• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
ODM Kilifi wasema Raila akiamua ni hivyo

ODM Kilifi wasema Raila akiamua ni hivyo

NA MAUREEN ONGALA

VIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) katika Kaunti ya Kilifi wamesema kuwa bado watatii amri ya kingozi wao Raila Odinga na kuungana na Wakenya katika kaunti nyingine kufanya maandamano ya kupinga gharama ya juu ya maisha.

Wakiongozwa na Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo, viongozi hao walisema Jumanne kuwa watafanya maandamano ya amani katika kaunti hiyo na kuwaonya waandamanaji dhidi ya kupora na kuharibu mali.

Wakiwahutubia wanahabari katika hoteli moja nje ya mji wa Kilifi, Bw Madzayo alisema kuwa watawasilisha kilio chao kwa kamishna wa kaunti ya Kilifi katika muda huo wa maandamano.

Bw Madzayo alieleza kuwa viongozi wa ODM walishindwa kuwasilisha kilio chao wakati wa maandamano ya Jumatano wiki jana baada ya kutawanywa na polisi kwa kutumia vitoa machozi.

“Ni aibu sana kuona kuwa Wakenya ndani ya Kilifi wakiongozwa na wabunge wao ambao hawana kitu chochote cha kutekeleza uhalifu ama madhara yoyote wanasumbuliwa na kurushiwa vitoa machozi na polisi,” akasema.

Seneta huyo alisema polisi walitumia risasi kuwatawanya waandamanaji hao japo kuwa hakuna aliyejeruhiwa.

Mbunge wa Kilifi Kusini Bw Ken Chonga alisema kuwa maandamano ndiyo njia pekee ambayo imebakia kwa Wakenya kutoa kilio chao kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha nchini.

Alitoa wito kwa vitengo vya usalama kujumuika na Wakenya kupaza kilio chao.

“Tunawaalika hata polisi wakuje tuandamane pamoja kwa sababu tunataka maandamanao ya amani,” akasema.

Bw Chonga alidai kuwa viongozi wa ODM walikuwa na taarifa kuwa baadhi ya vijana katika mrengo wa Kenya Kwanza wana njama ya kuvuruga maandamano hayo ya amani na kutoa onyo kali kuwa watapambana nao vilivyo.

“Sisi hatuna mpango wa fujo lakini tunataka kuwapatia ilani wale vibaraka ya kwamba tuko tayari. Wakitaka amani tutaandamana kwa amani lakini wakitaka fujo pia hatushindwi,” akasema.

Spika wa bunge la kaunti ya Kilifi Bw Teddy Mwambire alisema kuwa maandamano yatafanyika katika sehemu tofauti ya kaunti ya Kilifi, ikiwemo Mtwapa na Mariakani katika eneobunge la Kilifi Kusini na Kaloleni.

Juma lililopita viongozi hao walijumuika na wafuasi wao katika maandamano mjini Kilifi katika eneobunge la Kilifi Kaskazini.

Mwenyekiti huyo wa chama cha ODM katika Kaunti ya Kilifi alitoa wito kwa wote watakaoandamana kutobeba silaha yoyote.

Hata hivyo, alisema kuwa huenda waandamanaji wakazua vurugu iwapo polisi wataingilia kati maandamano na kuanza kutupa vilipua machozi.

“Agizo kutoka kwa Kiongozi wetu ni kuwa kila mahali hata kijijini, Wakenya wanastahili kutoka na kutoa kilio chao kwamba hawaridhiki na jinsi mambo yanavyoendelea Tunatarajia kuwa polisi watatupa usalama wa kutosha tunapofanya maandamano yetu,” akisema.

Mbunge wa Malindi Bi Amina Mnyazi alisema kuwa anapinga dhana potovu inayoendelea miongoni mwa wakenya kuwa maandamano hayo ni ya chama cha ODM na kusema kuwa ni kilio cha Wakenya wote ambao wanazidi kuumia na garama ya maisha.

“Kuna watu huko nje wanajaribu kuchafua jina la ODM lakini haya sio maandamano ya ODMkwa sababu bei ya chakula imepanda na gharama ya maisha imekuwa ghali na inaathiri wafuasi katika mirengo yote ikiwemo Kenya Kwanza,”akisema.

Bi Mnyazi aliwakosoa viongozi ambao hawajiunga na Wakenya kutaka serikali kurudisha gharama ya maisha nchini kuwa wanawasaliti wafuasi wao.

Kwa upande wake mbunge wa Magharini Bw Harry Kombe amewataka Rais William Ruto na Kiongozi wa Azimio Raila Odinga kuketi chini na kuzungumzia swala nyeti la gharama ya maisha.

“Kuna haja ya ndungu hawa wawili pasipo Mkenya yeyote kuingilia kati kurudi katika hali yenu ya kisawa na mzungumze na kupata suluhu ya kudumu kwa swala la kupunguza gharama ya maisha nchini ili Wakenya wakafurahie utawala wa nchi yao,” akasema Bw Kombe.

Alitaka vyombo vya usalama kulinda wananchi na mali zao na kuacha kuwasumbua Wakenya wanaondamana.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Jinsi wanafunzi wa Chadwick walivyonogesha tamasha za...

Viongozi wa kidini wahimiza Ruto na Raila washauriane...

T L