• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Ruto akome kuwashika mateka magavana wa Azimio – Raila

Ruto akome kuwashika mateka magavana wa Azimio – Raila

NA WACHIRA MWANGI

KINARA wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga amedai kwamba Rais William Ruto anawatolea vitisho na kuwahangaisha magava wa mrengo wa Azimio, hali inayowanyima mazingira tulivu ya kutekeleza kazi zao.

Bw Odinga amesema serikali imeteka baadhi ya majukumu ya magavana kinyume na katiba hali ambayo imewafanya magavana wake kushindwa kutekeleza kazi zao inavyopaswa.

Akizungumza baada ya kukutana na takriban magavana 17 jijini Mombasa, Bw Raila amemtaka Rais Ruto kuacha kuingilia kazi za magavana akimtaka kutoa fedha kwa wakati.

Kiongozi huyo wa upinzani amesema kuwa kazi ya serikali kuu ni kutoa fedha na si kuwalazimisha magavana kuunga mkono serikali.

“Magavana wanapaswa kupewa uhuru wa kusimamia masuala na utekelezaji wa majukumu katika kaunti zao. Jukumu la serikali ya kitaifa ni kuwafadhili kulingana na sheria na sio kulazimisha magavana kufanya hivi na vile. Ngazi mbili za serikali zinapaswa kukamilishana na sio moja kuwa chini ya nyingine,” akasema.

Na ili kuimarisha ugatuzi, viongozi hao wamesema watawasilisha mapendekezo kwa Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano ili kuongezwe kwa mgao wa rasilimali kwa kaunti kutoka asilimia 15 hadi 35.

Aidha, Kinara wa Azimio amesema kamwe hawakubaliani na ubinafshisaji wa bandari ya Mombasa akisema hatua hiyo ya serikali ya Kenya Kwanza ni kizungumkuti kilichozingirwa na siri nyingi na malengo yasiozingatia mwananchi wa kawaida.

“Malengo ya Kubinafsishwa kwa Bandari ya Mombasa na Kenya Kwanza bado ni kitendawili. Tumesikitishwa na uamuzi wa Bandari kubinafsishwa bila kushirikisha umma na kuhusika kwa Serikali ya Kaunti ya Mombasa,” akasema Bw Odinga.

Ingawa hivyo, Rais Ruto alikuwa amesema mapema Ijumaa kwamba bandari ya Mombasa haitabinafsishwa.

Rais Ruto amekanusha kwamba serikali inataka kubinafsisha bandari ya Mombasa.

  • Tags

You can share this post!

Maigo azikwa nyumbani Amasago uchunguzi wa mauaji yake...

Soshiolaiti Vera Sidika aduwaza mashabiki kudai bidhaa zote...

T L