• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 2:32 PM
Jinsi wanafunzi wa Chadwick walivyonogesha tamasha za muziki kanda ya Pwani

Jinsi wanafunzi wa Chadwick walivyonogesha tamasha za muziki kanda ya Pwani

NA SIAGO CECE

WANAFUNZI kutoka eneo la Pwani walipata fursa ya kuonyesha vipaji vyao katika tamasha za muziki zilizoandaliwa katika ukumbi wa Mvindeni, Kaunti ya Kwale.

Mamia ya wanafunzi walioshiriki kutoka shule za Pwani walionyesha vipaji vyao kutumia mashairi, densi na nyimbo za kisasa na kitamaduni.

Shule ya msingi ya Chadwick Academy kutoka katika Kaunti ya Mombasa ilikuwa moja ya shule katika mashindo hayo na densi ya “Ramogi Dance” iliyowaacha wengi wakiwa na hamu ya kutaka kutazama miondoko zaidi.

Haya yanajiri wazazi wakihimizwa kukuza talanta za watoto wao, mbali na masomo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Jackline Maseno alisema ni muhimu wazazi kukubali wanafunzi kuhusishwa katika densi na michezo tofauti mbali na vitabu.

“Katika mtaala wa kitambo, wazazi walikuwa wanazingatia masomo pekee, na baada ya siku  mwanafunzi anakosa talanta. Lakini mtaala huu unahimiza wanafunzi kujiunga na vilabu ambavyo vitakuza talanta yao,” Bi Maseno alisema.

Pia, alieleza tamasha hizo zinatayarisha wanafunzi kwa maisha ya kesho kwa kutambua na kukuza talanta zao.

Tamasha hizo ziliandaliwa ili kupata washindi kwa kila kitengo ambao watashiriki katika mashindano ya kitaifa baadaye muhula huu.

Wanafunzi walichorwa usoni, na kuvalishwa kamba na nguo za kitamaduni, yaani maleba, huku wakitumia ngoma na firimbi wakati wa kuimba na kucheza.

Mwalimu wa muziki wa shule hiyo Everlyne Akinyi alisema wimbo huo ni njia moja ya kuonyesha tamaduni kutoka maeneo tofauti ya taifa na pia kutumbuiza watu.

“Densi hii huimbwa na jamii ya Wajaluo, na huimbwa wakati wa sherehe,” Bi Akinyi alieleza.

Biden Ochieng’ mmoja wa wanafunzi, mwenye umri wa miaka 13 ambaye aliongoza wenzake wa shule ya Chadwick kwa nyimbo hizo alisema kuwa talanta yake ni ya kuimba.

“Nafurahi kuwa kuhudhuria tamasha hizi. Zinanifanya niendeleze kipaji changu na pia nikutane na wanafunzi kutoka shule tofauti,” Biden alisema, akieleza kuwa angependa kuwa mwanamuziki siku za usoni.

Mbali na densi hiyo ya Ramogi, shule nyingine zilishiriki kwa densi za taarabu, za Mijikenda, nyingine zikitumbuiza na nyimbo za kisasa.

Washiriki walikuwa wa shule za chekechea, msingi na za upili eneo la Pwani.

  • Tags

You can share this post!

Wanahabari wafukuzwa kikao cha kusikiliza kesi dhidi ya...

ODM Kilifi wasema Raila akiamua ni hivyo

T L