• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 4:39 PM
Ruto akaribia kumpokonya Uhuru chama cha Jubilee

Ruto akaribia kumpokonya Uhuru chama cha Jubilee

NA ONYANGO K’ONYANGO

MATUMAINI ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuendelea kudhibiti Jubilee yanadidimia baada ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu kuonekana kuidhinisha mapinduzi ya viongozi wa chama hicho.

Jana Jumanne, Bi Nderitu alisema kuwa mkutano wa Baraza Kuu la Jubilee (NEC) uliofanyika Ijumaa iliyopita na kuidhinisha kusimamishwa kwa Katibu Mkuu Jeremiah Kioni na Naibu Mwenyekiti David Murathe, ulikuwa halali.

Bw Kenyatta anatarajiwa kustaafu kutoka katika siasa kufikia Machi 13, 2023, hatua ambayo huenda ikatoa mwanya kwa Rais William Ruto kunyakua chama cha Jubilee bila pingamizi.

Rais Ruto ni miongoni mwa viongozi wakuu waliounda chama cha Jubilee mnamo 2016 lakini alilazimika kuhama alipotofautiana na Rais Kenyatta wakati huo baada ya uchaguzi wa 2017.

Kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Marupurupu ya Marais Wastaafu, kinahitaji rais mstaafu aliyekamilisha muda wake aache kujihusisha na siasa miezi sita baada ya kuondoka ikulu. Bunge la Kitaifa linaweza kupitisha hoja ya kumnyima marupurupu rais mstaafu anayeendelea kushiriki siasa baada ya miezi sita kukamilika.

Hoja hiyo ni sharti ipitishwe na theluthi tatu ya wabunge wa Bunge la Kitaifa.

Katika kikao cha Ijumaa, kundi la viongozi wanaochukuliwa kuwa waasi pia lilisimamisha kazi mwekahazina wa Jubilee Kagwe Gichohi.

Mkutano huo wa kisiri uliandaliwa siku chache baada ya Rais Ruto pamoja na naibu wake Rigathi Gachagua kukutana na wabunge 30 wa Jubilee Ikulu.

Bw Kenyatta alipuuzilia mbali mapinduzi hayo huku akisema kuwa katiba ya Jubilee imempa mamlaka kiongozi wa chama au katibu mkuu kuandaa mkutano.

Lakini Bi Nderitu, jana alisema kuwa mkutano huo uliandaliwa kwa kuzingatia katiba ya chama cha Jubilee.

Wandani wa Rais Ruto wakiongozwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei, jana walionekana kusherekea uamuzi huo wa Bi Nderitu.

Uamuzi huo wa Bi Nderitu unaamanisha kwamba viongozi walioteuliwa kujaza kwa muda nafasi za Mabw Kioni, Murathe na Gichohi, sasa watachukua rasmi.

“Tulipokea barua yenu ya Februari 13 kuhusu mkutano wa NEC uliofanyika Februari 10. Tumepokea maafikiano ya NEC na viongozi waliohudhuria. Baada ya kuchunguza kwa makini stakabadhi zilizowasilishwa, tumebaini kuwa mkutano huo ulikuwa halali na uliandaliwa kwa njia ifaayo,” akasema Bi Nderitu kupitia barua aliyoandikia Naibu Katibu Mkuu Joshua Kutuny.

Katika mkutano wa Ijumaa uliofanyika jijini Nakuru, mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) Kanini Kega, mbunge wa Eldas Adan Keynan na mwenzake wa Kitui Kusini Rachel Nyamai waliteuliwa kushikilia kwa muda nyadhifa za Katibu Mkuu, Naibu Mwenyekiti na Mwekahazina mtawalia.

Mbunge wa Bahati Irene Njoki, Mbunge Maalumu Sabina Chege, na Seneta Maalumu Margaret Kamar na mwakilishi wa Kike wa Nyamira Jerusha Momanyi waliteuliwa kuwa wajumbe wa NEC.

Bi Nderitu, hata hivyo, viongozi hao wa Jubilee kuhakikisha kuwa wanafuata utaratibu uliowekwa kusuluhisha mizozo ndani ya chama.

Rais Kenyatta na wandani wake sasa wanaweza kukimbia mahakamani kuzima juhudi za Kenya Kwanza kutaka kumeza chama cha Jubilee.

  • Tags

You can share this post!

NTSA yatayarisha sheria ya kudhibiti sekta ya bodaboda

Macharia ajitetea kuhusu uhaba wa walimu katika JSS

T L