• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 2:12 PM
Raila akunja mkia kuhusu vyama tanzu

Raila akunja mkia kuhusu vyama tanzu

BENSON MATHEKA Na GEORGE ODIWUOR

MGOMBEA urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga ameonekana kuingiwa na baridi na kuacha kushinikiza wagombeaji wa vyama tanzu vya muungano huo kujiondoa na kuunga wale walio maarufu.

Bw Odinga na Baraza Kuu la Azimio, walikubaliana kuwa ili kuimarisha nafasi ya muungano huo kushinda viti vingi, wagombeaji wasio maarufu wa vyama tanzu wajiondoe na kuwaachia wale maarufu.

Hata hivyo, pendekezo hilo lilipingwa na baadhi ya wagombeaji hasa wa vyama vidogo waliohisi kuwa hatua hiyo ingenufaisha vile vikubwa katika muungano huo.

Mnamo Jumamosi akiwa Siaya, Bw Odinga alionekana kuacha mpango huo ambao ulikuwa umezua uhasama na mihemko ndani ya Azimio na kutishia kuvuruga mikutano yake ya kampeni maeneo tofauti nchini.

“Hakuna mgombeaji atalazimishwa kujiondoa japo uhasama wa ndani unaweza kunyima muungano wetu baadhi ya viti ambavyo tungeshinda kwa kuweka nguvu zetu pamoja,” alisema Bw Odinga.

Alisema pendekezo hilo lilikuwa mkakati wa Azimio kushinda viti vingi katika viwango vya kaunti na kitaifa lakini hakuna atakayelazimishwa kujiondoa.

“Tukiwa na vyama 24 ndani ya Azimio, tuligundua kwamba kuwa na wagombeaji wengi katika kiti kimoja kutatufanya tushindwe katika maeneo tulio na umaarufu hata wa zaidi ya asilimia 70,” akasema waziri mkuu huyo wa zamani.

Aliongeza kuwa pendekezo hilo lilikubaliwa na vyama tanzu ili muungano pinzani wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto, usipenyeze katika ngome zao na kushinda viti.

“Katika baadhi ya viti, Azimio iko na wagombeaji watano huku wapinzani wetu wakiwa na mmoja. Hii inaweza kutufanya tupoteze viti ambavyo tungeshinda kama tungekubaliana kama muungano,” akasema Bw Odinga.

Hofu nyingine ya kiongozi huyo wa chama cha ODM ni kwamba; wagombeaji huru wanaweza kushinda viti katika ngome za muungano huo hasa kwa vile wagombeaji waliopendekeza wajiondoe wamekataa kubanduka.

Akiwa katika ziara ya kampeni eneo la Nyanza wikendi, Bw Odinga aliwarai wapigakura kuwachagua wagombeaji wa chama cha ODM ili kumwezesha kuwa na nguvu akishinda urais na kuunda serikali baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Nimetembea kila eneo Kenya kuomba kura na azma yangu imeungwa na wengi. Ninawaambia kuwa wanafuatilia kuona jinsi watu wangu watakavyofanya Agosti 9,” alisema.

“Msiniangushe kwa kukataa kuchagua wagombeaji wa ODM,” alisema.

Kauli yake ilijiri wakati ambao wagombeaji wa ODM katika ngome yake ya Nyanza wanakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wagombeaji huru na vyama tanzu vya Azimio.

“Hebu fikiria baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti vinara wa Azimio wakiketi kupanga mambo na kisha Bw Odinga awasilishe viongozi wachache waliochaguliwa. Tafadhali tumwepushie aibu hiyo kwa kuchagua wagombeaji wa ODM pekee,” akasema mwenyekiti wa ODM, Bw John Mbadi.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya kuendelea kununua unga wa mahindi kwa bei ghali

WANDERI KAMAU: Ewe Dkt Ruto kisasi kamwe hakijengi bali...

T L