• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Nitabwaga Raila Agosti, asema Ruto

Nitabwaga Raila Agosti, asema Ruto

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Willam Ruto jana Jumamosi alielezea imani yake kuwa atambwaga mpinzani wake mkuu katika kinyangányiro cha urais, Raila Odinga na kuunda serikali baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Akiongea katika mitaa mbalimbali ya Nairobi baada ya kuidhinishwa rasmi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwa mgombea urais katika uchaguzi huo, Dkt Ruto aliwakashifu wakosoaji wake ambao waliapa kuwa hatafika debeni.

“Kwa mara ya kwanza mtoto wa mtu masikini, ambaye baba yake hakuwahi kushikilia vyeo serikalini atapata nafasi ya kuwa rais wa Jamhuri ya Kenya kwa mapenzi ya Mungu. Na ningependa kuwahakikishia kwamba, kwa usaidizi wenu na mahasla wengine wengi nchini, tutawashinda na yule kibaraka wao; yule jamaa wa kitendawili (Raila),” akawaambia wafuasi wake katika mtaa wa South C.

Dkt Ruto alikuwa ameandamana na vigogo wengine wa muungano wa Kenya Kwanza (KKA) wakiwemo; mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, Moses Wetangúla (Ford Kenya), Alfred Mutua (Gavana wa Machakos), Justin Muturi (Spika wa Bunge la Kitaifa), Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki, miongoni mwa wengine.

Dkt Ruto, na vinara hao wa muungano huo, waliwahutubia wafuasi wao katika mitaa ya South B, Mukuru, Burma, Gikomba, Majengo kabla kuongoza mkutano mkubwa katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji.

Kila aliyezungumza alionekana kumshutumu Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli ambaye wakati mmoja alinukuliwa akisema Dkt Ruto hatafika debeni.

“Yule kibaraka wao aliyesema Ruto hatakuwa debeni ajue kwamba, mapenzi ya Mungu ni makuu. Tunataka kumweleza kwamba ndoto yake imefeli na Agosti 10, 2022, rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya hatakuwa yule Mzee mwenzake bali kiongozi mchapa kazi William Samoei Arap Ruto,” Bw Gachagua akasema.

Naye Bw Mudavadi alikariri kuwa, Dkt Ruto atamshinda Bw Odinga kwa kura nyingi katika awamu ya kwanza.

“Leo tunataka kuwahakikishia kuwa ushindi ni wetu katika ‘round one’. Kwa hivyo, tunaomba ninyi watu wa Nairobi na wafuasi wa Kenya Kwanza kote mrauke mapema ili tumshinde huyu jamaa katika awamu ya kwanza,” akasema katika uwanja wa Kamukunji.

Kwa upande wake, Dkt Mutua alisema watafanya kila wawezalo kulinda kura zao za urais ili zisiibiwe akisema baadhi yao wamewahi kuhudumu serikalini na wanaweza “kuziba mianya ya wizi wa kura.”

“Dkt William Ruto amehudumu kama Naibu Rais kwa miaka 10 sasa. Mudavadi amewahi kuwa makamu wa rais na waziri serikali, Weta amewahi kuhudumu serikalini na hata mimi nimewahi kuwa msemaji wa serikali. Kwa hivyo, tunajua ukora wote wa kutekeleza wizi wa kura na tutatibua maovu hayo,” akaeleza.

Wanasiasa wa muungano wa Kenya Kwanza wamekuwa wakidai kuwa baadhi ya mawaziri serikalini wanapanga njama ya wizi wa kura kumwezesha Bw Odinga kushinda.

Awali, katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Dkt Ruto na Bw Gachagua waliidhinishwa kushiriki kinyangányiro cha urais kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alisema Dkt Ruto alitimiza matakwa yote yanayohitajika kwa wagombeaji urais kulingana na katiba, sheria husika na kanuni zote zilizowekwa.

“Ombi la William Ruto na mgombea mwenza wake la kutaka kushiriki katika uchaguzi wa urais Agosti 9, 2022 limekubaliwa,” alisema Bw Chebukati huku viongozi wa Kenya Kwanza, na wafuasi wa Dkt Ruto, wakishangilia.

Dkt Ruto alielezea imani yake kwa IEBC katika jitihada zao za kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao utaendeshwa kwa njia huru na haki na ambayo matokeo yake yataaminika.

“Ni furaha yangu kupokea cheti ambacho kitaniruhusu mimi na naibu wangu kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka huu. Bw Mwenyekiti, tumejitolea kudumisha kanuni ya nidhamu ambayo tumetia saini. Tutashirikiana na tume hii kwa dhati ili kufanikisha uchaguzi huu,” Dkt Ruto akasema.

Alisema amehimili vikwazo vingi vikiwemo vya watu wenye ushawishi serikali wanaodaiwa kuamua mshindi wa urais na kwamba, hakuna kizingiti kitakachomzuia kuwa rais wa Kenya akishinda uchaguzi.

Naibu Rais pia alilaani baadhi ya vyombo vya habari kwa kile alichodai ni kumbagua na kupendelea Bw Odinga.

You can share this post!

Misri, Ghana mawindoni kufukuzia nafasi ya kuingia AFCON...

Italia na Ujerumani watoshana nguvu katika pambano la...

T L