• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:20 PM
Italia na Ujerumani watoshana nguvu katika pambano la Nations League

Italia na Ujerumani watoshana nguvu katika pambano la Nations League

Na MASHIRIKA

CHIPUKIZI wa Italia waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya mabingwa mara nne wa dunia, Ujerumani, katika mchuano wa Uefa Nations League mnamo Jumamosi usiku mjini Bologna.

Baada ya kukosa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za Novemba-Disemba 2022 nchini Qatar, Italia wamepania kujisuka upya chini ya mkufunzi Roberto Mancni.

Kocha aliwajibisha idadi kubwa ya matineja dhidi ya Ujerumani huku Wilfried Gnonto, 18, akiridhisha zaidi. Chipukizi huyo wa FC Zurich nchini Uswisi alichangia bao ambao Italia walifungiwa na nahodha wa AS Roma, Lorenzo Pellegrini, katika dakika ya 70 kabla ya Ujerumani kusawazisha kupitia kwa Joshua Kimmich.

Matokeo hayo yaliendeleza rekodi nzuri ya Ujerumani ambao sasa hawajapoteza pambano lolote kati ya 10 yaliyopita chini ya mkufunzi mpya Hansi Flick aliyejaza nafasi ya Joachim Loew mnamo Julai 2021.

Ujerumani watavaana na Uingereza jijini Munich katika mechi ijayo ya Kundi A3 kwenye Nations League mnamo Juni 7, 2022. Uingereza wanaonolewa na kocha Gareth Southgate watashuka dimbani kwa ajili ya mchuano huo wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya Hungary kuwatandika 1-0 mnamo Jumamosi. Italia ambao ni mabingwa watetezi wa Euro, wataalika Hungaru.

Kati ya wanasoka wote waliowajibishwa na Italia dhidi ya Ujerumani, wa pekee mwenye tajriba pevu na anayejulikana sana miongoni mwa mashabiki wa kabumbu ni kipa wa Paris Saint-Germain (PSG), Gianluigi Donnarumma, 23, ambaye amevalia jezi za Italia mara 44.

Huku Ujerumani wakijiandaa sasa kualika Uingereza jijini Munich hapo kesho kwa mechi nyingine ya Kundi A3, Italia watakuwa wenyeji wa Hungary kabla ya kuvaana na Uingereza katika uwanja wa Molineux ambao hutumiwa na Wolverhampton Wanderers kwa ajili ya mechi zao za nyumbani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Nitabwaga Raila Agosti, asema Ruto

Antonio Rudiger aagana rasmi na Chelsea na kuyoyomea...

T L