• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 11:30 AM
Ruto aahidi kuiweka Kenya katika viwango vya juu kiuchumi

Ruto aahidi kuiweka Kenya katika viwango vya juu kiuchumi

NA LAWRENCE ONGARO

NAIBU Rais Dkt William Ruto amezuru mjini Thika Jumatano ili kuwarai wapigakura wamchague ifikapo Jumanne, Agosti 9 wiki ijayo.

Dkt Ruto amesema ana imani ya kwamba ataibuka mshindi katika uchaguzi mkuu ujao.

Amesema serikali yake itatenga Sh50 bilioni ili kusimamia biashara za watu wa chini.

“Serikali yetu itafanya juhudi kuona ya kwamba vijana 5 milioni wanapata ajira na pia watatafutiwa mipango ya kujikimu kimaisha,” akaahidi Dkt Ruto.

Ameshambulia kampuni za kura za maoni kama Ipsos, na Tifa kwa kudai kuwa wapinzani wao wa Azimio wanaongoza kwa kura ya maoni.

“Sisi tuna imani na wananchi tukijua ya kwamba watatupigia kura ifikapo Agosti 9, 2022. Kwa hivyo kura ya maoni haitutishi,” alijitetea naibu wa rais.

Amesema lengo lao kuu ni kuona ya kwamba wanabadilisha maisha ya mwananchi wa chini na hasa vijana ili wajiepushe na dawa za kulevya.

Wakazi wa Thika wajitokeza kuhudhuria mkutano wa kisiasa wa mgombea urais wa UDA ndani ya muungano wa Kenya Kwanza Dkt William Ruto. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Amesema serikali yake itafanya juhudi kuona ya kwamba inazindua Bima ya Afya kwa kila mwananchi ili matibabu yawe nafuu.

Amewaeleza wakazi wa Thika jinsi katika awamu ya kwanza ya uongozi wa Jubilee, walivyofanikiwa kuleta maendeleo mengi.

Hapo akataja barabara za kilomita 11,000, reli kilomita 700, na kwamba watu 11 milioni walipata umeme katika makazi yao.

Amedai wapinzani wao wa Azimio hawana ajenda yoyote ya kuwasaidia Wakenya.

“Wapinzani wetu hawana ajenda yoyote ya kuwasaidia wakenya na kwa hivyo ni vyema kuwachagua viongozi wenye maono kama sisi wa Kenya Kwanza,” amesema.

Amesisitiza kwamba chama cha UDA kina mipango mikubwa ya kubadilisha uchumi wa nchi na kwa hivyo wapigakura wawe makini watakapofanya uamuzi wao wakati wa uchaguzi.

Wakati wa ziara hiyo Ruto aliandamana na naibu wake Rigathi Gachagua, mwaniaji kiti cha ubunge mjini Thika Bi Alice Ng’ang’a, Moses Kuria, mwaniaji wa useneta kaunti ya Kiambu Karungo wa Thang’wa, mwaniaji waq kiti cha Mwakilishi wa Kike Anne Muratha, mwanijai ugavana Kiambu Bw Kimani Wamatangi, na viongozi wengine mashuhuri.

Naibu wa rais aliwarai wakazi wa Thika kwa heshima yao wapige kura kwa chama cha UDA kutokea kiti cha urais hadi kile cha MCA.

Wakazi wa Thika walikuwa na msisimko wakati viongozi wengine walichukua nafasi ya kuwahutubia huku wakiahidiwa mazuri iwapo serikali ya UDA itachukua usukani.

  • Tags

You can share this post!

Raila apata uungwaji kutoka kwa Wakenya wanaoishi Uingereza

Serikali haitafunga mawasiliano ya intaneti – Mucheru

T L