• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Raila alivyochezwa

Raila alivyochezwa

NA WANDERI KAMAU

IMEFICHUKA kuwa huenda maafisa wa ngazi za juu katika serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta walimcheza kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, kwamba wangemsaidia kutumia nguvu ya serikali kushinda urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

Ijapokuwa Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilitumia njia za kichinichini “kumnyang’anya” ushindi wake, msimamo huo unatofautiana vikali na kauli zinazoendelea kutolewa na maafisa waliosimamia mikakati ya kampeni za Azimio kwenye uchaguzi huo.

Kulingana na Profesa Mutahi Ngunyi, aliyehudumu kama mshauri wa mikakati ya kisiasa kwa Bw Kenyatta, maafisa wengi katika serikali hiyo “hawakujitayarisha vilivyo” kumsaidia Bw Odinga kushinda urais kwenye uchaguzi huo.

“Maafisa wengi waliofaa kutoa usaidizi wa vifaa, mipango na ujasusi walilegea kimakusudi, kwani wengi hawakuwa na ufahamu wowote kuhusu vile wangemfanyia kampeni Bw Odinga,” akasema Prof Ngunyi kwenye mahojiano na wanahabari wa shirika la Nation Media Group.

Prof Ngunyi anadai kuwa Bw Kenyatta alipuuza ushauri wake kwamba ilikuwa vigumu kumuuza Bw Odinga katika baadhi ya maeneo, hasa eneo la Kati.

“Nilimwambia (Uhuru) kwamba nilikuwa na tatizo kuhusu vile alikuwa akimfanyia kampeni Bw Odinga. Nilimwambia ikiwa angetaka kufaulu kumfanyia kampeni Bw Odinga, alifaa kufanya mambo mawili; kwenda kwa wananchi kumfanyia kampeni na kutumia nguvu za serikali (Deep State) kuhakikisha Bw Odinga ameibuka mshindi. Hata hivyo, hakuna lolote kati ya hayo yalifanyika,” akasema Prof Ngunyi.

Kauli za msomi huyo zinajiri miezi michache baada ya matamshi kama hayo kutolewa na Bw Saitabao Ole Kanchory, aliyehudumu kama Ajenti Mkuu wa Urais wa Bw Odinga kwenye uchaguzi huo.

Mnamo Aprili, Bw Kanchory alizua hisia kali katika mrengo wa Azimio, baada ya kudai kuwa Bw Odinga “alisalitiwa na washirika wakuu aliowategemea kumsaidia kuendesha na kusimamia kampeni zake”.

Kwenye kitabu chake “Why Raila is not the 5th” (Sababu Raila si Rais wa Tano), Bw Kanchory anasema kuwa wasimamizi wa mikakati katika Azimio walipuuza ushauri muhimu waliokuwa wakipewa kuhusu njia ambazo wangetumia kuboresha kampeni za Bw Odinga.

“Bw Odinga alisalitiwa na watu aliowategemea kuendesha kampeni zake. Baadhi walikosa kuzingatia ushauri tuliowapa. Binafsi, ushauri wangu ulipuuzwa na nikafurushwa kutoka kundi la watu waliofaa kumpa Raila mwongozo,” akaeleza Bw Kanchory.

Kulingana na wadadisi, kauli za Prof Mutahi na Bw Kanchory zinaonyesha kuwa Azimio inafaa kujilaumu yenyewe kwa kukosa kutwaa ushindi kwenye uchaguzi huo.

Bw Odinga alishindana na Rais William Ruto, aliyewania urais kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Baadhi ya wanasiana na maafisa wa ngazi za juu waliotajwa na Bw Kanchory “kumwangusha” Bw Odinga, ni Kiranja wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed, aliyekuwa msemaji wa Sekretariati ya Azimio Prof Makau Mutua, aliyekuwa Waziri wa Habari na Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru kati ya wengine.

Hata hivyo, wamejitokeza na kupuuza madai yake.

  • Tags

You can share this post!

Washwash: Raia wa Nigeria wamnyoa mfanyabiashara Sh60m...

Kenya Shujaa yaanza maandalizi ya kushiriki Kombe la Afrika

T L