• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
ODM walemea Kenya Kwanza ubunge Pwani

ODM walemea Kenya Kwanza ubunge Pwani

NA WAANDISHI WETU

MATOKEO ya awali ya uchaguzi wa ubunge katika kaunti za Pwani, yameonyesha Muungano wa Kenya Kwanza ukilemewa kupata ushindi wa viti vya ubunge dhidi ya ODM.

Kufikia wakati wa gazeti la Taifa Leo kwenda mitamboni, Chama cha ODM kinachoongozwa na mgombeaji urais wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Bw Raila Odinga, kilikuwa kikielekea kuendeleza udhibiti wake wa siasa za ukanda huo kupitia kwa ubunge.

Chama hicho, kilikumbwa na makabiliano makali ya kisiasa kutoka kwa UDA kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto, na PAA kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Ushindani ulioshuhudiwa wakati wa kampeni ulitishia kutikisa udhibiti ambao Bw Odinga amekuwa nao Pwani kwa miaka mingi sasa.

Hata hivyo, matokeo ya mwanzo ambayo bado yalikuwa yanasubiriwa kutangazwa rasmi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), yalionyesha UDA na PAA zingali na kibarua kigumu kupenya katika ukanda huo kisiasa.

UDA ilikuwa mbele katika maeneobunge mawili pekee, ambayo ni Nyali (Mombasa) na Msambweni (Kwale).

Kwa upande wake, PAA ilitangazwa mshindi katika eneobunge la Kinango (Kwale) ambapo mgombewaji wake alikuwa ni Bw Gonzi Rai, huku ikiongoza Rabai na Ganze, Kaunti ya Kilifi.

Chama cha ANC ambacho kiko ndani ya Kenya Kwanza kilikuwa kinaongoza katika eneobunge la Matuga.

Baadhi ya wanasiasa ambao kufikia jana walikuwa wametangazwa kushinda kupitia tikiti ya ODM ni Bw Rashid Bedzimba, aliyewania ubunge Kisauni, Kaunti ya Mombasa, na Said Hiribae aliyewania ubunge Galole, Kaunti ya Tana River.

ODM ilikuwa inaongoza kwa idadi za kura za ubunge katika maeneobunge ya Mvita, Likoni, Changamwe na Jomvu yaliyo Kaunti ya Mombasa.

Katika Kaunti ya Kilifi, chama hicho kilikuwa kinaongoza Malindi, Kilifi Kaskazini, Kilifi Kusini, Magarini na Kaloleni, mbali na eneobunge la Garsen (Tana River).

Chama cha Wiper, kilicho chama tanzu cha Azimio, kilizoa ushindi katika maeneobunge ya Wundanyi, Taveta na Voi, Kaunti ya Taita Taveta, ambapo waliotangazwa washindi ni Danson Mwashako, John Bwire na Abdi Chome mtawalia.

Kwa upande mwingine, Jubilee ambacho pia kiko ndani ya Azimio, kilikuwa mbele katika maeneobunge ya Mwatate (Taita Taveta), Lamu Mashariki, na Lamu Magharibi.

Licha ya hayo, ODM ilipata pigo katika Kaunti ya Kilifi baada ya wimbi la Kenya Kwanza kusambaratisha udhibiti wake wa bunge la kaunti hiyo.

Katika uchaguzi wa 2017, chama hicho kilizoa karibu viti vyote vya udiwani lakini matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanywa Jumanne, yameonyesha vyama vya UDA na PAA kwa pamoja vimemega viti karibu sawa na vile vya ODM.

Kutoka kwa jumla ya wadi 35, hesabu za kura ambazo bado hazijatangazwa rasmi na IEBC zilionyesha ODM ikiwa na ushindi katika wadi 15, huku PAA ikishinda katika wadi nane na UDA wadi sita.

Madiwani watatu walishinda wakiwa wagombeaji huru, huku vyama vya Jubilee, Shirikisho na ANC vikiwa na wadi moja moja.

  • Tags

You can share this post!

Bedzimba avunja ‘mkosi’ akipewa fursa tena Kisauni

DOMO: Kagundua followers sio wapigakura

T L