• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
Raila ataka maendeleo sawa kote

Raila ataka maendeleo sawa kote

NA SHABAN MAKOKHA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga amewataka wafuasi wake ‘kutopigia magoti’ serikali ya Kenya Kwanza ili kupata maendeleo huku akisema kuwa Wakenya wote wanalipa ushuru.

Bw Odinga pia alimtaka Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua kupata idhini ya bunge kabla ya kuongeza ushuru.Kiongozi huyo wa Azimio alimtaka Rais kuitisha vikao vya kukusanya maoni kutoka kwa umma kabla ya kuongeza ushuru.

“Uamuzi kuhusu kuongezwa kwa ushuru unapaswa kujadiliwa na umma. Ushuru haufai kutozwa bila uwakilishi,” akasema Bw Odinga akieleza kuwa kila Mkenya anafaa kuwa na usemi katika suala hilo kuu la kuongezwa kwa ushuru.

Bw Odinga, ambaye alikuwa ameandamana na viongozi kadhaa akiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, alisema hayo Jumatatu katika hafla ya mazishi ya mama Philomena Barasa, ambaye ni mama yake Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, katika eneobunge la Mumias Mashariki, Kaunti ya Kakamega.

Viongozi hao waliapa kuhakikisha kuwa serikali ya Dkt Ruto inasambaza maendeleo katika maeneo yote ya nchi bila kuzingatia miegemeo ya kisiasa.

Mabw Odinga na Musyoka waliishinikiza Serikali ya Kenya Kwanza kutekeleza ahadi ilizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, ili kupunguza makali yanayosababishwa na kupanda kwa bei ya bidhaa za kimsingi na ukame.

Mnamo Jumamosi wiki jana, Rais Ruto alitoa wito kwa Wakenya kulipa ushuru ili kuiwezesha serikali yake kufikia kiwango cha ukusanyaji ushuru cha Sh6 trilioni kwa mwaka mnamo 2027.

Serikali, kupitia Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) imeanzisha mpango wa kutekeleza mageuzi katika mfumo wa ukusanyaji ushuru kwa kuhakikisha kuwa kila Mkenya mwenye umri wa miaka 18 kwenda juu analipa ushuru.

Dkt Ruto alisema mpango huo wa uimarishaji kiwango cha ukusanyaji ushuru, utawezesha serikali kukoma kutegemea mikopo ili kufadhili mipango na miradi yake.

Rais alisikitika kuwa ni Wakenya milioni saba pekee waliosajiliwa kwa Nambari ya Utambulisho wa Kibinafsi (PIN) ilhali idadi ya Wakenya waliojisajili kwa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu ni 30 milioni.

“Tunahitaji kulipa ushuru ili tupate pesa za kufadhili miradi ya maendeleo na pia kuweza kulipa madeni yetu kama taifa,” Dkt Ruto akasema Jumamosi katika ukumbi wa KICC, Nairobi.

Wakati huu, rekodi za KRA zinaonyesha kuwa asasi hiyo hukusanya karibu Sh1.88 trilioni kama ushuru kila mwaka. Pesa hizo ni sawa na pesa ambazo hutengwa katika bajeti ya kitaifa kila mwaka kwa ajili ya kugharimia matumizi ya Serikali ya Kitaifa.

Viongozi hao walitisha kuzua fujo iwapo Serikali ya Rais Ruto haitasambaza miradi ya maendeleo hadi katika maeneo ambayo hayakumpigia kura kwa wingi.

“Wakenya hulipa ushuru bila kuzingatia mipaka ya kisiasa na hivyo maendeleo pia yanafaa kusambazwa kwa njia hiyo hiyo. Wakenya hawafai kupiga magoti mbele ya mtu yeyote ili waweze kuhudumiwa, ni haki yake ya kidemokrasia kupata huduma hizo. Tutafanya mambo kuwa magumu kwa serikali ikiwa maendeleo yatasambazwa kwa mapendeleo.

  • Tags

You can share this post!

Kilio Seneti wahasiriwa wakisimulia masaibu yao mikononi...

Samuel Njoroge sasa ndiye Karani mpya wa Bunge la Kitaifa

T L