• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Njama ya Kenya Kwanza kuzika ODM Pwani

Njama ya Kenya Kwanza kuzika ODM Pwani

MAUREEN ONGALA NA ALEX KALAMA

VIONGOZI wa vyama vinavyoegemea upande wa serikali ya Rais William Ruto, wameanza kuweka mipango ya kushawishi wenzao waliosalia upande wa Azimio la Umoja-One Kenya wajiunge nao.

Nafasi ambazo rais alitengea wanasiasa wa Pwani katika serikali yake, na utekelezaji wa ahadi alizotoa kwa Wapwani zimeibuka kuwa baadhi ya chambo kinachotumiwa katika mikakati hiyo.

Kufikia sasa, gavana mstaafu wa Kilifi, Bw Amason Kingi, alichaguliwa kuwa Spika wa Seneti, mwenzake wa Kwale akateuliwa kuwa waziri wa Uchimbaji Madini, Uchumi wa Baharini na masuala ya Ubaharia, huku aliyekuwa mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, akiteuliwa kuwa waziri wa Utumishi wa Umma na Jinsia.

Inatarajiwa kuwa wanasiasa wengine walioegemea upande wa Kenya Kwanza katika uchaguzi wa Agosti pia watazingatiwa kwa nyadhifa nyingine ikiwemo makatibu wa wizara, ubalozi na usimamizi wa mashirika ya serikali.

Rais Ruto pia alitoa amri kwamba shughuli za bandari zirudishwe Mombasa, na sasa hilo limeanza kutekelezwa.

Juhudi za kuunganisha viongozi wa Pwani kisiasa zimekuwa zikipata pigo kutokana na jinsi wanasiasa wanavyoegemea vyama tofauti.

Viongozi wa chama cha Pamoja African Alliance (PAA), kinachoegemea upande wa Kenya Kwanza, walisema tayari wameanza mipango ya kuendeleza mbele lengo lao la kuleta umoja wa Pwani kisiasa.

Kulingana nao, serikali tayari ishaonyesha nia ya kutendea Pwani mambo ambayo hayakushuhudiwa katika serikali zilizotangulia.

“Siasa imeisha na tunaganga yajayo. Sauti yetu haikuisha Agosti. Tumeanza safari ya kuunganisha Wapwani kuwa na sauti moja kwa sababu hivyo ndivyo maeneo mengine nchini yalivyoanya. Hakuna umuhimu wowote kuendelea kuunga mkono chama cha ODM kwani ni dhahiri kuwa PAA ndicho chama cha Pwani,” akasema Bw Ben Kai, ambaye aliwania useneta Kilifi kupitia kwa PAA.

Kulingana na Bw Kai, PAA inalenga ‘kuwatongoza’ wanasiasa katika vyama vingine katika eneo la Pwani kujiunga nao kwa manufaa ya Wapwani.

Kwa sasa, chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Raila Odinga, bado kina idadi kubwa ya viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi wa Agosti.

Vilevile, Bw Odinga alimshinda Dkt Ruto kwa wingi wa kura ukanda huo, ingawa pengo kati yao lilipungua ikilinganishwa na kura alizopata miaka iliyopita dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta.

Kati ya magavana watatu wastaafu Pwani; ni Bw Hassan Joho, ambaye pia ni naibu kiongozi wa ODM ndiye wa pekee aliye nje ya serikali.

Baadhi ya wazee wa Kaya za Mijikenda walisema kuwa njia pekee ambayo Pwani itafanikiwa kukabiliana na dhuluma za tangu jadi ni kwa wanasiasa kuungana na kushirikiana na serikali.

Wakizungumza Kilifi wikendi, walisema hatua ya Rais Ruto kumuunga mkono Bw Kingi kuwa spika wa seneti na kuwateua Bw Mvurya na aliyekuwa mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, kuwa mawaziri ni ishara ya nia njema aliyo nayo kwa Wapwani.

Vilevile, walisema hatua ya Rais kuamrisha huduma za bandarini zirudishwe Mombasa alipoapishwa imeleta matumaini kwamba atatekeleza ahadi nyingine alizotolea eneo hilo.

Msemaji wa Kaya Fungo, Bw Nguma Charo, alisema iwapo viongozi wa kisiasa wataungana ili kuzungumza kwa usemi mmoja bila kujali tofauti za mirengo yao ya kisiasa, itasaidia kusukuma ajenda nyingi zaidi za maendeleo.

“Viongozi wote wa kisiasa wakiwa pamoja tunaweza kumaliza matatizo yetu ya kihistoria kwa urahisi kama vile masuala ya ardhi,” akasema Bw Charo.

Vilevile alisema ingawa huduma za bandari zimerudi Mombasa, wangependa Rais ateue mwenyeji kama mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya.

Aidha, wazee hao wamemtaka Bw Kingi, Bw Mvurya, na Bi Jumwa kuwatembelea ili kupokea baraka za wazee baada ya kufanikiwa kupata nyadhifa za juu serikalini.

  • Tags

You can share this post!

Hofu njaa kuleta vurugu za kijamii

Magavana watafutia wachumba wao mlo

T L