• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
PENZI LA KIJANJA: Tahadhari mapenzi ya mtandaoni yasikuletee majuto

PENZI LA KIJANJA: Tahadhari mapenzi ya mtandaoni yasikuletee majuto

NA BENSON MATHEKA

MAPENZI ya mtandaoni yamechacha siku hizi.

Watu wanatafuta wapenzi wa kuwaondolea upweke kwenye mitandao ya kijamii wakivutiwa na picha za warembo, mabarobaro, mashugamami na masponsa, zinazoambatanishwa na mistari mitamu na ahadi za kutoa nyoka pangoni.

Kuna wanaotangaza kuwa wanataka warembo na wanaume wa kuanzisha uhusiano wa kudumu na kuongeza kuwa watakaoangukia hawatakosa chochote. Na hii imefanya wengi kuchangamkia mapenzi ya mtandaoni kiasi cha kusahau kuna wanaume karibu nao wanaowamezea mate. Wasichofahamu ni kuwa mapenzi ya mtandaoni sio mapenzi halisi.

Kumejaa utapeli na ulanguzi wa mapenzi ambao umefanya wengi kujuta.

Hivyo basi, usitekwe moyo na akili na simulizi za watu wanaodai waliangukia masonko kuruka kwenye Face book au mitandao mingine ya kijamii. Hii ni mistari ya kukuvutia ujibwage katika bahari usiojua kina chake. Ahadi hizi na mistari mitamu ni vifumba macho.

Kwa hakika, wengi wanaotoa ahadi hizi wanasaka watu wa kuwalisha uroda tu. Sio ndoa.

“Mapenzi ya mtandaoni yanaweza kuwa hadaa, kabla ya kuyachangamkia, fikiria mara mbili,” ashauri Purity Mwongeli, mwanasaikolojia na mshauri wa masuala ya mahusiano.

Anasema watu wengi wamekuwa wakivutiwa na maneno matamu ya wapenzi wanaokutana nao katika mitandao ya kijamii na tovuti za kuunganisha wapenzi wanaowaahidi ardhi na mbingu.

“Inashangaza wanaotafuta wapenzi katika tovuti hizi wameongezeka licha ya hadaa zinazohusishwa nayo. Tovuti hizi zinapotosha wanaowinda wapenzi mtandaoni. Wengi wamejipata wakishirikishwa katika utumwa wa ngono wakifuata maisha ya anasa wanayoaihidiwa na wapenzi wanaokutana nao mtandaoni,” asema.

Ingawa mtandao umerahisisha mawasiliano na umefaulu kukutanisha wapenzi, wataalamu wanashauri watu kuwa waangalifu.

“Awali ni wanawake waliolengwa zaidi na matapeli wa mapenzi mitandaoni lakini siku hizi, wanaume wanalengwa na wanawake au wahalifu wanaojifanya wanawake wenye pesa,” asema Mwongeli.

Anasema watu wanaoshiriki ufuska mtandaoni wanajiweka katika hatari kubwa.

“Watu waache kupagawa kimapenzi na watu wasiowajua katika mitandao na waache kushiriki mazungumzo ya ufuska kwa sababu wanajiweka katika hatari ya kuanguka mikononi mwa walaghai,” asema Mwongeli na kuongeza kuwa kuna wanaovunja uchumba wao wakinyemelea wapenzi wa mtandaoni.

Mwongeli anashauri watu kutumia mtandao kwa masuala ya kujijenga kimaisha badala ya kuutumia kushiriki ufuska.

“Watu wanafaa kutumia mtandao kwa manufaa yao na sio kusaka wapenzi wanaowatumbukiza katika majuto,” asema

  • Tags

You can share this post!

Ruto abomoa kwa jirani nyufa zikitokea kwake nyumbani

Muheria asema bei za mafuta zinalemea masikini  

T L