• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Uhasama wa ndani watesa miungano

Uhasama wa ndani watesa miungano

NA WAANDISHI WETU

JINAMIZI la ushindani na kutoheshimiana limejitokeza katika mirengo ya Azimio-One Kenya na Kenya Kwanza, na kutishia kusambaratisha matumaini ya kunyakua nyadhifa mbalimbali.

Katika kila pembe ya nchi, wawaniaji walio na vyama vyao ndani ya miungano hiyo mikuu miwili, wameonyesha uadui na katika baadhi ya sehemu, hawaonani ana kwa ana.

Katika eneo la Mlima Kenya, maafisa wa serikali wamekuwa wakifanya kampeni ya kuwaambia wakazi kupigia kura wawaniaji wa Jubilee pekee katika maeneo ambayo kuna vyama vingine vishirika ndani ya Azimio.

Katika Kaunti ya Kirinyaga, anakotoka mwaniaji mwenza wa Azimio, Martha Karua wa Narc-Kenya, maafisa wa serikali wamekuwa wakifanyia kampeni wawaniaji wa Jubilee dhidi ya wenzao wa Narc-Kenya.

Hali ni sawa katika Kaunti ya Nyeri ambako maafisa wa serikali wanapigia debe Priscilla Nyokabi wa Jubilee dhidi ya Kabando wa Kabando wa Narc-Kenya.

Mivutano hii imezua taharuki kwa uongozi wa Azimio, hali iliyolazimisha waitishe kikao cha dharura Ijumaa iliyopita kujadili mbinu za kukomesha mivutano baina ya vyama vishirika katikaa muungano huo, hali ambayo wanahofia itagharimu muungano huo vyama kwa manufaa ya wapinzani wao wa Kenya Kwanza.

Muungano wa Kenya Kwanza nao unakumbwa na mizozano ya vyama tanzu hasa baada ya mwaniaji mwenza wake Rigathi Gachagua kuendeleza kampeni kali ya kuhimiza wakazi wapigie kura wawaniaji wa United Democratic Alliance (UDA) pekee.

Kampeni hiyo ya Bw Gachagua imezua uadui kati ya UDA na vyama washirika wake katika Kenya Kwanza, hali ambayo inatatiza.

Jumapili katika kaunti ya Machakos, wafuasi wa Nzioka Waita (Chama Cha Uzalendo) na Wavinya Ndeti (Wiper) ambao wako katika Azimio, walipigana Makonde mbele ya mwaniaji wao wa urais Raila Odinga.

Katika Kaunti ya Kwale, Naibu Gavana Fatuma Achani (UDA) na Chai Lung’anzi (PAA) kila mmoja amekuwa akijifanyia kampeni japo wameonekana katika ukumbi mmoja wakati wa mazishi ya baba yake Gavana Salim Mvurya eneo la Kasemeni, Kinango.

Hatua hiyo inaonekana kuwagawanya wapigakura katika kaunti hiyo.

Huku Bi Achani akifurahia uungwaji mkono kutoka kwa Bw Mvurya ambaye sasa ni mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Kenya Kwanza, Bw Lung’anzi pia anaungwa mkono na kiongozi wa PAA Amason Kingi, ambaye pia alipewa mamlaka ya kuratibu kampeni za Kenya Kwanza Pwani.

Hali ni sawa na hiyo upande wa Azimio ambako Prof Hamadi Boga (ODM) na Chirau Mwakwere (Wiper) wanazozana.

Prof Agnes Mwang’ombe (ANC) na Bw John Mruttu (UDA) kila mmoja anawania kivyake Taita Taveta, huku Dkt Ruto akitaka wapigakura wamchague mwaniaji wa UDA.

Mambo si tofauti Lamu, Kisii, Kajiado, Nakuru, Bungoma, Vihiga na kwingineko. Mizozo hii inatishia uwezo wao kushinda viti vingi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Katika Kaunti ya Bungoma, Seneta Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Mbunge wa Mt Elgon, Bw Fred Kapondi wamekuwa kama paka na panya.

Bw Kapondi ametangaza kuwa wawaniaji kupitia chama cha UDA hawatafanya tena kampeni za pamoja na wenzao wa Ford Kenya.

Akizungumza katika eneo la Kaptama, Bw Kapondi alishangaa ni vipi watafanya mikutano ya kampeni ya pamoja, ilhali viongozi wa Ford Kenya wamekuwa wakiwataka wapigakura wawakatae wawaniaji wa chama chake cha UDA.

“Hatuwezi kufanya kazi au kushirikiana na wenzetu ambao hawatuheshimu. Bw Wetang’ ula ameamua kuwa kampeni anazofanya akiwa na watu wa ANC ni za kutudhalilisha sisi watu wa UDA,” akasema.

Katika Kaunti ya Kajiado, Gavana Joseph ole Lenku (ODM) na mtangulizi wake David ole Nkedianye wako katika hali sawa na hiyo. Wawili hao ambao walibadilishana vyama, kila mmoja anavutia kwake.

Kisii inashuhudia ushindani mwingine ambapo mbunge wa Dagoreti Kaskazini Simba Arati wa ODM hasikizani na Sam Ongeri (DAP) na Chris Obure (Jubilee), wote wakiwa katika Azimio.

Ripoti za Winnie Atieno, Lucy Mkanyika, Cece Siago na Brian Ojamaa

  • Tags

You can share this post!

Uswisi waduwaza Ureno katika Uefa Nations League

Aliyeachiliwa na Rais asakwa kwa mauaji ya mamaye

T L