• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 7:55 PM
Raila apata uungwaji kutoka kwa Wakenya wanaoishi Uingereza

Raila apata uungwaji kutoka kwa Wakenya wanaoishi Uingereza

NA CHARLES WASONGA

SAFARI ya mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga kuingia ikulu imepigwa jeki baada ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa Wakenya wanaoishi Uingereza.

Wakiongozwa na mshirikishi wa vuguvugu kwa jina, Rao Diaspora, Ali Ali na katibu mkuu Rose Seko, kundi hilo lilisema limepanga makundi mengine kote ulimwenguni yanayolenga kuunga mkono ndoto ya Bw Odinga.

“Matunda ya juhudi zetu yataonekana mnamo Agosti 9. Tuko na makundi kadha ya kuendesha kampeni za Bw Odinga hapa Uingereza na mataifa mengine duniani, ikiwemo Kenya,” akasema Ali.

Ali na wenzake walimtaja Bw Odinga kama kiongozi mwanamapinduzi na mchapakazi ambaye ndiye anayefaa kuiongoza Kenya baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu.

Miongoni mwa mipango ya kundi hilo ya kuvumisha ndoto ya urais ya Bw Odinga inajumuisha mkutano wa kupitia mitandaoni.

Mpango mwingine ni misafara kwa jina Diaspora Caravan katika eneo la Mlima Kenya ambayo imekuwa ikinadi jumbe za Azimio La Umoja-One Kenya.

“Tuko na makundi katika maeneo ya Mlima Kenya, Rift Valley na Magharibi mwa Kenya yanayoendesha kampeni za nyumba hadi nyumba kuhakikisha kuwa Raila na Martha Karua wanashinda uchaguzi,” Bw Ali akaongeza.

Aliwaonya Wakenya dhidi ya kumchagua Naibu Rais William Ruto na kundi lake la Kenya Kwanza, akiwataja kama wafisadi na ambao hawawezi kuaminika.

“Hawa ni viongozi wafisadi ambao hawawezi kuaminiwa kwa kutunukiwa nyadhifa za uongozi. Huwezi ukachagua mtu mfisadi kupambana na ufisadi. Raila na Karua ni wanasiasa safi kwa hivyo wanaweza kuaminiwa kupambana na jinamizi hili,” akasema mshirikishi huyo wa Rao Campaign.

Ujumbe sawa na huo ulitolewa na Seko ambaye alisema kuwa kuna hatari ya uchumi wa Kenya kuporomoka endapo utasimamiwa na viongozi wafisadi.

“Sharti tumpigie kura Raila na Karua ili tuwanyime wezi mamlaka ya kusimamia serikali. Tusipofanya hivyo, tutaumia kama taifa. Kenya iko salama mikononi mwa Baba na Martha,” akasema Seko.

Kundi hilo lilimsifu Rais Uhuru Kenyatta kwa kumuunga mkono Bw Odinga, likitaja hatua hiyo kama itakayoleta manufaa makubwa kwa Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Aliyekuwa Rais wa Botswana ajiondoa ghafla kama mwenyekiti...

Ruto aahidi kuiweka Kenya katika viwango vya juu kiuchumi

T L