• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:52 PM
Raila, Uhuru kupanga ndoa yao upya wikendi

Raila, Uhuru kupanga ndoa yao upya wikendi

Na LEONARD ONYANGO

KINARA wa ODM, Raila Odinga wikendi hii atakuwa na shughuli nyingi huku muungano wa Azimio la Umoja ukianza rasmi kampeni ya kuelekea Ikulu Agosti 9.

Vyama vya Jubilee na ODM leo Ijumaa na kesho Jumamosi vinatarajiwa kuandaa vikao vya wajumbe (NDC) katika maeneo tofauti kabla ya kuandaa mkutano mkubwa Jumapili katika uwanja wa Kamkunji, Nairobi, ambapo Bw Odinga atatawazwa rasmi kuwa mwaniaji wa urais wa muungano wa Azimio la Umoja.

Rais Uhuru Kenyatta, anatarajiwa kuongoza mkutano wa zaidi ya wajumbe 4,000 wa Jubilee katika Jumba la KICC, Nairobi.

Wajumbe hao wa Jubilee wataidhinisha uamuzi wa kuunga mkono Bw Odinga chini ya mwavuli wa Azimio la Umoja.

Rais Kenyatta alipokutana na wabunge na maseneta wa Jubilee katika Ikulu ya Nairobi wiki iliyopita, alisema chama hicho tawala hakitasimamisha mwaniaji wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, na badala yake kitaunga mkono Bw Odinga.

Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka jana Alhamisi aliashiria kuwa huenda akahudhuria mkutano wa Jubilee – ishara kwamba huenda jitihada za Rais Kenyatta kumtaka kuunga mkono Bw Odinga zinaelekea kuzaa matunda.

Bw Musyoka na Bw Odinga jana Alhamisi walikutana katika mkutano wa wajumbe wa chama cha United Democratic (UDP) kinachoongozwa na aliyekuwa mbunge wa Lugari, Cyrus Jirongo.

“Sisi viongozi wa OKA (One Kenya Alliance) tuna maono sawa na muungano wa Azimio la Umoja. Sote tunaamini katika kuunganisha Wakenya. Lakini bado tunazungumza,” akasema Bw Musyoka.

Bw Jirongo ambaye ni mmoja wa viongozi wa OKA, aliidhinisha Bw Odinga kuwania urais.Kamati Kuu (NEC) ya ODM jana iliidhinisha rasmi Bw Odinga kuwa mwaniaji wa urais wa chama hicho.Wajumbe zaidi ya 3,000 wa ODM watakutana uwanjani Kasarani ambapo Bw Odinga ataidhinishwa kujiunga na Azimio la Umoja.

“Mkutano wa ODM utajumuisha magavana, manaibu gavana, wabunge, madiwani na viongozi wa chama wa matawi,” akasema Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna.

Kulingana na mwenyekiti wa ODM John Mbadi, chama hicho cha Bw Odinga kimemwalika Rais Kenyatta katika mkutano wake.

Hii itakuwa mara ya tano kwa Bw Odinga kuwania urais huku akiwa na mzigo mzito wa kuwamegea vyeo mawaziri kadhaa wa serikali ya Jubilee ambao walikosa kujiuzulu ili kumsaidia kuchapa kampeni wakiwa afisini, iwapo atashinda urais.

Bw Odinga pia anatarajiwa kuwafaa viongozi wa vyama visivyopungua 15 ambao wametangaza kuunga mkono Azimio la Umoja.

Wengi wa magavana wanaohudumu muhula wa pili kama vile Alfred Mutua (Machakos), Kivutha Kibwana (Makueni), Amason Kingi (Kilifi), Ali Roba (Mandera), Martin Wambora (Embu), Alex Tolgos (Elgeyo-Marakwet), Cornel Rasanga (Siaya), Sospeter Ojaamong (Busia), Cyprian Awiti (Homa Bay) na James Ongwae (Kisii) pia wameweka hatima yao ya kisiasa kwa Bw Odinga.

Mawaziri Peter Munya (Kilimo), Ukur Yatani (Fedha), Eugene Wamalwa (Ulinzi), Dkt Fred Matiang’i (Usalama), Joe Mucheru (Teknolojia ya Mawasiliano), Keriako Tobiko (Mazingira), Mutahi Kagwe (Afya) na James Macharia (Uchukuzi) walisitisha azma zao za kutaka kuwania ugavana na wakaamua kumuunga mkono Bw Odinga.

Kiongozi wa chama cha Party of National Unity (PNU) Bw Munya jana Alhamisi aliambia wajumbe wa chama hicho kwamba, amefanya mkataba na Rais Kenyatta ambaye atatetea masilahi yao kwa Bw Odinga.

Bw Odinga alikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria jana Alhamisi mkutano wa NDC wa PNU katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Wajumbe wa PNU walimshinikiza Bw Odinga kumteua Waziri Munya kuwa mwaniaji mwenza wake.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Bw Odinga, Ndiritu Muriithi, aliambia Taifa Leo kuwa, mkutano wa Kamkunji utakuwa uzinduzi wa muungano wa Azimio la Umoja.

“Viongozi wa vyama ambavyo vimekubali kuunga mkono muungano wa Azimio la Umoja wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa Kamkunji,” akasema Bw Muriithi.

Gavana huyo wa Laikipia, hata hivyo, hakuthibitisha ikiwa Rais Kenyatta atahudhuria mkutano huo wa Kamkunji au la.

Rais Kenyatta alipokuwa akihutubu katika Ikulu ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, alialika vyama vidogo katika eneo la Mlima Kenya kujiunga na Azimio la Umoja.

  • Tags

You can share this post!

Afueni kwao baada ya Uhuru kupiga marufuku biashara ya...

TAHARIRI: Walimu wasihujumu mitihani ya kitaifa wakitafuta...

T L