• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 3:24 PM
Raila: Washirika wa Kalonzo sasa walegeza kamba

Raila: Washirika wa Kalonzo sasa walegeza kamba

NA PIUS MAUNDU

WASHIRIKA wenye msimamo mkali wa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, sasa wamelegeza msimamo wao na kukubali amuunge kiongozi wa (ODM) Raila Odinga kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Seneta wa Kitui Enoch Wambua, mwenzake wa Makueni Mutula Kilonzo Junior na mbunge wa Makueni Daniel Maanzo, walikuwa wamesisitiza kuwa Bw Musyoka hakufaa kujiunga na Azimio la Umoja ambalo mgombea urais wake na Bw Odinga, wakisema angejimaliza kisiasa.

Wiki moja iliyopita, Bw Musyoka alikanyagia breki azma yake ya urais na kumuidhinisha Bw Odinga na washirika wake sasa wameamua kukubaliana naye.

“Kwa kuwa kiongozi wetu ameamua kuwa sehemu ya Azimio, tumekubaliana naye na tutasaidia tuwezavyo kuhakikisha kuwa Bw Odinga atakuwa rais. Hata hivyo, wanachama wa Wiper ni lazima wawe sehemu ya serikali ya Bw Odinga,” alisema Bw Kilonzo Jnr akiwa mjini Wote mnamo Jumamosi.

Seneta huyo ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa Wiper anayesimamia mikakati, aliungana na Bw Wambua na Bw Maanzo, ambao wamemtaka Bw Odinga kumteua Bw Musyoka kuwa mgombea mwenza wake kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Washirika wa Bw Musyoka wameshutumu wanachama wa kampeni ya Bw Odinga na magavana wa kaunti tatu za Ukambani kwa kusisitiza kuwa, Wiper kilijiunga na Azimio kama chama na sio mwanachama wa One Kenya Alliance, muungano unaojumuisha vyama vya KANU, Narc-Kenya, MDG, UDP na Farmers Party.

Wanachama wa Wiper, wanasema katika mpangilio wa kiti chenye miguu mitatu, Bw Musyoka atakuwa katika kiwango kimoja na Rais Uhuru Kenyatta na Odinga katika uongozi wa Azimio la Umoja.

Hii itahakikisha kuwa Bw Musyoka atachukua usukani wa kampeni za Bw Odinga eneo la Ukambani, hatua ambayo imezua uhasama mpya kati ya makamu rais huyo wa zamani na magavana Alfred Mutua (Machakos), Charity Ngilu (Kitui) na Kivutha Kibwana (Makueni), ambao vyama vyao vinaunga azma ya urais ya Bw Odinga.

Magavana hao walio viongozi wa vyama vyao vya kisiasa wanahisi kwamba vyama vyote vinafaa kuruhusiwa kushindana katika eneo hilo.

“Hatuna cha kuambia jamii na watu wanaounga Wiper. Lazima kuna kitu ambacho Bw Musyoka anataka kwa kuacha azma yake ya kugombea urais kwa mara ya tatu. Tulipopendekeza Kalonzo Musyoka mwaka wa 2007 kuwa makamu rais, sisi wote, akiwemo marehemu baba yangu, tulifahamu wazi kuwa tungetwaa wadhifa wa naibu rais. Huo ndio msimamo wa Wiper,” Bw Kilonzo alisema.

Wito wa washirika wa Bw Kalonzo unajiri ikisemekana kwamba Bw Odinga anafaa kuteua mgombea mwenza kutoka eneo la Mlima Kenya.

Muungano wa Kenya Kwanza Alliance ambao mgombea urais wake ni Naibu Rais William Ruto, pia umeonekana kuhimizwa kusaka mgombea mwenza mlimani.

You can share this post!

Tammy Abraham aweka rekodi ya ufungaji mabao Serie A

Muhatia atawazwa kama Askofu Mkuu mpya wa Kisumu

T L