• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 2:31 PM
Ruto adai baadhi ya viongozi wa Azimio wanamuunga mkono kisiri

Ruto adai baadhi ya viongozi wa Azimio wanamuunga mkono kisiri

NA JACOB WALTER

NAIBU Rais William Ruto anadai kuwa baadhi ya viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya wanamuunga mkono faraghani.

“Kuna viongozi wa Azimio wanaonipigia simu usiku. Wananihakikishia kuwa wananiunga mkono lakini wanahofia hatima yao kisiasa. Usiku wananiunga mkono huku mchana wakimuunga mkono Raila,” akasema Dkt Ruto.

Akijipigia debe eneo la Moyale, Kaunti ya Marsabit, Dkt Ruto alidai kuwa kuna wafuasi wake waliojiunga na muungano wa Azimio baada ya kutishiwa na serikali.

“Wafuasi wangu wanaokumbwa na kesi za ufisadi walijiunga na muungano wa Azimio baada ya kutishiwa,” akasema Dkt Ruto.

Aliahidi kuwa serikali yake itainua sekta ya ufugaji katika Kaunti ya Marsabit.

Aliwarai wakazi wa Marsabit kutompigia kura Bw Odinga akidai serikali ya kiongozi huyo wa ODM itafanya kaunti hiyo kupoteza ufadhili wa maeneo kame.

Kuhusu ufichuzi kuwa kampuni ya Ugiriki iliyopewa kandarasi ya kuchapisha karatasi za kura ina uhusiano na Seneta Moses Wetangula wa Bungoma, Dkt Ruto aliyapuzilia mbali akisema hiyo ni ishara ya Azimio kuhisi kushindwa.

“Wanahisi kushindwa ndiposa wameanza propaganda. Sisi hatujali nani anachapisha karatasi za kura kwani tuko tayari kwa uchaguzi na tunajua tutashinda,” akasema Dkt Ruto.

Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale naye alidai Azimio wanaingilia Tume ya Uchaguzi na Mipaka kwa kuhofia kushindwa.

  • Tags

You can share this post!

Okutoyi aingia robo-fainali ya Wimbledon wachezaji wawili...

Azma ya Nyamweya yapata pigo baada ya mwenza wake kutoroka

T L