• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Kang’ata asema chama cha Jubilee ni meli iliyozama

Kang’ata asema chama cha Jubilee ni meli iliyozama

NA GATUNI WACHIRA 

SENETA wa Kaunti ya Murang’a Bw Irungu Kang’ata amesema kwamba chama cha Jubilee kinaweza kufananishwa na meli kubwa ambayo inaelekea kuzama baada ya kushindwa kuchuana na mawimbi makali ya bahari ya siasa.

Bw Kang’ata ambaye amekuwa akisakata siasa zake bila kuficha, alisema kwamba chama hicho chafaa kutupiliwa mbali na nafasi yake kutwaliwa na chama kingine chenye nafasi ya wananchi.

“Mimi naona kwamba chama hiki cha Jubilee kimekosa makali,na kinafanana na meli kubwa inayojaribu kuchuana na mawimbi makali ya bahari,lakini haiwezi,inashindwa kabisa. Binafsi naona wakitupilie mbali chama hicho kwa sababu hakina usemi popote,” alisema seneta huyo wakati wa mkutano wa chama cha UDA.

Katika kutetea tetesi zake kwamba chama hicho hakina usemi tena, Bw Kang’ata alisema kwamba Jubilee  kimeendelea kupoteza wanachama ambao ndio nguzo muhimu katika kuendesha shughuli zake.

Kulingana na Bw Kang’ata , wanachama kama vile Gavana wa Kiambu wa zamani Bw Ferdinand Waititu, Bi Ann Waiguru, Mbunge wa Gatundu Kusini Bw Moses Kuria, Gavana wa zamani wa Kiambu Bw William Kabogo na Spika wa Seneti Bw Ken Lusaka ni wanachama watajika ambao walikitelekeza chama hicho.

“Hawa viongozi wanaendelea kupoteza chama. Meli hii ya Jubilee  inazama jamani. Watu waliokuwa na usemi kwa Jubilee tayari wameruka nje. Wameona meli inazama,” alisema Bw Kang’ata.

 Akirejelea takwimu za chaguzi ndogo zilizoandaliwa hivi majuzi, Bw Kang’ata alisema kwamba chama hicho kilipoteza nafasi nzuri za ushindi katika chaguzi ndogo za  ngome zake kama vile Juja, Rurii na Gaturi.

“Wakubali tu kwamba chama kilishindwa huko Gaturi, Rurii na Juja na chama cha UDA.  Na mimi niliamua kutoficha siri tena, nikaona nimwandikie Rais Uhuru Kenyatta kuhusu hali ya chama, na nikamwambia ukweli. Wenyewe mliona,s iku chache baada ya barua yangu, mpango mzima wa BBI uligonga mwamba,” alisema Bw Kang’ata.

Alisema kwamba ishara kwamba mambo si mazuri katika chama hicho ni  dalili zinazojitokeza kwa wanaowania nyadhifa mbalimbali ambao kulingana naye, hakuna hata mmoja anayewania kiti cha ugavana katika Kaunti ya Murang’a kwa kutumia chama hicho.

“Hata Katibu mmoja wa Kudumu aliyejiuzulu kuwania wadhifa fulani, Bw Kanini Keega alipojaribu kumvisha kofia ya chama hicho, alikataa,” aliongeza seneta huyo.

Wadhifa wa ugavana kwa sasa umeshikiliwa na Gavana Mwangi Wa Iria, ambaye ametangaza azma yake ya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta mwakani, baada ya kumaliza awamu zake mbili za uongozi . Wa Iria atawania urais kwa kutumia Chama chake cha Civic Renewal Party (CRP) kinachofahamika kama Usawa Kwa Wote.

Mfafanuzi wa masuala ya kisiasa Prof Peter Kagwanja amesema kwamba atakayechaguliwa kuwa gavana lazima awe na rekodi nzuri ya maendeleo bila kusahau usemi wa Rais Uhuru Kenyatta katika siasa za Mlima Kenya.

“Kwa sasa hali ni telezi huku Mlima Kenya  na hauwezi kuchora taswira halisi ya mambo kwa sasa,” alisema Prof Kagwanja ambaye pia ametangaza azma yake kuwania useneta katika Kaunti ya Murang’a.

  • Tags

You can share this post!

FARHIYA HUSSEIN: Pengo waliloacha Ngala, Nassir na Maitha...

Rais aamua kurudisha mkono kwa Jaramogi

T L