• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 2:49 PM
Ruto abomoa kwa jirani nyufa zikitokea kwake nyumbani

Ruto abomoa kwa jirani nyufa zikitokea kwake nyumbani

NA WANDERI KAMAU

WAKATI Rais William Ruto anapambana kuwarushia chambo maseneta na wabunge waliochaguliwa na chama cha Orange Democratic Movement (ODM), nyufa zinaanza kujitokeza katika muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Mnamo Septemba 13, 2023, Seneta wa Kisumu Profesa Tom Ojienda na wabunge waliochukuliwa hatua za kinidhamu na chama cha Orange Democratic Movement (ODM) walihudhuria kikao kilichoongozwa na Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Prof Ojienda na wabunge Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Phelix Odiwuor (Lang’ata), Mark Nyamita (Uriri), Caroli Omondi (Suba Kusini) na Paul Abuor (Rongo) ambao wanachukuliwa kuwa waasi, walichukua hatua hiyo wiki moja baada ya ODM inayoongozwa na Raila Odinga kuwaadhibu.

Seneta wa Kisumu pamoja na wabunge wanne isipokuwa Bw Nyamita na Bw Abuor, walitimuliwa chamani ODM. Hata hivyo, mnamo Jumanne wiki jana, Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDT) ilipiga ODM breki kali.

Taarifa kutoka kwa kikao hicho cha Ikulu ilisema waliangazia masuala manne makuu.

“Kwanza kwa niaba ya wakazi wa Nyanza tunaishukuru serikali kwa kuchukua hatua madhubuti kufufua sekta ya sukari. Tutaunga mkono mswada wa sukari utakaowasilishwa bungeni kesho Alhamisi,” ikasema sehemu ya taarifa hiyo.

Pia walijadili suala la kuanza kwa safari za ndege hadi Migori na wakamualika Rais kutembelea eneo la Luo Nyanza kwa ziara ya kikazi.

Mwisho walisisitiza wataendelea kuiunga mkono serikali kwa ajili ya ufanikishaji wa maendeleo katika maeneo yao ya uwakilishi na kote nchini.

Merikebu

Lakini sasa mrengo tawala wa Kenya Kwanza unakabiliwa na ubabe baina ya viongozi wake tofauti, hali inayotishia kuzamisha merikebu ya Rais Ruto, hivyo kumzuia kutimiza baadhi ya ahadi alizotoa kwa Wakenya.

Licha ya Rais Ruto kuusawiri mrengo huo kama wenye mshikamano mkubwa, kinaya ni kuwa mizozo hiyo baridi ya kisiasa inawahusisha washirika wake wa karibu.

Mizozo hiyo inawahusisha Naibu Rais Rigathi Gachagua na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala dhidi ya Seneta Boni Khalwale (Kakamega), Bw Gachagua na mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Gavana Irungu Kang’ata wa Murang’a dhidi ya Waziri wa Maji Alice Wahome na Bw Mudavadi dhidi ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.

Kulingana na wadadisi wa siasa, mvutano baridi wa kimamlaka baina ya Bw Gachagua na Bw Mudavadi, ulianza mara tu baada ya Rais Ruto kumteua Bw Mudavadi kama kinara wa mawaziri.

Mvutano huo ulionekana kupanuka zaidi, baada ya Rais Ruto kumkabidhi Bw Mudavadi majukumu makubwa ya kitaifa, yaliyoonekana kuzidi yale ya Bw Gachagua.

Kwenye mpangilio wa serikali yake aliotangaza Januari, Rais Ruto alimpa Bw Gachagua jukumu la kuendesha mageuzi katika sekta ya kilimo, huku Bw Mudavadu akipewa jukumu la kusimamia utendakazi wa wizara mbalimbali.

Kando na hilo, Bw Mudavadi amekuwa akifanya ziara nyingi za nje, hali iliyoibua hofu kwamba Bw Mudavadi alionekana kumzidi kimamlaka Bw Gachagua.

Ni hali iliyomfanya Bw Mudavadi kujitokeza wazi na kutangaza kwamba hakuwa kwenye ushindani wowote wa kisiasa na Bw Gachagua.

“Sina ushindani wa kisiasa na yeyote. Ziara za nje ambazo nimekuwa nikifanya huwa ninatumwa na Rais. Lengo jingine la ziara hizo ni kupanua juhudi zetu za kidiplomasia duniani,” akasema Bw Mudavadi.

