• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Rais aamua kurudisha mkono kwa Jaramogi

Rais aamua kurudisha mkono kwa Jaramogi

NA CHARLES WASONGA

KATIKA kile kinachoonekana kuwa marudio ya historia, Rais Uhuru Kenyatta ameamua kulipa wema ambao babake, Mzee Jomo Kenyatta, alitendewa na babake kiongozi wa ODM Raila Odinga, marehemu Jaramogi Oginga Odinga, miaka ya 1960s.

Amefanya hivyo kwa kumwidhinisha Raila kuwa mrithi wake katika Ikulu mwaka huu, miaka 59 baada ya Jaramogi kumpisha babake (Jomo) kuwa Rais wa kwanza wa taifa hili mnamo Desemba 1964.

Awali, mnamo 1963, Jaramogi alimtendea Jomo hisani kubwa zaidi alipokataa ombi la wakoloni waliomtaka kutwaa uongozi wa Kenya wakati Mzee alikuwa gerezani Kapenguria.

Jaramogi alikataa pendekezo hilo na kushinikiza Jomo aachiliwe huru kwanza ili awaongoze kuunda serikali ya kwanza ya Mwafrika Kenya.

Katika kitabu chake, “In Kenya: A History Since Independence,” mwanahistoria Charles Hornsby anaandiki hivi: “Ni mtu mmoja tu, Jaramogi aliyesisitiza kuwa sharti Kenyatta aachiliwe huru ili aongoze Kenya kupata uhuru. Alifanya hivyo wakati viongozi wa Kiafrika nyakati hizo walimchukia Kenyatta na hawakutaka atoke jela.”

Hatimaye Mzee Kenyatta aliachiliwa huru na kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu kabla ya kutawazwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya mnamo Desemba 12, 1964. Marehemu Jaramogi alihudumu kama makamu wa rais wa kwanza katika serikali hiyo ya kwanza ya Mwafrika; kuanzia mwaka huo hadi 1966 alipojiuzulu.

Wadadisi wanasema historia inaelekea kujirudia katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, ambapo licha ya kustaafu, Rais Kenyatta anapania kuunda serikali ijayo na Bw Odinga, jinsi wazazi wao walivyofanya.

“Ni kweli kwamba, endapo Raila atashinda katika uchaguzi mkuu ujao, yeye na Uhuru ndio wataunda serikali ijayo. Tayari duru zinasema chama cha Jubilee ambacho Uhuru atasalia kuwa kiongozi wake ndicho kitatoa mwaniaji mwenza wa Raila ambaye atachukua wadhifa wa Naibu Rais muungano wa Azimio la Umoja ukishinda,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Barack Muluka.

“Ikiwa hilo litatendeka, bila shaka uongozi wa Kenya utarejea mikononi mwa familia za Kenyatta na Odinga ili kuendeleza falsafa ya ufalme wa familia hizi mbili,” anaongeza msomi huyo ambaye aliwahi kuhudumu kama Katibu Mkuu wa chama cha Amani National Congress (ANC).

Mnamo Februari 26 mwaka huu, Rais Kenyatta alihudhuria kongamano la wajumbe wa ODM (NDC) ambapo alimiminia sifa Raila akimtaja kama kiongozi shupavu, mpatanishi na mshauri mkuu.

“Niko hapa sio kwa sababu Raila Amollo Odinga ni mwanasiasa. Mwanasiasa ni yule ambaye nimeshindana naye kwa miaka mingi. Niko hapa kwa sababu Raila Odinga ni kiongozi. Raila na mpatanishi na mleta amani. Nataka kuwaambia Wakenya kwamba Raila ni mpenda amani.

Kwa upande mwingine sawa na baba zao, Rais Kenyatta na Bw Odinga wamewahi kugongana kisiasa miaka ya nyuma. Uhasama huo ulichipuza kwa mara ya kwanza 2002 Rais wa zamani Daniel Moi alipompendekeza Uhuru kuwa mrithi wake katika Ikulu.

Bw Odinga aliongoza uasi ndani ya Kanu na pamoja na viongozi wengine wakashirikiana na mrengo wa upinzani ulioongozwa na Mwai Kibaki kuunda muungano Narc.

Odinga alimpendekeza Kibaki kuwa mgombea urais katika uchaguzi huo ndipo akambwaga Uhuru katika uchaguzi wa mwaka huo na kusitisha miaka 40 ya utawala wa Kanu.

Kwa mara nyingine, Bw Odinga na Rais Kenyatta walikuwa katika mirengo kinzani katika uchaguzi mkuu wa 2013 na ule wa 2017 waliposhindana katika kinyang’anyiro cha urais.

Rais Kenyatta amewahi kutumia maafisa wa usalama kupambana na Bw Odinga pamoja na wafuasi wake katika kipindi hicho.

Taswira sawa na hiyo ilishuhudiwa kuanzia Machi 13, 1966, Jaramogi alipovuliwa wadhifa wa makamu wa rais wa chama cha Kanu na kufurushwa kutoka chama hicho. Hatua hiyo ilichukuliwa katika kongamano la wajumbe wa chama hicho Limuru ambapo wafuasi wa Mzee Kenyatta waliamua kubuni nafasi nane za manaibu rais ili kudhoofisha ushawishi wa Jaramogi.

Baadaye mnamo Aprili 14, 1966 Jaramogi aliamua kujiuzulu wadhifa wake kama makamu rais, Kisha akaongozwa wabunge 30 wandani wake kuondoka Kanu na kubuni chama cha Kenya Peoples’ Union (KPU).

Mnamo Novemba 1969, wafuasi wa Jaramogi walizua fujo Mzee Kenyatta alipozuru Kisumu kufungua rasmi Hospitali ya Kuu ya Nyanza Maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi wakajeruhiwa katika makabiliano kati ya raia na polisi.

  • Tags

You can share this post!

Kang’ata asema chama cha Jubilee ni meli iliyozama

Kisanga AP akiacha kulinda mtihani na kukimbilia chang’aa

T L