• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 6:50 AM
Ruto arushia wanawake chambo kwa ahadi ya kuwapa nusu ya mawaziri

Ruto arushia wanawake chambo kwa ahadi ya kuwapa nusu ya mawaziri

VALENTINE OBARA NA WINNIE ATIENO

NAIBU Rais William Ruto, amerushia chambo wapigakura wa kike kwa kuahidi kuwatengea nusu ya idadi ya mawaziri endapo atashinda urais katika uchaguzi ujao.

Hatua hiyo ya Dkt Ruto imejiri wakati ambapo mpinzani wake Raila Odinga anajizolea sifa kwa kuteua mwanamke, Bi Martha Karua awe mgombea mwenza wake.

“Serikali yetu itagawa wizara kati ya wanawake na waume nusu kwa nusu,” akasema Dkt Ruto alipokuwa akizungumza Jumatano katika mkutano wa muungano wake wa Kenya Kwanza jijini Mombasa.

Aliahidi pia kuhakikisha kuna usawa wa kijinsia inavyohitajika Kikatiba katika afisi zote za serikali.

Wanasiasa wengi wanaowania urais na ugavana mwaka huu waliamua kuteua wagombea wenza wa jinsia tofauti na yao, katika hatua inayoonekana kulenga kuvutia idadi kubwa ya wapigakura wa kike.

Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, alikosoa hatua ya Bw Odinga kwamba mbali na kuwa mgombea mwenza, Bi Karua ameteuliwa pia kuwa waziri wa haki endapo Azimio itaunda serikali ijayo.

Bw Kingi alinukuu sehemu 147(4) ya Katiba kuhusu majukumu ya Naibu Rais, ambayo inasema naibu rais hatakubaliwa kusimamia afisi nyingine yoyote ya umma.

“Kama wewe ni rais, ukiapishwa unaapa kulinda Katiba lakini hiyo ni kumaanisha unajua Katiba inasema nini. Karua alitangazwa atakuwa mgombea mwenza na tukaambiwa mbali na kuwa naibu rais, atakuwa pia waziri wa haki. Katiba yasema nini?” akasema.

Hata hivyo Azimio inayoongozwa na Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, huwa imeashiria uwezekano wa kufanyia marekebisho Katiba endapo itaunda serikali ijayo.

Dkt Ruto alikuwa ameandamana na viongozi mbalimbali wa vyama tanzu vya Kenya Kwanza, akiwemo Gavana wa Machakos, Alfred Mutua (Maendeleo Chap Chap), Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria (Chama Cha Kazi) miongoni mwa viongozi wengine.

  • Tags

You can share this post!

Majonzi mshambuliaji akiwaua wanafunzi 19

RB Leipzig wapepeta Freiburg kupitia penalti na kutawazwa...

T L