• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Raila adokeza kuhudumu kwa muhula mmoja akishinda urais 2022

Raila adokeza kuhudumu kwa muhula mmoja akishinda urais 2022

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amedokeza kuwa atahudumu kwa muhula mmoja pekee endapo atachaguliwa kuwa rais wa tano wa Kenya katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Kwenye mahojiano ya moja kwa moja na runiga ya Citizen, Jumatano usiku, Bw Odinga alisema lengo lake kuu ni kuendeleza maendeleo ambayo yameanzishwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“Hamna shida, mbona nisihudumu muhula mmoja? Inawezekana! Nataka kuendeleza Kenya mahala ambapo Rais Uhuru Kenyatta atakuwa ameachia. Namshukuru kwa kuanzisha miradi ya miundomsingi kama vile ujenzi wa barabara ya kisasa, reli kati ya miradi mingine. Ninataka kufanya mengi kuzidi hayo ili kuiweka Kenya katika kiwango kimoja na mataifa mengine yaliyostawi ulimwenguni; mataifa kama vile ya bara Asia ambayo yalikuwa kiwango sawa kimaendeleo na Kenya katika miaka ya sitini yaani 1960s,” akasema Bw Odinga.

“Ninaamini kuwa ninaweza kutekeleza wajibu huo licha ya kuwa na umri mkubwa. Rais Joe Biden wa Amerika amenizidi kiumri kwa mwaka mmoja lakini analiongoza taifa hilo vizuri,” waziri huyo mkuu wa zamani akaongeza.

Bw Odinga alikariri kuwa hana nia ya kusalia mamlakani kwa kipindi kirefu bali anataka kuweka msingi bora wa uongozi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa ODM kudokeza kuwa huenda asiwanie urais kwa mara nyingine katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Kuhusu iwapo atakubali kushindwa katika uchaguzi wa urais mwaka 2022, Bw Odinga alisema atakubali kushindwa iwapo uchaguzi huo utaendeshwa kwa njia ya haki.

“Kama mwanademokrasia, nitakubali kushinda au kushindwa. Ikiwa nitashindwa kwa njia ya haki, nitakubali. Nimewahi kuwa mwanakandanda na ninafahamu fika kwamba ukishindwa, unakubali. Asiyekubali kushindwa si mshindani,” akakariri.

Kwa mara nyingine Bw Odinga alikana madai ya mrengo wa Naibu Rais William Ruto kwamba yeye ni mradi wa Rais Kenyatta kutokana na sababu kwamba kiongozi wa taifa anaonekana kuunga mkono azma yake ya urais.

“Sitaki kuidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta lakini ninataka kura yake. Ikiwa Rais atanipa kura yake, nitashukuru zaidi,” Bw Odinga akasema.

Wanasiasa wandani wa Dkt Ruto wamedai kila mara kwamba Bw Odinga ni “mradi wa serikali” katika kinyang’anyiro cha urais na ndiyo maana anaungwa mkono na mawaziri kadhaa serikalini.

Dkt Ruto na Bw Odinga ndio wanachukuliwa kuwa wagombeaji wakuu wa urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

  • Tags

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: ‘Nimefika kuchelewa’ ni dhana isiyo na...

Waheshimiwa bila heshima

T L