• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
Ruto akubaliana na IEBC, Raila apinga

Ruto akubaliana na IEBC, Raila apinga

NA CHARLES WASONGA

WAGOMBEAJI wakuu wa urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, William Ruto na Raila Odinga jana walitofautiana hadharani kuhusu mfumo wa kuwatambua wapiga kura siku ya uchaguzi mkuu.

Katika mkutano wa wagombea urais na wakuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika mkahawa wa Windsor jana, Dkt Ruto alikubaliana na pendekezo la tume hiyo kwamba sajili ya kieletroniki inatosha kuwatambua wapiga kura Agosti 9.

Lakini Bw Odinga alishikilia kuwa IEBC inafaa kuruhusu matumizi ya mfumo mbadala wa sajili ya daftari endapo mitambo ya kielektroniki itafeli kwa sababu moja ama nyingine.

“Ningependa kufafanua kuwa sisi katika Kenya Kwanza hatuna shida yoyote na uamuzi wa IEBC wa kutumia sajili ya kielekroniki. Tunaamini kuwa sajili hii ndio inafaa kwa sababu itahifadhi maelezo yote ya mpiga kura kwa njia sahihi,” akaeleza Dkt Ruto.

Kambi ya Bw Odinga nayo ilishikilia kuwa sehemu ya 44A ya Sheria ya Uchaguzi inahitaji IEBC iweke mfumo mbadala wa kuwatambua wapiga kura.

Wakili Paul Mwangi kwa niaba ya Bw Odinga alisema katika uchaguzi mkuu wa 2017 jumla ya wapiga kura 2.5 milioni walitambuliwa kwa kutumia sajili ya daftari baada ya mitambo ya kielektroniki (KIEMs) kupata hitalafu.

“Wengi ni wale ambao hawangeweza kutambuliwa kupitia mitambo ya KIEMs kutokana na hitalifu kwenye alama za vidole vyao. IEBC haijatoa hakikisho kwamba changamoto kama hizi hazitokea tena Agosti 9,” akaongeza.

Kwa upande wake, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Agano David Waihiga Mwaure alikubaliana na uamuzi wa IEBC wa kukumbatia matumizi ya sajili ya kielektroniki.

“Tuko katika enzi ambapo teknolojia inatumika katika nyanja mbalimbali za maisha. Sioni kwa nini tusitumie teknolojia katika chaguzi zetu,” akaeleza.

Mgombea urais wa chama cha Roots, Profesa George Wajackoyah, ambaye alikuwepo katika mkutano huo, hakutoa kauli yoyote kuhusu suala hilo.

Awali, Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein Marjan alitetea aumuzi wa IEBC kutumia sajili ya kidijitali pekee akisema matumizi ya sajili ya daftari katika chaguzi zilizopita yalitoa mwanya kwa maafisa walaghai kufanya hila katika upigaji kura.

“Ni rahisi daftari kutumiwa na maafisa wa kusimamia uchaguzi kuendesha hila kwa manufaa ya mgombeaji fulani. Hali hii hutokea katika maeneo ambako hamna waangalizi,” Bw Marjan akasema.

“Katika uchaguzi mkuu wa 2017, kulitokea visa ambapo baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi na makarani walishirikiana kupiga kura kwa kutumia nambari ya vitambulisho vya wapiga kura ambao hawakujitokeza. Hii ndio maana baadhi ya vituo viliandikisha kiwango cha asilimia 98 au hata 99 cha wapiga kura waliojitokeza,” akaongeza.

HOFU

Bw Marjan aliondoa hofu ya mrengo wa Azimio kwamba huenda wapiga kura fulani wakazuiwa kushiriki uchaguzi kwa kukosa kutambuliwa kielektroniki.

“IEBC imenunua mitambo ya kutosha ya KIEMs ambapo kila moja ya wadi 1,450 nchini itakuwa na mitambo sita ya ziada. Mitambo hiyo itatumika endapo ile ya awali itakumbwa na hitalafu,” akasema.

“Kwa wapiga kura ambao alama zao za vidole zina hitalafu au hata hawana mikono, makarani watatumia nambari zao za vitambulisho kuwatambua. Watafanya hivyo kwa kubonyeza nambari hizo ndani ya KIEMs,” Bw Marjan akaeleza.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema tume hiyo iko huru kutoa ufafanuzi kwa wadau wote kuhusu masuala ya uchaguzi.Kuhusu shinikizo za mrengo wa Kenya Kwanza kwamba tume hiyo iadhibu wanasiasa waliochochea fujo katika mkutano wake uwanjani Jacaranda jijini Nairobi mapema mwezi huu, mwenyekiti huyo alisema IEBC haina mamlaka ya kuchukua hatua kama hiyo.

“Mikono yetu imefungwa na uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu kesi iliyowasilishwa na Mbunge Mwanamke wa Murang’a Sabina Chege,” akasema Bw Chebukati.

  • Tags

You can share this post!

Gikaria, Arama, Ngunjiri wahojiwa kuhusu genge la...

Kenya Kwanza yadai bandari zote nchini zimeuzwa kwa Dubai

T L