• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
CECIL ODONGO: Raila akiacha dhana ya ‘mradi’ ishike atajilaumu

CECIL ODONGO: Raila akiacha dhana ya ‘mradi’ ishike atajilaumu

Na CECIL ODONGO

KINARA wa ODM Raila Odinga na wandani wake wanafaa waweke mikakati ya kukabiliana na dhana inayoendelezwa na mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto kuwa yeye ni mradi wa serikali.

Dhana kuwa Bw Odinga ni mradi wa Jubilee itachangia kuuzima umaarufu wake na kumyima kura nyingi wakati huu ambapo anajikakamua kupata angalau umaarufu wa maana hasa katika eneo la Mlima Kenya ambako Dkt Ruto anajivunia uungwaji mkono mkubwa.

Bw Odinga amekuwa akifahamika kama mwanasiasa mzalendo ambaye amepigania maslahi ya raia na uhuru wa kujieleza nchini. Hasa anakumbukwa kwa kupigania mfumo wa vyama vingi kando na kusaidia nchi kupata katiba mpya ya 2010 ambayo imeleta mfumo unaoshabikiwa mno wa ugatuzi uliosambaza maendeleo mashinani.

Kando na hayo, siasa za waziri huyo mkuu wa zamani zimekuwa zikijikita katika uanaharakati ambao umemvunia ushabiki mkubwa hasa kutoka maeneo ambayo yalitelekezwa na kupitia dhuluma za kihistoria wakati wa tawala ziliopita.

Hata hivyo, kumsawiri kama mradi wa serikali kutaondoa sifa hizi zote ambazo Bw Odinga amekuwa akijivunia kwa miaka mingi. Kwanza hili la mradi ni mbinu ya Dkt Ruto kujitoa katika makosa ya utawala wa Jubilee kisha Bw Odinga alaumiwe.

Mara si moja, Dkt Ruto amekuwa akidai kuwa Jubilee haijaweza kuafikia malengo yake ya kuwapa Wakenya miradi iliyoahidi hasa katika kipindi hiki cha pili baada ya Bw Odinga kuridhiana na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2018.

Ingawa hivyo, inafahamika kuwa Jubilee hata kipindi chake cha kwanza haikuwatimizia Wakenya miradi mingi iliyoahidi ila ilizingirwa na sakata nyingi za ufisadi. Hata ahadi ya kuwapa wanafunzi vipakatalishi imesalia ahadi hewa na haijatekelezwa kikamilifu hadi leo.

Hizi lawama zote huenda zikaangukia Bw Odinga iwapo Dkt Ruto atafanikiwa kumsawiri kama mradi wa serikali. Katika eneo la Mlima Kenya, wakazi wameeleza kero lao dhidi ya utawala wa Jubilee hasa baada ya kuporomoka kwa viwanda na bei ya majanichai na kahawa kushuka.

Kuna imani kuwa anayeingia mamlakani iwapo anaungwa mkono na utawala uliopo ataendeleza sera za serikali hiyo. Kutokana na kufeli kwa serikali ya Jubilee katika nyanja mbalimbali, Wakenya wengi hawatamshabikia mwanasiasa ambaye ataendeleza utawala wa sasa uliochangia sana ugumu wa maisha ikilinganishwa na enzi za Rais Kibaki.

Vilevile, viongozi ambao hutajwa kama miradi huwa hawafaulu katika uchaguzi mkuu. Rais Uhuru Kenyatta alianguka kura vibaya mnamo 2002 kwa kuwa alikuwa mradi wa marehemu Rais Daniel Arap Moi wakati wa siasa za urithi.

Vivyo hivyo, mnamo 2013 ilidaiwa kuwa Kinara wa ANC Musalia Mudavadi alikuwa akipigiwa upatu na Rais Mstaafu Mwai Kibaki. Madai hayo yalichangia kushuka kwa umaarufu wa Bw Mudavadi ambaye wakati moja alikuwa karibu kushirikiana na Rais Kenyatta na Dkt Ruto ili kuwa mwaniaji wa Urais wa muungano wao ila hilo halikutimia.

Kwa hivyo, ODM wanafaa wawe wajanja na kubuni njia ya kuondoa hii dhana ya kuwa Raila ni mradi wa serikali. Mfumo wao wa kuwapa vijana wasiokuwa na ajira na pia familia maskini Sh6,000 kila mwezi unaonekana kufanya vyema dhidi ya sera ya ‘Bottom Up’ ya Dkt Ruto na vivyo hivyo, watafaa kukabili hili la Bw Odinga kuwa mradi wa serikali.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Changamoto tele Mlima ukijaribu kuja pamoja

Raila alilia vijana Nyanza wajisajili kwa kura za 2022

T L