• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 9:55 AM
Nitafurusha jeshi la Uganda kutoka Migingo – Raila

Nitafurusha jeshi la Uganda kutoka Migingo – Raila

IAN BYRON NA LEONARD ONYANGO

MWANIAJI wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga ameahidi kutimua wanajeshi wa Uganda kutoka kwenye Kisiwa cha Migingo kinachozozaniwa.

Bw Odinga alisema kuwa Migingo ni ya Kenya na wanajeshi wa Uganda hawafai kuendelea kuwa katika kisiwa hicho.

“Tayari nimezungumza na Rais Yoweri Museveni na nimemweleza kuwa Kisiwa cha Migingo ni cha Kenya.

“Nikichukua hatamu za uongozi wa nchi wavuvi wa Kenya wataenda kuvua samaki hadi upande wa Uganda kwa sababu samaki wengi walio katika Ziwa Victoria wanatoka upande wa Kenya,” akasema Bw Odinga alipokuwa akizungumza katika eneobunge la Nyatike, Kaunti ya Migori.

Bw Odinga alikutana na Rais Museveni katika Ikulu ya aila Entebbe mnamo Mei 2022, lakini haijulikani ikiwa mzozo kuhusu umiliki wa Kisiwa cha Migingo ni miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa.

Aidha, Bw Odinga aliahidi kuwapa mafunzo mapya maafisa wa polisi ili wawe na ‘utu’.

Alisema kuwa tofauti na polisi wa Tanzania na mataifa ya Magharibi, maafisa wa Kenya wamefunzwa kutesa na kudhulumu watu badala ya kuwahudumia kwa ukarimu.

“Sare, bunduki, mshahara, risasi na nyumba za polisi zinalipiwa ushuru na Wakenya. Hivyo polisi wanafaa kuhudumia raia na wala si kuwanyanyasa,” alisema Bw Odinga.

Kinara wa Azimio alionekana jana alionekana kukwepa kuwambia wakazi wa Migori kupigia kura wawaniaji wa Azimio huku akiwataka ‘kutumia akili’.

“Mnaona leo nimevalia nguo ya chama. Mfanye hivyo. Sitaki kuzungumza zaidi ya hapo; mjijazie,” akasema Bw Odinga.

Bw Odinga amekita kambi katika eneo la Nyanza katika juhudi za kuzima moto huku wawaniaji wa ODM wakikabiliwa na ushindani mkali.

Bw Odinga leo Ijumaa anazuru Kaunti ya Nyamira na Jumamosi atakuwa katika Kaunti ya Siaya ambapo wawaniaji wa ODM wanakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wagombea wa vyama vingine na wale wa kujitegemea.

Jumapili, Bw Odinga atakuwa katika Kaunti ya Homa Bay siku tatu baada ya mwaniaji mwenza wake Martha Karua kuzuru eneo hilo na kupigia debe wawaniaji wa ODM.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Chokoraa wangali tishio jijini

DOMO: Bahati asiye na bahati!

T L