudumu Kenya kwa kuwa inazidisha mgogoro wa kijamii na ushindani na mgawanyiko katika uchaguzi,” asema Dkt Mbugua akichangia katika mtandao wa The Elephant.

Hilo ilmedhihirika huku Bw Odinga na kiongozi wa chama Wiper Kalonzo Musyoka ambao wanaunga mchakato huo, wakiendelea kurushiana lawama kuhusu utapeli wa kisiasa.

Wiki hii, wawili hao, walishutumiana Bw Musyoka akimlaumu Bw Odinga kwa usaliti wa kisiasa ilhali BBI wanayounga inafaa kuwaleta pamoja.

Huku serikali ikiendelea kupigia debe ajenda zake, imebainika kuwa haina pesa na inategemea mikopo kuendeleza shughuli zake.

You can share this post!

Ruto akejeli muungano wa Uhuru na Raila

Mjukuu wa Moi asusia DNA, hatarini kushtakiwa