Katika Kaunti ya Kakamega, mvutano baina ya Bw Malala na Dkt Khalwale uliendelea kudhihirika hapo Ijumaa.

Hili ni baada ya Dkt Khalwale kuwaongoza baadhi ya wanachama wa UDA kutishia kutomtambua Bw Malala kama Katibu Mkuu wa UDA.

Wanachama hao walisema kuwa Bw Malala bado ni mwanachama wa Amani National Congress (ANC).

Walisema kuwa yeyote anayehama kutoka vyama vya Ford-Kenya, ANC, DP au PAA, ambavyo bado ni wanachama wa mrengo wa Kenya Kwanza, na kujiunga na UDA, hatakubaliwa kuchukua nafasi za uongozi katika chama hicho.

Dkt Khalwale alisema kuwa lengo kuu la wanachama hao, waliokutana katika eneo la Malinya, Ikolomani, linalenga kuweka taratibu zitakazowiana na mikakati ya kuimarisha mwonekano wa chama hicho nchini, kinapojitayarisha kwa chaguzi za mashinani zilizopangiwa kufanyika Desemba.

“Tunataka UDA kuwa chama cha mabadiliko. Hatuwezi kufikia hili ikiwa tutaruhusu watu kuhama kutoka vyama vyao asubuhi na kuwa viongozi wa chama chetu nyakati za jioni,” akasema.

Katika ukanda wa Mlima Kenya, vita baridi baina ya Bw Gachagua na Bw Nyoro vilianza Februari, baada ya baadhi ya viongozi kumpendekeza Bw Nyoro kuwa kiongozi na msemaji wa kisiasa wa ukanda wa Mlima Kenya.

Kama Naibu Rais, Bw Gachagua amekuwa akiendeleza juhudi za kujijenga kama mrithi wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, ijapokuwa mikakati yake imekuwa ikikumbwa na upinzani wa kichinichini kutoka kwa Bw Nyoro.

Baadhi ya wanasiasa waliompendekeza Bw Nyoro kuwa kiongozi wa kisiasa Mlimani ni Seneta Samson Cherargei (Nandi), mbunge Didmus Barasa (Kimilili), John Kiarie ‘KJ’ (Dagoretti), Cynthia Muge (Nandi), Njeri Maina (Kirinyaga), Seneta Joe Nyutu (Murang’a) kati ya wengine.

Bw Nyutu alizua msisimko, aliposema kuwa wakati umefika kwa Kaunti ya Murang’a kumtoa Rais.

“Ni zamu ya Kaunti ya Murang’a kumtoa Rais. Rais wa kwanza na wa nne walitoka katika Kaunti ya Kiambu, huku wa tatu akitoka katika Kaunti ya Nyeri. Nafasi ya Unaibu Rais pia imeenda Nyeri. Ni zamu yetu kupewa nafasi ya urais kupitia Bw Nyoro,” akasema.

Tangu wakati huo, viongozi hao huwa hawahudhurii hafla moja, na huwa wanafanya hivyo tu wanapoandamana na Rais Ruto.

Duru zinasema kuwa kumeibuka mvutano wa kichinichini baina ya Dkt Kang’ata na Bi Wahome, ikiibuka kuwa waziri huyo anajitayarisha kuwania ugavana 2027.

Katika eneo la Magharibi, duru zinaeleza kumeibuka vita baridi kati ya Mabwana Mudavadi na Wetang’ula, hilo likitajwa kuchangiwa na udhibiti wa siasa za ukanda huo, hasa baada ya kuibuka kuwa huenda Rais Ruto akamuunga mtu kutoka ukanda huo kuwa mrithi wake 2032.

Wadadisi wanasema ijapokuwa wawili hao huonyesha bado wako pamoja kisiasa, kuna uwezekano wa vita baridi baina yao kuibuka.

“Ilivyo sasa, lazima tangazo la Rais Ruto lizue ushindani wa kisiasa baina ya vigogo hao wawili, kwani kila mmoja anapania kuwa kiongozi na msemaji wa jamii ya Mulembe,” asema mdadisi wa siasa Martin Andati.

Wadadisi wanasema ni lazima Rais Ruto azime makabiliano hayo, la sivyo huenda yakaipaka tope serikali yake, hivyo kushindwa kutimiza baadhi ya ahadi alizotoa.

  • Tags

You can share this post!

Waajiri wakataa mswada wa wafanyakazi kutojibu simu

PENZI LA KIJANJA: Tahadhari mapenzi ya mtandaoni...

T L