• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
Waheshimiwa bila heshima

Waheshimiwa bila heshima

Na CHARLES WASONGA

FUJO zilitanda bungeni Jumatano alasiri wabunge walipopigana wakati wa mjadala kuhusu Mswada tata wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Kisiasa.

Wabunge wa mirengo ya Tangatanga na handisheki walirushiana chupa za maji wakibishania madai ya wizi wa kura wakati wa upigaji kura kuhusu pendekezo la kuondolewa kwa sehemu ya mswada huo unaopendekeza kuundwa chama cha muungano. Hoja hiyo iliwasilishwa na Mbunge wa Kandara Alice Wahome, mfuasi sugu wa Naibu Rais William Ruto.

Spika wa muda Chris Omulele alilazimika kusitisha kwa muda shughuli za kikao hicho maalumu cha bunge hilo ili kutuliza joto.

Hata hivyo, tulipokuwa tukienda mitamboni saa kumi na mbili jioni, mrengo wa handisheki chini ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, ulifaulu kuangusha pendekezo hilo la Bi Wahome kwa kura 158 dhidi ya kura 134 za wabunge wa tangatanga.

Baada ya hali kutulia, Bw Omulele alimtimua Kiongozi wa Wachache John Mbadi kutoka bungeni kwa kumshambulia na kumjeruhi Mbunge wa Sigowet/Soin Benard Koros wakati wa sokomoko hilo.

“Mheshimiwa Spika nimejeruhiwa. Inaskiitisha kuwa nimejeruhiwa ndani ya bunge hili lenye hadhi. Nimeshambuliwa na shujaa wa fujo katika bunge hili. Hatuwezi kukubali kujeruhiwa katika bunge hili, Uhuni kama huu haufai kuruhusiwa kuendelea Mheshimiwa Spika,” akalalamika Bw Koros.

Mbunge huyo, ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto, alijeruhiwa usoni, na kutokwa damu, wakati wa makabiliano hayo yaliyodumu wa karibu dakika 15.

“Kwa kuzingatia sheria nambari 107 na kuthibitisha kwamba John Mbadi alimshambulia mbunge wa Sigoweti/Soin nakuamuru wewe Mbadi uondoke katika kikao cha leo. Umezimwa kuhudhuria vikao vitano vya bunge hili,” akaamuru Bw Omulele.

Bw Omulele pia walitoa onyo kali kwa wabunge David Sankok (Maalum), Wafula Wamunyinyi (Kanduyi), John Kiarie (Dagorreti Kusini) Bi Wahome (Kandara) na David Gikaria (Mbunge Mashariki) kwa “kudhihirisha utovu wa nidhamu” wakati wa vurumai hizo.

“Ewe Mheshimwa Sonkok, nimeshuhudia ukirusha chupa za maji lakini nakuonya kwamba usirudie kosa hilo. Na enyi waheshimiwa Alice Wahome, Wamunyinyi, Gikaria na wewe John Kiarie nilishuhudia vituko vyenu vilivyoonyesha utovu wa nidhamu. Ni jambo la kusikitisha mno, tabia zenu zinashusha hadhi ya bunge hili,” Bw Omulele akaonya.

Lakini akiongea na wanahabari dakika chache baada ya kufurushwa, Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini alijitetea akisema alifumania Bw Koros akishiriki wizi wa kura.

“Nilimpata huyo mbunge, ambaye simfahamu lakini nasikia anaitwa Koros, nilimpata akiandika jina la mbunge mwingine ambaye hakuwepo. Makarani walipojaribu kumzuia kufanya hivyo ndipo akazua fujo na ikabidi nimburute kutoka mezani,” akasema Bw Mbadi ambaye pia ndiye mwenyekiti wa kitaifa wa ODM huku akidai yeye pia alijeruhiwa kidole.

Awali, cheche zilitanda bungeni wabunge wa ‘Tangatanga’ walipomzomea kiongozi wa wengi, Amos Kimunya kwa kumkosea heshima Bi Wahome.

Mbunge huyo alihoji uelewa wa Bi Wahome wa sheria kwa kudai mswada huo unakiuka kipengele cha 91 na kile cha 260 kwa kupendekeza kuundwa wa chama cha muungano.

“Sijui ni chuo kipi cha uanasheria Mheshimiwa Wahome alihudhuria kwa sababu kama mwanasheria anapaswa kuelewa kwamba mswada huu haujakiuka Katiba kwa njia yoyote. Aidha, ni wazi kuwa haelewi namna sheria hutengenezwa katika bunge hili,” akasema Bw Kimunya.

Hapo ndipo wabunge wa ‘Tangatanga’ walimfokea kwa kusema, “Kimunya must go! Kimunya must go! (Kimunya aende! Kimunya aende!)

Bw Kimunya akajibu: “Nimezoe kelele zikiwemo hizo za Kimunya must go.”

Akitetea pendekezo lake Bi Wahome alilalamika kuwa sehemu ya sita ya mswada huo inakiuka katiba kwa kupendekeza kuundwa kwa chama cha muungano.

“Bunge hili litakuwa likihujumu vipendele vya 91 na 260 kuhusu sifa za vyama vya kisiasa endapo tutapitisha mswada huu jinsi ulivyo. Ndiposa napendekeza kuondolewa kabisa sehemu ya sita ya mswada huo,” akasema Mbunge huyo wa Kandara.

Awali, wabunge wa ‘Tangatanga’ walionekana kuzua aina mbalimbali za ubishi ili kupoteza wakati na kwa lengo la kuhujumu kukamilishwa kwa mswada huo kama ilivyoratibiwa na afisi ya Spika wa Bunge Justin Muturi.

You can share this post!

Raila adokeza kuhudumu kwa muhula mmoja akishinda urais 2022

Mbinu za mrengo wa ‘Tangatanga’ kuchelewesha...

T L