• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Pesa za Ruto zamgeukia

Pesa za Ruto zamgeukia

Na WAANDISHI WETU

MIZOZO ya mara kwa mara kati ya viongozi na wafuasi wa Naibu Rais William Ruto, kuhusu mamilioni ya pesa ambazo hutoa kila anapozuru maeneo tofauti ya nchi imeanza kuwa tishio kuu kwa kampeni zake za urais.

Katika eneo la Pwani, mizozo inazidi kutokota Kaunti za Mombasa, Kilifi na Taita Taveta ambapo makundi ya vijana yanalaumu wanasiasa wakidai wamekatalia pesa ambazo Dkt Ruto alitangaza kuwaachia alipokita kambi huko hivi majuzi.

Maeneo mengine nchini ambapo mizozo aina hiyo imewahi kutokea ni Makueni, Busia, Sotik katika Kaunti ya Bomet, na Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

Katika Kaunti za Mombasa, Kilifi na Kisumu, makundi yameibuka pia kuwapinga aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, na mtaalamu wa kupanga mikakati ya kisiasa, Bw Eliud Owalo ambao ni vinara wa kampeni za Dkt Ruto katika maeneo hayo mtawalia.

Imebainika mojawapo ya chanzo cha mizozo hii ni mvutano kuhusu usimamizi wa pesa ambazo hutumiwa kugharamia kampeni zake, kando na zile ambazo yeye huwaachia viongozi kugawia makundi ya kijamii.

Kisa cha hivi punde zaidi kilitokea Jumatatu wakati walimu wawili waliponea chupuchupu walipodaiwa kuhepa na Sh1m zilizotolewa na Naibu Rais kwa wahudumu wa bodaboda.

“Wawili hao walitoroka hadi katika kituo cha polisi kwa usalama wao lakini wahudumu wa bodaboda wakawafuata huko wakitaka polisi wawatoe nje ili wawaadhibu. Uchunguzi unaendelea kuhusu kisa hicho,” ripoti ya polisi ikasema.

Mjini Mombasa, wafanyabiashara katika soko la Kongowea na wahudumu wa bodaboda katika eneo la Jomvu walilalamika kutopokea Sh3 milioni walizoachiwa na Naibu Rais, karibu wiki mbili baada ya Dkt Ruto kufanya kampeni hapo.

“Kati ya Sh2 milioni ambazo Naibu Rais alitoa, kuna sehemu nyingine watu walipewa Sh5,000 kila mmoja ilhali wengine wakapewa Sh100 na hata Sh50. Tunahangaika ilhali alitupiga jeki. Tunampenda sana lakini wanaomzunguka ni walaghai,” akasema mwenyekiti wa wachuuzi wa Kongowea, Bw Richard Nyangoto.

Lalama hizo zilitokea wakati mzozo wa Sh1.2 milioni zilizotolewa kwa vijana na Dkt Ruto umewagawanya viongozi wanaoegemea Chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika Kaunti ya Kilifi. Bi Jumwa, alidai baadhi ya wanasiasa walitaka kutwaa hela hizo kwa manufaa yao wenyewe. “Katika orodha ya watu iliyowasilishwa kwangu, niligundua majina 50 ni ya wanasiasa,” alisema Bi Jumwa, alipozungumza katika soko kuu la Gongoni lililoko Magarini, Kaunti ya Kilifi.

Baadhi ya viongozi wanaoegemea UDA walikuwa wamemlaumu wakidai alitoroka na pesa hizo.

Bw Furaha Ngumbao anayetarajia kuwania udiwani kupitia kwa UDA, alidai mbunge huyo hajajitolea kushirikiana na wenzake katika kampeni.

“Sitafanya kazi tena na Aisha japo nitakitafutia kura chama cha UDA kwa udi na uvumba nihakikishe kuwa naibu rais Dkt William Ruto anakuwa rais wa Kenya,” akasema Bw Ngumbao.

Dkt Ruto alipokuwa ziarani Busia wikendi, kulitokea rabsha ambapo ilidaiwa vijana waliohusika walitaka walipwe Sh400,000.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Bw Martin Andati, mivutano ya viongozi na wafuasi wa Dkt Ruto itahatarisha kampeni zake za urais na za UDA kwa jumla.

Alitoa mfano wa uchaguzi mdogo wa Matungu ambako UDA ilishindwa, akisema kuna uwezekano mkubwa matokeo hayo ni kwa sababu ya mivutano ya viongozi wa Magharibi wanaomuunga mkono.

Imebainika kuwa, idadi ya wabunge wanaoegemea upande wa Naibu Rais eneo la Magharibi imezidi kupungua ikiaminika mojawapo ya sababu ni mzozo kuhusu usimamizi wa fedha za kampeni.

Katika kampeni zake awali, Naibu Rais alikuwa akiandamana na zaidi ya wabunge kumi akizuru eneo hilo.

Baadhi yao ni Mwambu Mabonga (Bumula), Dan Wanyama (Webuye Magharibi), John Waluke (Sirisia) na Didmus Barasa (Kimilili).

Kikosi hicho kilikuwa pia na Emmanuel Wangwe (Navakholo), Bernard Shinali (Ikolomani), Malulu Injendi (Malava), Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), na Charles Gimose (Hamisi).

Kando na hao, kuna aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale na aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa.

Ripoti za Winnie Atieno, Shaban Makokha, Alex Kalama na Valentine Obara

You can share this post!

Wataalamu wahimizwa kusaidia wafanyakazi kiakili

Ingwe imani tele itafufuka timu zikijiandaa kwa ligi

T L