• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Raila apokonywa mamlaka ya kuteua mgombeaji mwenza wake

Raila apokonywa mamlaka ya kuteua mgombeaji mwenza wake

NA CHARLES WASONGA

MWANIAJI urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga sasa amepokonywa mamlaka ya kuamua ni nani atakuwa mgombeaji mwenza wake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Badala yake uteuzi wa mgombeaji mwenza wake sasa utafanywa na jopo maalum ambalo litateuliwa na Baraza Kuu la Azimio linaloongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Hii ni mojawapo ya maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano wa kwanza wa baraza hilo ambao ulifanyika Alhamisi, Aprili 21, 2022 katika jumba la mikutano ya kimataifa la Kenyatta (KICC) jijini Nairobi.

“Tumelipa jopo la ushauri wajibu wa kupendekeza watu ambao wanahitimu kuwa wagombeaji wenza, ili mmoja wao apendekezwe kwa mgombeaji urais wa Azimio,” akasema Katibu Mkuu wa baraza hilo Junet Mohamed kwenye kikao na wanahabari baada ya mkutano huo.

Hata hivyo, Bw Mohamed, ambaye ni Mbunge wa Suna Mashariki, hakutaja majina ya wanachama wa jopo hilo.

Vile vile, hakutaja ni lini jopo hilo litakamilisha shughuli ya kutambua watu wanaofaa kwa wadhifa huo.

Kumekuwa na vuta nikuvute kuhusu ni nani ambaye Bw Odinga anafaa kumteua kuwa mgombeaji mwenza wake huku makataa yaliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) yakikaribia.

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, Gavana wa Machakos Dkt Afred Mutua, aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth, Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Waziri wa Kilimo Peter Munya ni miongoni mwa wanaopigiwa upatu kuteuliwa katika wadhifa huo.

Wiki jana, Bw Musyoka na viongozi wa Wiper walisisitiza kuwa yeye ndiye Bw Odinga anafaa kumteua kuwa mgombeaji mwenza wake.

Nalo kundi la viongozi wanawake wakiongozwa na Gavana wa Kitui Charity Ngilu walimpigia debe Bi Karua wakadai ndiye aliyehitimu kwa nafasi hiyo.

Kulingana na taratibu iliyowekwa na IEBC wagombeaji uraia wanafaa kuwasilisha majina ya wagombeaji wenza wao kufikia Aprili 18, 2022.

Kando na suala la mgombeaji mwenza wa Bw Odinga, mkutano huo wa KICC pia umependekeza kubuniwa kwa asasi mbalimbali ndani ya muungano wa Azimio ambao sasa ni chama cha kisiasa.

Asasi hizo zinajumuisha, Bodi ya Uchaguzi, Bodi ya Kusikiliza Malalamishi kutokana na Uchaguzi, Kamati ya Kitaifa ya Nidhamu na Kamati ya Kutatua Mizozo.

Baraza Kuu la Kitaifa la Azimio (NCEC) litawasilisha majina ya watu wanaofaa kuhudumu katika asasi hizo.

Kando na Rais Kenyatta, mkutano wa Alhamisi asubuhi pia umehudhuriwa na mgombeaji urais wa muungano huo Raila Odinga, kiongozi wa Wiper Bw Musyoka, Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi, Martha Karua (Narc Kenya), Charity Ngilu (Narc) na Wafula Wamunyinyi (DAP- K).

Wengine walikuwa ni Naomi Shabaan (Mbunge wa Taveta), Sabina Chege (Mbunge wa Kike, Murang’a) na Junet mwenyewe.

  • Tags

You can share this post!

Helikopta yaibua msisimko katika kampeni za Muthama

TUSIJE TUKASAHAU: Kwa kupigia chapuo...

T L